Wednesday, 24 April 2013

KUMFUATILIA MPENZI WAKO NI UJINGA, KWA NINI USIMUACHE TU?

Ndugu zangu, katika mapenzi wapo waliodondokea kwa watu pasua kichwa. Unamkuta mwanaume yuko na msichana ambaye anaonesha dhahiri hajatulia au mwanamke anakuwa na mwanaume ambaye ni kiwembe.

Katika mazingira haya penzi lazima liwe chungu zaidi hata ya shubiri na watu wa sampuli hii suluhisho ni kuwaacha na si kuendelea kuwa nao wakati wanatutibulia maisha yetu.
Haipendezi kuwa na mpenzi ambaye anakufanya umfuatilie kila mara kwa sababu unaamini anakusaliti. Kufuatiliana, kuchunguzana kwa wapenzi kwa kweli haipendezi, ninachoona ni kwamba, kama humuamini bora umuache kuliko kujipa kazi ya kumfuatilia kila wakati badala ya kufanya mambo mengine ya msingi.
 Ninachotaka kukiweka wazi leo ni kwamba, ukishaingia kwenye uhusiano na mtu ambaye moyo wako umempa nafasi, mpende, muamini na weka akilini mwako kwamba, ametulia na hawezi kukusaliti licha ya kwamba kinyume chake pia ni sawa. Hiyo itakusaidia wewe kuendelea kuishi maisha ya furaha yasiyokuwa na presha.
Hivi ni wanaume wangapi ambao wake zao wanatoka nje ya ndoa lakini waume zao hawajui na wanawaamini sana? Ni wanawake wangapi ambao waume zao ni viwembe kwelikweli lakini wake zao wanawaamini kupindukia? Unadhani ni kwa nini? 
Kama hujui ni kwa nini, basi leo tambua kuwa hiyo imetokana na kuwepo kwa uaminifu uliopitiliza ambao humfanya mtu ahisi hawezi kusalitiwa asilani.
 Tutambue tu kwamba, katika  maisha ya kimapenzi kuna kitu kuridhika. Unapokuwa na mtu ambaye anakupa kila aina ya furaha maishani mwako bila kuonesha tabia zozote zinazokutia mashaka juu ya penzi lake, huyo mpende, mheshimu na muamini. 
Hata kama kuna uwezekano wa yeye kuwa anaficha makucha yake na kuyachomoa pale anapokuwa mbali na wewe, kwa sababu huna uhakika na hujawahi kumuona, chukulia kwamba yeye ni msafi kisha yaache maisha yenu yaendelee kuwepo.
  Nasema hivyo kwa sababu, tukianza kufuatiliana na kuchunguzana, hakuna ambaye ni msafi kwa asilimia mia moja. Kila mtu anajiamini mwenyewe lakini huwezi kuiamini nafsi ya mwenzako kwa asilimia zote.
Ndiyo maana nikasema, unapoingia katika uhusiano na mtu ambaye umetokea kumpenda sana, ongea na moyo wako! Moyo wako ndiyo utakueleza kama mpenzi wako ni muaminifu ama siyo.
Ukiona dalili za kwamba ni tapeli wa mapenzi, usimng’ang’anie eti tu kwa sababu umekufa kwake, muache! Nasema muache kwa sababu, kutokuwa muaminifu ni ishara tosha kwamba hana mapenzi ya kweli kwako na ukiendelea naye atakupa kazi ya wewe kumchunga, una muda huo?
Tatizo tulilonalo wengi wetu ni kutokuwa tayari kuwaacha wale ambao tumetokea kuwapenda sana bila kujua kwamba unaweza kumpenda mtu lakini yeye akawa hana mapenzi na wewe bali anapita tu. 
Ifike wakati basi tukubaliane na uhalisia kwamba, unapoona uliyenae anakuzingua, yupo mwingine mwenye penzi la dhati kwako anayesubiri umuache huyo uliyenaye ili awekeze penzi lake kwako.

Nimesema mengi sana lakini mwisho naomba niseme yafuatayo. Mapenzi ya siku hizi usipoangalia yanaweza kukufanya ukachanganyikiwa. Hii ndiyo inayosababisha baadhi ya watu kufikia hatua ya kusema hawahitaji wapenzi. Kwa nini? Kwa sababu kila uhusiano wanaoingia wanakutana na usanii.
Elewa tu kwamba, una haki ya kupenda na kupendwa, ukishampata yule unayedhani atayafanya maisha yako kuwa ya furaha, mpende kwa dhati na muamini kwamba hawezi kukusaliti.
Lakini la kuzingatia zaidi ni kwamba, kuchunguzana na kufuatiliana siyo utaratibu mzuri wa maisha ya kimapenzi. Kumbuka ukimchunguza sana bata huwezi kumla.

No comments:

Post a Comment