Monday, 22 April 2013

MIZOGA YA NGURUWE YAGEUZWA KITOWEO


UAMUZI wa Serikali kuzuia biashara ya nyama ya nguruwe, kutokana na mlipuko wa homa ya nguruwe, umesababisha biashara ya mzoga wa mnyama huyo kukua tena kwa faida kubwa. Uchunguzi wa gazeti hili, umebaini mzoga wa nguruwe unauzwa kwa bei nafuu. Nyama ya mzoga huo iliyotayarishwa, imekuwa ikiuzwa kwa bei sawa na ya nguruwe ambaye si mzoga.
“Biashara ni nzuri namshukuru Mungu kwani mzoga wa nguruwe tunanunua kwa kati ya Sh 50,000 na Sh 70,000, kulingana na uzito wake, awali nguruwe hai alikuwa akiuzwa hadi Sh 200,000 kulingana na uzito wake.
“Sasa faida inakuja pale unapokaanga na kuuza mzoga huo kwa bei ile ile ya awali ya Sh 4,000 kwa kilo,“ alisema mmoja wa wafanyabiashara hao. Biashara hiyo haramu imeendelea kwa kificho, huku wanunuzi na wauzaji wakijua athari yake kiafya kwa binadamu na kwa kutambua athari hiyo, sasa nyama yake inaitwa ’maziko saa nane.’
Majina mengine ya nyama ya mnyama huyo, kabla ya biashara ya mizoga yake kuibuka, ni kitimoto, mdudu, kondoo au mbuzi katoliki na mkuu wa meza.
Wauzaji hawali Baadhi ya mashuhuda wa biashara hiyo, ambao hawakupenda kutajwa gazetini, wamedai kwamba baadhi yao huchinja nguruwe ambaye nyama yake huchanganywa na mzoga uliotokana na nguruwe waliokufa wa ungonjwa huo wa homa ya nguruwe.
Wauzaji wengine waliozungumza na gazeti hili, wamekiri kuwa wao na familia zao hawali kabisa nyama hiyo, kwa kuhofia madhara yanayoweza kuwapata kiafya. Uchunguzi umebaini kuwa baadhi ya wafugaji walilazimika kuuza mizoga baada ya nguruwe zizi zima kufa.
“Mie najuta, nilipuuza masharti nikamuazimisha jirani yangu dume la mbegu kwa muda kwa kuwa majike yake yalikuwa kwenye joto. Sasa aliporudisha tu, baada ya siku mbili dume hilo na nguruwe wote wanane zizini walikufa na kuniingizia hasara ya zaidi ya Sh milioni 2.5.

Nakiri kuwa mizoga hiyo nimefanikiwa kuiuza kwa bei ya kutupa ya kati ya Sh 60,000 na 80,000 kwa kila mmoja kulingana na uzito wake,“ alisema.
Hivi karibuni Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga ilizuia biashara ya nyama ya nguruwe na kuweka katika karantini tarafa tano, kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa homa ya nguruwe.
Tarafa zilizowekwa chini ya karantini ni Laela, Mwimbi, Matai, Mpui na Kasanga katika mwambao wa Ziwa Tanganyika. Karantini hiyo ilitangazwa na Daktari wa Mifugo na Mkaguzi wa Mifugo, Dk Seleman Kataga ambaye alionya kwamba kuanzia sasa hakuna ruhusa ya kuondoa, kuingiza, kupitisha au kuchinja mifugo hao katika maeneo yaliyo chini ya karantini.
Vilevile alipiga marufuku usafirishaji wa nguruwe kutoka kijiji kimoja hadi kingine, ndani na nje ya maeneo hayo.
“Biashara yoyote ya nguruwe na mazao yake ikiwemo nyama, mbolea, manyoya, mifupa, ngozi na vyakula vya kusindikwa, imepigwa marufuku iwapo itafanyika bila idhini ya kibali cha maandishi cha daktari mwenye dhamana,“ alisisitiza. Katika tarafa hizo zilizokumbwa na mlipuko wa homa hiyo, nguruwe 4,181 wamekufa. Kabla ya ugonjwa huo, kulikuwa na nguruwe 28,630 na sasa wamebaki 24,449.
Alitaja changamoto kadhaa zilizojitokeza katika kukabiliana na ugonjwa huo, kuwa ni pamoja na uelewa mdogo wa wananchi juu ya athari za ugonjwa huo kiuchumi na jinsi unavyoweza kusambaa kwa kasi.
Ugonjwa huo unadaiwa kuingia wilayani humo kwa mara ya kwanza Julai 2011 kupitia nguruwe hai walioingizwa katika kijiji cha Chombe, kata ya Kaoze kutoka kata ya Chilulumo wilayani Mbozi mkoa wa jirani wa Mbeya.
Akizungumza kwa njia ya simu mwishoni mwa wiki, Ofisa Mifugo na Uvuvi wa Halmashauri ya Sumbawanga, Denis Magala, alisema homa hiyo haina madhara kwa binadamu.
Alisema inapomshambulia nguruwe, haina tiba wala chanjo na isitoshe unasababisha hasara kubwa kwa mfugaji, kwani unaenea kwa kasi na kuua nguruwe wote walioshambuliwa na ugonjwa huo.
Ndiyo maana biashara yoyote ya nguruwe na mazao yake ikiwemo nyama, mbolea , manyoya , mifupa , ngozi na vyakula vya kusindikwa imepigwa marufuku ili ikiwa ni jitihada za makusudi za kudhibiti na ugonjwa huo, “ alisisitiza


No comments:

Post a Comment