Tuesday, 23 April 2013

SIFA MUHIMU ZA KUZINGATIA UTAFUTAPO MTU WA KUISHI NAE...





MARA nyingi vijana hupata taabu sana
katika suala la kuchagua mchumba.
Vijana wa kiume ndio hasa hupata
wakati mgumu zaidi kwani jamii
imewapa wajibu wa kuanzisha
mazungumzo yahusianayo na mapenzi. Hata hivyo, vijana wa kike
nao wanao wajibu wa kuchagua ili
kuhakikisha kuwa hawaanguki
mikononi mwa mabazazi wa
kuwalaghai na kuwatumia kwa raha
za miili yao kisha kuwaacha kwenye mataa. Ni jambo la kawaida kwa vijana walio
wengi, wawe wa kike au wa kiume,
kuangalia sura na mwonekano wa
mtu. Lakini unapotafuta mchum ba
kwa malengo ya kuishi naye maisha
yako yote kama mume na mke haipendezi kuangalia tu mwonekano,
maana Waswahili husema si kila
king’aacho ni almasi. Kwa sababu
hiyo, hapa yatabainishwa mambo
muhimu ya kuangalia na kuzingatia
katika suala hili. 1. UADILIFU Pamoja na sifa zote za uzuri
zinazoweza kubainishwa na
kufanywa kuwa vigezo vya uzuri wa
mwanamke na mwanaume na hata
zikatumiwa kumpata Miss au Mr
Tanzania, sifa kuu impasayo mtu anayefaa kuwa mchumba kuwa nayo
ni sifa ya uadilifu. Mtu anapokuwa na uadilifu (pengine
uaminifu), maana yake ni kwamba
tabia ya mtu huyu anayoionesha nje
ndiyo tabia yake halisi na anapofanya
jambo jema analifanya kwa roho yake
na si kwa unafiki. Mtu anapokuwa mwadilifu
ataheshimu maadili na kufanya wema,
hata pale inapokuwa rahisi kwa
wengine kukengeuka na kufuata njia
za mkato ambazo mara nyingi si za
halali. Mtu mwadilifu pia huwa na sifa za
ukweli na kujitolea kuwasaidia watu
wengine bila kujali faida – haya yote ni
mambo muhimu ambayo mtu mwenye
kuwa nayo huwa na msingi wa ujenzi
wa uhusiano imara na wa kudumu. Watu wanaoweza kujivunia furaha ya
kweli katika maisha yao ya ndoa, ni
watu ambao wamekutana wote
wakiwa na sifa ya uadilifu ambayo
hujumuisha mambo mengi. Zipo ndoa nyingi zenye furaha ya
bandia. Furaha hii mara nyingi
hutokana na ridhiko la kimwili
alipatalo mtu kutokana na kukidhiwa
kwa mahitaji yake ya kimwili
yanayohusiana na haki za msingi za binadamu – yaani chakula, mavazi na
malazi. Lakini furaha ya kweli ya
maisha ya ndoa, watu hawaipati
isipokuwa katika uhusiano ambao
wenza wamethibitishana kuwa
waadilifu. 2. HEKIMA Mtu mwenye uadilifu wa kweli, mbali
na kuwa mwema kwa mwenzake, pia
huhakikisha anakabiliana kwa busara
na hekima na matatizo yote
yanayoweza kusababisha kuyumba
kwa uhusiano, hususan yale yaliyo nje ya uwezo wake. Uzoefu unaonesha kuwa wapenzi,
hususan wanandoa walio katika
uhusiano wa muda mrefu
wanaoendelea kufurahia unyumba
wao si wale ambao walipendana kwa
mvuto na wala hawana mambo mengi ya asili yanayowaunganisha kuliko
wale wanaotengana. Lakini la muhimu
ni kwamba watu hawa huwa
wamejifunza jinsi ya kukabiliana kwa
hekima na matatizo yanayojitokeza,
hususan yale yanayotokana na tofauti zao kimtazamo. Ukiachilia mbali sifa ya uadilifu, watu
hawa huwa wamejifunza kukabiliana
na matatizo kuhusiana na uzazi na
ulezi wa watoto, uhusiano na ndugu,
jamaa na marafiki, suala la ngono,
fedha na maisha ya unyumba kwa ujumla. Habari njema ni kwamba uadilifu na
hekima ni mambo ambayo mtu yeyote
anaweza kujifunza na kisha kufanyia
kazi. Ndiyo maana wanandoa
hufundishwa kabla ya ndoa na hata
wanapokuwa tayari wameoana huendelea kuhudhuria semina za
kidini na kijamii kwa ajili ya
kujiimarisha. Kwa hiyo, kama mume/mke wako
mtarajiwa anaonekana kuwa na
utayari wa kujifunza kuhusiana na
jinsi ya kuishi na mtu wa jinsia
nyingine, ana nafasi kubwa ya kuwa
mke/mume mzuri baadaye. 3. UPOLE Mfalme Suleiman katika mojawapo ya
semi zake za hekima alisema
mwanamke mpumbavu huibomoa
nyumba yake kwa mikono yake.
Yamkini ndivyo ilivyo pia kwa
mwanaume mpumbavu, maana upumbavu haujengi. Siku zote kitu kinachovunja uhusiano
wa kindoa si makombora ya nyuklia,
bali ni ulimi. Kwa kadri mtu
anavyoutumia ulimi wake anaweza
kuijenga au kuibomoa nyumba yake. Katika kumwangalia mtu ambaye
unaweza kujenga naye nyumba ya
kudumu, ni vema kumchunguza na
kuhakikisha kuwa si mtu mwenye
kupenda kurefusha maneno, maana
hakika huyu atasababisha ugomvi mara kwa mara na uhusiano
hautadumu. Wapo watu ambao ndoa zao zina sifa
ya ugomvi na karibu kila mtu
anafahamu na hata wamekuwa kero
kwa ndugu, jamaa na majirani zao,
mara kwa mara wakiwaamsha watu
usiku wa manane wakitafuta suluhu. Mara nyingi wanaume ndio huanzisha
ugomvi, lakini ugomvi huwa na nguvu
zaidi kama mwanamke ni msemaji.
Dawa ya kuzuia ugomvi usiokuwa na
mpango ni kupunguza maneno na
kuepuka kutafuta ushindi katika ubishi. Lakini kinga ya tatizo hili ni
kuepuka kujiingiza katika uhusiano
na mtu ambaye umejihakikishia kuwa
si mwingi wa maneno. Bahati nzuri, jamii huwatambua
wanawake/wanaume ambao
wanaweza kuwa wake/waume bora
baadaye kwa hiyo ni wajibu wa
mtafutaji kuhakikisha kuwa anafanya
uchunguzi wa kina kabla ya kujitosa kwa mtu ambaye baadaye
atamtaabisha. Mwanandoa aliyeifahamu vema dhana
ya ndoa – kwamba ni maisha ya
kuvumiliana na kuchukuliana,
hufahamu ni wakati gani wa kusema
na wakati gani wa kukaa kimya. Mtu
huyu pia hufahamu njia nzuri na salama ya kujiondoa kwenye tatizo
anapoona mwenzake anaelekea
kubaya, ili hatimaye uhusiano wao
uendelee kuwa salama japo wao
wanaweza kuwa wamekwaruzana. Mtu huyu mwenye upole hujiweka
katika mkao wa upatanishi na
huhakikisha kuwa kila mjadala mkali
unapita na kumalizika salama. Ni wazi
kuwa katika kutafuta, kama
hukukurupuka, utamwona mtu mwenye hulka hii – upole. 4. MVUTO Hisia za mvuto wa kimapenzi ni
muhimu katika kujenga uhusiano. Mtu
mmoja akauliza, ni yupi bora – yule
anayenivutia sana au yule
anayenipenda sana? Maisha ni ya
ajabu sana. Huwa inatokea kuwa mtu unayevutiwa naye sana yeye havutiwi
nawe, bali anavutiwa na mwingine
ambaye naye hana mpango naye! Haya ndiyo maisha. Uzoefu unaonesha
kuwa asilimia kubwa ya watu walio
katika ndoa hawajawaoa/kuolewa na
watu waliokuwa wakiwapenda sana
enzi za ujana wao, au wale waliotimiza
ndoto za ujana wao. Bahati njema miongoni mwa wanandoa hawa
wapo wale wenye ndoa imara sana. Mvuto wa kimapenzi ni muhimu sana,
lakini watu husema maji yakisema
usininywe yajibu kuwa wewe pia
huna kiu nayo. Japo inaweza
kuonekana kama ni aina ya ‘sizitaki
mbichi hizi’ lakini si vema kujisumbua na mtu asiyekupenda. Badala ya kujihangaisha na mtu
asiyekupenda, kaa chini na umsubiri
anayekupenda hata kama huhisi
kuvutiwa naye sana. Baadaye
utamzoea na maisha yatakuwa
mazuri, kisha utajiuliza baadaye yule aliyekuringia alikuwa na nini cha
ziada? Lakini iwapo mambo mengine yote
yatakwenda sawa, ni vema na
muhimu kabisa kuhakikisha kuwa
mtu unayepanga kuwa naye maisha
yako yote ni mtu anayekuvutia kimwili
na kiakili, maana vinginevyo unaweza kupata sababu ya kukidhi kiu yako
nje – jambo ambalo si maadili mema
katika ndoa na maisha. NI MUHIMU KUWA MAKINI Katika nyakati za ujana, watu wengi
hubabaishwa kwa mengi. Vijana wa
kiume hubabaishwa na sura,
maumbile na pengine rangi na
kusahau mambo muhimu yaundayo
orodha ya sifa za mke mwema. Kwa upande wao, vijana wa kile pia
waweza kubabaishwa na pesa,
maumbile, sura, utanashati, umaarufu
au kuchoshwa na shinikizo la umri,
hivyo kujikuta wakijitumbukiza kwa
wanaume wasio na sifa za waume wazuri. Lakini tukirejea kwenye msemo wa
zamani kuwa uzuri si hoja bora tabia,
ni wazi kuwa tutafikia mahali
tutajenga mahusiano imara na
yasiyotikiswa na sunami zozote za
kimaisha. Ilimradi tu uhakikishe kuwa mtu mwenyewe anakupa mvuto
kimapenzi, maana vinginevyo
kutakuwa hakuna maana.

No comments:

Post a Comment