Monday, 22 April 2013

Tambua Madhara ya Sindano za uzazi wa mpango....



UTAFITI umebaini kuwa sindano za uzazi wa mpango zinachangia kasi ya maambukizi ya virusi vya Ukimwi,kwa kuwa zina vichocheo vingi ambavyo vinahuisha virusi vya Ukimwi katika nyumba ya uzazi na kuvipa nguvu ya kusambaa. Inaelezwa kuwa walio katika hatari zaidi ya maambukizi hayo ni wanawake walioko katika ndoa kwa kuwa ndiyo wanaotumia zaidi sindano hizo. Utafiti huo uliofanywa na wanasayansi wa Marekani na kuripotiwa na gazeti la The Guardian la Uingereza, umebaini kuwa wanawake wanaotumia sindano za uzazi wa mpango wapo katika hatari mara mbili ya kupata maambukizi ya Ukimwi au kuwaambukiza wenzi wao, kuliko wengine. Katika utafiti huo uliofanywa katika nchi saba zinazoendelea barani Afrika ikiwamo Tanzania, wanasayansi hao kutoka Chuo Kikuu cha Washington,walipendekeza ushauri zaidi utolewe kwa wanandoa kabla mtu hajajiingiza kwenye matumizi ya sindano kama njia ya kupanga uzazi. Utafiti huo ulifanyika kwa wanandoa 3,790 kutoka nchi za Tanzania, Afrika Kusini, Zimbabwe, Uganda, Kenya, Rwanda na Botswana, ulichapishwa kwa mara ya kwanza katika Jarida la Afya la Lancet kabla ya kunukuliwa na gazeti la The Guardian. Utafiti umebaini pia kuwa zaidi ya wanawake 140 milioni duniani,wanatumia njia mbalimbali za uzazi wa mpango, huku wanandoa wengi katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, wanaoishi na VVU wakichagua kutumia sindano kama njia ya kuzuia mimba zisizotarajiwa. Wanasayansi hao walikusanya taarifa kati ya wanandoa 3,790 ambao mmoja wao anaishi na VVU na mwenza wake akiwa hana maambukizo. Aidha wanawake ambao wanaishi na VVU na wanatumia sindano hizo pia,walikuwa katika hatari zaidi ya kuwaambukiza wenzi wao. Vipimo vilionyesha kuwa sindano hizo ambazo zina vichocheo ambavyo vinavipa nguvu virusi ndani ya nyumba ya uzazi (cervix). Imeelezwa kuwa njia za uzazi wa mpango zinazohamasishwa zaidi na kupendwa zaidi na wanawake ni sindano, ambazo wanawake wanasema kuwa zinadumu kwa muda mrefu na zinaweza kutumika bila ya ruhusa au mume kufahamu. Kiongozi mkuu wa utafiti huo Renee Heffron wa Chuo Kikuu cha Washington,alisema sindano za uzazi wa mpango zina vichocheo vingi ambavyo huvihuisha vijidudu vya Ukimwi katika nyumba ya uzazi na kuvipa nguvu ya kusambaa. Mwanasayansi mwingine, Charles Morrison wa Kituo cha Afya cha Durham, nchini Marekani alisema uhamasishaji wa matumizi ya sindano za uzazi wa mpango unachochea maambukizi zaidi katika nchi za Jangwa la Sahara. Na ameshauri nchi zinazoendelea kuacha matumizi ya njia za uzazi wa mpango zenye vichocheo, ili tupunguze maambukizi. Alivitaka vituo vya afya vitoe ushauri kwa wanawake kutumia kondomu badala ya sindano au vidonge. Mara nyingi watu wanaotumia vidonge, wengi si wanandoa, mtu anayemeza vidonge vya kuzuia mimba anaogopa zaidi mimba si Ukimwi. Huchoche hamu ya mapenzi. Mfamasia katika Kitengo cha Dawa kwa watu wanaoishina VVU katika Hospitali ya Amana Christopher Masika,alisema anaafiki kuwa sindano na hata vidonge vinaweza kuwa ni sababu inayochochea maambukizi kwa sababu ya uhuru. Kwa sababau Mtu anapotumia sindano huwa huru kufanya ngono,kwa kuwa hana hofu ya mimba hicho kinaweza kumfanya apate maambukizi kwa urahisi, tofauti na anapotumia kondomu. Amesema wapo baadhi ambao wakitumia sindano hizo vichocheo vinawafanya wapate hamu zaidi ya kufanya mapenzi, hivyo huanza kutembea na wanaume wengine.

No comments:

Post a Comment