JOSEPH Owino amesema ataurudisha ufalme wake Simba, suala ambalo limeungwa mkono na Kocha Mkuu wa timu hiyo, Abdallah King Kibadeni ambaye amekubali uwezo wa beki huyo wa Uganda.
Lakini cha kufurahisha zaidi, beki huyo aliyetokea URA ameikubali kombinesheni yake na Adam Miraji aliyecheza naye nafasi hiyo katika mechi yake ya kwanza dhidi ya SC Villa ya Uganda waliposhinda 4-1 katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Akiwa Simba atacheza nafasi hiyo ya beki wa kati pamoja na Mrundi Kaze Gilbert watakaosaidiwa na wazawa Adam na Rahim Juma ama Shomari Kapombe ambaye yupo katika majaribio Ulaya.
Owino alisema: “Naipenda Simba na ndiyo maana nimerudi kwa mara nyingine na mambo yatakuwa mazuri zaidi kwa sababu nitajituma kadri niwezavyo kuifanyia makubwa.
“Hakuna asiyefahamu uwezo wangu, maumivu ya goti yaliyokuwa yananisumbua yamepona na sina tatizo jingine lolote, kilichopo ni kazi tu.
“Simba ipo vizuri na nimefurahia kombinesheni tulicheza na yule dogo beki wa kati, anajitahidi sana, msikivu unapomwelekeza uwanjani na anajituma na pia bado mdogo sana, nilivyomwona ni mzuri na atakuja kuwa tishio baadaye,”alisema Owino ambaye ana shahada ya biashara.
“Sijaona tatizo lolote kwenye kikosi cha Simba na naamini wakija wengine ambao hawajafika Simba itakuwa vizuri, mambo mengine ni juu ya kocha,”alisema Owino.
Kibadeni alimzungumzia, Owino na kusema: “Hakuna asiyemfahamu Owino kwani kila mmoja anajua ni beki bora na ndivyo ilivyo, ni mzoefu na anafanya vizuri.”
Owino ataungana na wachezaji wengine wa kimataifa kutoka Burundi straika, Amis Tambwe na beki wa kati Kaze Gilbert ambao wanatarajiwa kufika wiki hii.
Katika mechi ya Jumamosi, mabao ya Simba yalifungwa na Betram Mombeki mawili, Jonas Mkude na William Lucian ‘Gallas’.
No comments:
Post a Comment