Serikali ya Rwanda imetoa tamko linaloonyesha kutoielewa kauli ya Rais Jakaya Kikwete, iliyoamuru wahamiaji haramu kuondoka nchini, hali inayoonekana kukwepesha hoja.
Rwanda kupitia waziri wake wa Mambo ya Nje, Louise
Mushikiwabo, ilikaririwa ikieleza kwamba hawatajibu mapigo agizo la
Rais Jakaya Kikwete ya kuwataka Wanyarwanda wote waliolowea Magharibi
mwa Tanzania kuondoka haraka.
Mushikiwabo alisema wako tayari kuwapokea na
kuwalinda wote waliofukuzwa Tanzania kwa kisingizio kuwa ni wahamiaji
haramu, akieleza kwamba anasikitishwa kwa kuwa Tanzania haikufanya
jitihada yoyote kuwasiliana na Rwanda kuhusu suala hilo kabla ya
kuchukua uamuzi huo.
“Ni uamuzi ambao umeshachukuliwa,
hatukushirikishwa kwa namna yoyote na jukumu letu kama serikali na taifa
ni kuwahakikishia ulinzi wote wanaokuja, na hili ndilo suala
tunalolishughulikia kwa sasa,” alisema.
Kwa mujibu wa gazeti la New Times, Mushikiwabo
aliwaeleza waandishi wa habari kwamba agizo hilo la Rais Kikwete pamoja
na ushauri wa kuitaka Serikali ya Rwanda kuzungumza na wanamgambo hasimu
wa FDLR waliopo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), hayatayumbisha
uhusiano imara baina ya Watanzania na Wanyarwanda.
“Sisi si majirani tu, tuna mfungamano imara baina
ya watu wetu pia, tuna mfungamano wa damu, wa kibiashara, na mengine
mengi ya kutufanya tuendelee kuwa pamoja,” alisema na kutumia fursa hiyo
kuwakaribisha Watanzania nchini Rwanda.
Watanzania wanaweza kuishi hapa kwa umri wowote
wanaotaka. Tunawachukulia kuwa ni watu wetu muhimu kwenye fungamano la
Jumuiya ya Afrika Mashariki,” alisisitiza.
Rais Kikwete wakati akihitimisha ziara yake mkoani
Kagera alitoa agizo la kuwataka wanaomiliki silaha kinyume cha sheria
na wahamiaji haramu ama kuondoka au kuhalalisha ukazi wao, huku akitoa
wiki mbili kwa zoezi hilo kutekelezwa, kabla ya kuanza kwa operesheni ya
kuwasaka watu hao.
Kauli hiyo ilitokana na kushamiri vitendo vya
kihalifu katika eneo la Kanda ya Ziwa, Rais hakutaja jina la nchi ya
wahamiaji hao. Kwa ukanda huo Tanzania inapakana na Kenya, Uganda,
Rwanda, Burundi na DRC.
Pia, Rais Kikwete katika hotuba yake ya mwisho wa
mwezi alizungumzia kusikitishwa na kauli za shutuma, kejeli na
udhalilishaji zilizotolewa na Rais Paul Kagame wa Rwanda dhidi yake.
Mvutano baina ya Rwanda na Tanzania ulianza
kuwekwa hadharani Mei mwaka huu, baada ya Rais Kikwete kuishauri Rwanda
kukaa na kuzungumza na FDLR wenye makao yao DRC, hatua ambayo
haikuifurahisha Serikali ya Rwanda.
Wakati Rwanda ikieleza hayo jana Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue alizungumza na gazeti hili, na kutaka majibu ya kauli hiyo ya Rwanda yatolewe na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Mkumbwa Ally alisema kauli
iliyotolewa na Rais Kikwete ilikuwa ni ushauri, kwamba Rwanda wanaweza
kuukubali ama la.
“Kilichomkasirisha Rais Kikwete ni lugha za matusi
zilizokuwa zikitolewa na viongozi wa Rwanda, ila kwa hicho
walichokisema sidhani kama kitakuwa na tatizo kwetu,” alisema Mkumbwa.
Alifafanua kwamba, alipokuwa mkoani Kagera Rais
Kikwete hakutoa agizo la Wanyarwanda kufukuzwa, bali alitoa agizo la
kuanza kwa operesheni ya kuwakamata wahamiaji haramu, wale wanaomiliki
silaha kinyume na taratibu.
“Rais alizungumzia masuala ya jinai ‘Criminal Element’, siyo kuwafukuza Wanyarwanda,” alisisitiza.
Hatutazungumza na FDLR
Waziri wa Mambo ya Nje, Louise Mushikiwabo,
aliendelea kusema sera ya Rwanda kuhusiana na makundi ya aina hiyo, iko
wazi na haitabadilika, kauli ambayo amekuwa akiirudia kila mara na
kuwataka wote wanaofikiria kuhusu Rwanda kuzungumza na FDLR kwa namna
yoyote kusahau wazo hilo.
“Kama umehusika kwa namna yoyote na maangamizi,
wewe utakuwa adui wa kila mtu. Ni wazi kwamba Wanyarwanda wote watakuwa
kwenye majonzi iwapo kwa namna yoyote kutakuwa na mawasiliano ya FDLR,”
alifafanua.
Kundi la FDLR ambalo ni kifupisho cha Democratic
Forces for the Liberation of Rwanda, linaundwa na watu walioshiriki
kwenye mauaji ya kimbari yaliyowalenga watu wa kabila la Watutsi mwaka
1994, na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 800,000 kwa miezi mitatu.
Kundi hilo ambalo limeweka makazi yake mashariki
mwa DRC, linadaiwa kufanya mashambulizi kadhaa yakiwamo ya milipuko ya
mabomu nchini Rwanda, ambapo mwezi uliopita shambulio la aina hiyo mjini
Kigali lilisababisha vifo vya watu watatu na kujeruhi watu kadhaa.
Uhusiano wa kihistoria
Familia za Rwanda zikiwamo zilizoishi Tanzania
tangu miaka ya 1950, zimeelezwa kuwa zimekuwa zikiwasili nchini humo
kupitia mpaka wa Rusumo baada ya agizo la Rais Kikwete kuwataka wawe
wameondoka ndani ya wiki mbili, kabla ya kuanza kwa operesheni rasmi ya
kuwaondoa.
Kwa mujibu wa mamlaka nchini Rwanda, mamia ya
Wanyarwanda waliokuwa wakiishi mkoani Kagera ambako ndiko Tanzania
inapopakana na Rwanda wamekuwa wakirejea kwa wingi, ambapo hadi juzi,
zaidi ya watu 300 walikuwa wameshaorodheshwa kwenye ofisi za Uhamiaji.
No comments:
Post a Comment