WAKATI hatima ya kutiwa saini mkataba wa amani kati ya Serikali ya DRC
na waasi waliosambaratishwa wa M23 ikiwa haijulikana, uhusiano wa
maswahiba wawili wa eneo la Maziwa Makuu, Rais Yoweri Museveni wa Uganda
na Paul Kagame wa Rwanda umetikisika baada ya Museveni kumtaka mwenzake
huyo azungumze na waasi.
Ni ushauri kama huo aliopewa Kagame Mei
mwaka huu na Rais Jakaya Kikwete ukilenga kuleta na kuimarisha amani
Mashariki mwa Congo ndio ulioyumbisha uhusiano kati ya Tanzania na
Rwanda, kabla ya Kikwete kuifafanua na kisha kukutana na Kagame jijini
Kampala, Uganda Agosti mwaka huu.
Kwa mujibu wa mtandao wa AfroAmerica Network, Museveni, baada ya
kurejea kutoka kwenye mkutano wa wakuu wa nchi za SADC na zile za Maziwa
Makuu (IGGLR) huko Pretoria, Afrika Kusini wiki iliyopita, alimpigia
simu Kagame na kumwambia: “Huenda sasa ni wakati muafaka wa kuzungumza
na wapinzani wako wenye silaha.”
Chanzo cha habari cha mtandao
huo kimemnukuu mmoja kati ya viongozi wa juu wa Jeshi la Rwanda (RDF),
akisema Museveni alimwomba Kagame kuzungumza na waasi hao haraka kabla
muda haujapita mara tu Rais huyo wa Uganda aliporejea Kampala Alhamisi
iliyopita.
Mkutano wa pamoja wa wakuu wa nchi za SADC na ICGLR
uliofanyika kuanzia Jumatatu wiki iliyopita chini ya uenyekiti wa marais
watatu, Joyce Banda (Malawi, SADC), Museveni (Uganda, ICGLR) na wa
Afrika Kusini, Jacob Zuma, ulitoa wito kwa M23 kuweka silaha chini. Siku
mbili baadaye waasi hao wanaodaiwa kuungwa mkono na Rwanda, walishindwa
vita na kutangaza kuacha uasi.
Kagame hakuhudhuria mkutano huo, badala yake aliwakilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje, Louise Mushikiwabo.
“Ni
ushauri tu. Nimerejea kutoka kwenye mkutano na SADC uliojadili amani
eneo la Maziwa Makuu. Bahati mbaya inaonekana kwamba karibu viongozi
wote wanaamini kikwazo kikubwa cha amani ni kuwapo kwa waasi wa
Kinyarwanda mashariki mwa DRC.
“Hakika suala hili linapaswa
kuzungumzwa kwa njia moja au nyingine. Na viongozi hao wanaamini kwamba
hili halitatatuliwa bila serikali ya Rwanda kukaa kwenye meza ya
usuluhishi na wapinzani wake wenye silaha. Hata mimi ninaamini hivyo,
huenda wakati umefika kwako kuzungumza nao,” alinukuliwa Museveni
akimwambia Kagame katika mazungumzo ya simu yaliyodumu kwa takriban
dakika 15.
Kagame alijibu: “Sitozungumza na FDLR, washiriki wa mauaji ya kimbari. Never, … , ever. Sitozungumza kamwe na wahalifu.”
Hata
hivyo, inadaiwa Museveni alimkumbusha Kagame kuwa si waasi wote wa
Rwanda walioko DRC ni wanachama wa FDLR au wahalifu na kwamba wapo
anaoweza kuzungumza nao kwa kuanzia.
Baada ya mazungumzo hayo,
Kagame aliitisha mkutano wa dharura na washauri wake wakuu na kuwaeleza
walichozungumza na Museveni na kuongeza:
“Nimekuwa nikiwaambia
mara kwa mara kuwa tuko peke yetu. Hata Yoweri, tuliyemwamini kama
rafiki yetu na mwenzetu anatugeuka! Leo anatuambia hiki, kesho anakwenda
kukutana na viongozi wengine na kutubadilikia.”
Baadaye
akawataka washauri hao kuja na mpango mkakati wa nini cha kufanya wakati
huu Rwanda ikizidi kutengwa na nchi za Afrika na hata za nje ya Afrika.
Mwanzoni
mwa mwezi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry na mwenzake
wa Uingereza walimwonya Kagame kuachana mara moja na ushiriki wake
kwenye machafuko ya mashariki mwa DRC, ikiwa ni mara ya pili ndani ya
mwaka mmoja kwa wakubwa hao kutoa onyo kama hilo.
Wakati hayo
yakiendelea, zipo taarifa kwamba Rais Museveni amepanga kutuma ujumbe
nchini kuja kuzungumzia mustakabali wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC)
baada ya Rais Jakaya Kikwete kuwaambia Watanzania kwamba Tanzania
haijakiuka chochote katika makubaliano ya msingi, ila wenzetu hao ndio
huenda wana ajenda yao.
Kauli ya Kikwete ilihitimisha hali ya
wasiwasi wa Tanzania kujitoa EAC na iwapo ujumbe wa Uganda utakuja,
itakuwa ni mwendelezo wa kilichofanywa mwishoni mwa wiki na Kenya
waliomtuma Waziri wa Mambo ya Nje kuja Dar es Salaam kuweka mambo sawa.
>>>Hali nchini Kenya
Mapema
wiki hii, aliyekuwa Mwanasheria wa Serikali ya Kenya, Amos Wako ambaye
pia ni Seneta wa Bisia alitoa wito kwa Rais Uhuru Kenyatta kuhakikisha
kuwa EAC haisambaratiki, akidai kuwa watakaoumia zaidi ni Wakenya.
Wako
aliyekuwa kwenye mkutano wa hadhara pamoja na Mbunge wa Budalangi,
Ababu Namwumba, alisema wakati jumuiya ya awali ilipovunjika mwaka 1977,
Wakenya wengi waliokuwa wakifanyakazi nje ya nchi ndio walioathirika
zaidi.
“Wapo watu mashuhuri kama Raila Odinga na Kalonzo Musyoka
wanaokubalika ndani na nje ya nchi ambao kama Uhuru anataka wanaweza
kumsaidia kuzungumza na Rais Kikwete wa Tanzania. Hatutaki jumuiya hii
ivunjike, si busara hata kidogo,” alisema Wako.
No comments:
Post a Comment