KATIKA uhusiano wa kimapenzi hakuna kitu kinachouma kama kusikia
mpenzi wako uliyempa nafasi kubwa kwenye moyo wako anatembea na mtu
mwingine.
Licha
ya kwamba ni kitu kinachoumiza sana, bado tumekuwa tukishuhudia baadhi
ya watu wakiwasaliti wenza wao tena wakati mwingine waziwazi.
Aidha, wapo ambao wanafanya usaliti kwa kujificha sana kiasi kwamba wenzao wanaamini hawasalitiwi.
Huko
nyuma utakumbuka nilishawahi kuzungumza kwamba, unapoingia kwenye
uhusiano na mtu ambaye moyo wako umemzimikia, hutakiwi kuwa na mashaka
naye.
Muamini na weka akilini mwako kwamba hawezi kukusaliti. Kwa kufanya hivyo maisha yako yatakuwa ni yenye amani siku zote.
Lakini
wakati ukweli ukiwa hivyo, tumekuwa tukiwashuhudia marafiki, ndugu na
hata majirani zetu ambao tunawaona wametulia wakiwasaliti wenza wao kila
kukicha.
Wapo wake za watu ambao tumekuwa tukiwaamini kuwa wametulia lakini siku moja tunawaona wakiingia gesti na wanaume wengine.
Achilia
mbali hilo, wewe unayesoma makala haya unaweza kuwa na rafiki yako
ambaye unajua fika ana mtu wake lakini unashangaa anampa nafasi mtu
mwingine na wanakuwa wakikutana kwa siri huku wewe ukiambiwa iwe siri
yako.
Binafsi kuna dada mmoja ambaye namheshimu sana, ni jirani yangu
ana mume wake ambaye inaonekana anampenda sana. Yule mume amekuwa na
imani kubwa kwa mkewe kwamba hawezi kumsaliti lakini nimeshawahi kumuona
na wanaume wengine na akanisihi sana nisimwambie mume wake. Na kweli
siri hiyo imebaki moyoni mwangu hadi leo.
Sasa katika mazingira hayo
huwa nakaa na kujiuliza, wale wanaosema wanawaamini wapenzi wao kwa
asilimia zote ujasiri wanaupata wapi? Hata kama ni suala la imani lakini
siyo kwa mazingira tunayoishi sasa na sarakasi za usaliti zilivyo.
Utakuwa
ukijilazimisha kuamini mpenzi wako hawezi kukusaliti lakini kuna wakati
unajiwa na hisia kwamba anakusaliti ila hisia hizo unazipotezea ili
kutojipa vidonda vya tumbo, si ndiyo ee?
Kikubwa nisisitize kwamba
mapenzi ni imani. Ni sawa na kuamini kwamba Mungu yupo licha ya kwamba
hujawahi kumuona. Vivyo hivyo, amini tu kwamba mpenzi wako anakupenda
kwa dhati na hawezi kukusaliti licha ya kwamba kinyume chake pia ni
sawa. Hiyo itakusaidia wewe kuendelea kuishi maisha ya furaha na amani.
Hivi
ni wanaume wangapi ambao wake zao wanagawa penzi nje ya ndoa lakini
waume zao hawajui na wanawaamini kupita maelezo? Ni wanawake wangapi
ambao waume zao ni viwembe kwelikweli lakini wake zao wanawaamini
kupindukia?
Tutambue tu kwamba, katika maisha kuna kitu kuridhika.
Unapokuwa na mtu ambaye anakupa kila aina ya furaha maishani mwako bila
kuonesha tabia zozote zinazokutia mashaka juu ya penzi lake, huyo
mpende, mheshimu na muamini.
Hata kama kuna uwezekano wa yeye kuwa
anaficha makucha yake na kuyachomoa pale anapokuwa mbali na wewe, kwa
sababu huna uhakika na hujawahi kumuona, chukulia kwamba yeye ni msafi
kisha yaache maisha yenu yaendelee kuwepo.
No comments:
Post a Comment