Saturday, 1 February 2014

Vodka inawaua wanaume Urusi

Idadi kubwa ya vifo vya mapema nchini Urusi vinatokana na watu kunywa pombe nyingi , hasa Vodka.
Ripoti hii ni kulingana na utafiti uliofanywa hivi karubini nchini humo.


 


 Wanaume walevi Urusi
Utafiti huo kwenye jarida la Lancet unasema kuwa robo ya wanaume nchini Urusi wanakufa kabla ya kufikisha umri wa miaka 55 na wengi wao wanakunywa sana pombe.
 
Watafiti walichunguza tabia ya ulevi ya wanaume zaidi ya laki moja na hamsini katika miji mitatu ya Urusi kwa miaka kumi.

Pia walitathmini utafiti wa awali kuhusu kiwango cha Pombe walichokuwa wamekunywa wanaume kadhaa kabla ya kufariki.

Utafiti uligundua kuwa idadi ya vifo vilipungua kutokana na matukio ya kisiasa na mabadiliko katika sera kuhusu Pombe.

Mnamo mwaka 1985 chini ya utawala wa aliyekuwa Rais Gorbachev,unywaji pombe uliwekewa vikwazo na hivyo vifo kutokana na ulevi vikapungua.

Kisha baada ya kuporomoka kwa mfumo wa kikomunisti na misukosuko iliyofuata , watu walianza tena kulewa sana huku idadi ya vifo ikiongezeka.

Watafiti wamesema kuwa inatokana na ambavyo warusi hulewa hasa wanaokunywa sana Vodka ambayo inachangia idadi kubwa ya vifo.

Kodi na vikwazo vilivyoanza kutumika mwaka 2006,vimesaidia kupunguza unywaji wa pombe , lakini watafiti wanasema kuwa viwango vya juu vya ulevi ni sehemu ya mtindo wa maisha nchini Urusi na hilo ndilo linahitaji kubadilika.

No comments:

Post a Comment