MAUMIVU YA MAPENZI KUWA FURAHA
BILA
shaka mpenzi msomaji umzima buheri wa afya na muda huu unanifuatilia
katika busati letu zuri la mahaba, mahali tunapojuzana na kuelimishana
mambo kadha wa kadha yahusuyo mapenzi na uhusiano. Nakukaribisha kwa
moyo mkunjufu tuijadili mada yetu ya leo kama inavyojieleza hapo juu.
Ni
ukweli usiopingika kuwa katika zama hizi za sayansi na teknolojia,
maumivu ya mapenzi yameongezeka maradufu. Kile tunachoamini kuwa ni
maendeleo, kinazidi kuzitesa hisia na nafsi zetu na suala la kutendwa,
kuumizwa, kuvunjika mioyo au kusalitiwa, linaonekana kuwa fasheni siku
hizi.
Kinachowasumbua
wengi ni kushindwa kuelewa nini cha kufanya baada ya kuangukia katika
dimbwi la maumivu ya kimapenzi. Hebu kila mtu ajiulize:
Umewahi
kukuta SMS ya mapenzi kwenye simu ya mpenzi wako akimtumia mtu mwingine
tofauti na wewe? Ulijisikiaje uliposikia mtu mwingine akiitwa majina
mazuri ya kimapenzi na mpenzi wako, pengine kuliko hata yale ambayo
huyatumia kwako? Ulichukua uamuzi gani?
Kila
mtu ataeleza anavyojua yeye lakini ukweli ni kwamba wengi hawajui
kukabiliana na maumivu hata yale yanayosababishwa na maisha ya kawaida.
Kwa kuwa maumivu, usaliti, kuvunjika kwa mioyo na uongo katika mapenzi
ni jambo ambalo kwa kiasi kikubwa halikwepeki katika zama hizi, jambo la
msingi ni kujua nini cha kufanya baada ya kutokewa na dhoruba hizo za
kimapenzi.
Hebu msikilize msomaji wangu, alivyokuwa analalama:
“Wiki
nzima inaisha sasa, siendi kazini, chakula hakipandi, usingizi sipati
wala sitamani kitu chochote, kitu pekee ninachokifanya ni kulia usiku na
mchana, naomboleza na kulalama katika kila sekunde inayopotea mpaka
natamani kujiua, sioni tena thamani ya kuishi, nayachukia mapenzi,
nawachukia wanaume,” alisema Jane huku akilia kutokana na kutendwa na
mwandani wake aliyemsaliti kwa kutoka na rafiki yake kipenzi.
Yawezekana
Jane hayuko peke yake, wapo wengi ambao wanateswa sana na mapenzi
lakini hawana sehemu ya kuyatoa maumivu yao, wanaumia ndani kwa ndani,
miili yao inadhoofika kila siku, hawana furaha japokuwa wanapata
mahitaji yote muhimu, chanzo kikuu kikiwa ni mapenzi.
Hapo ndipo ninapoona umuhimu wa kila mmoja kujua namna ya kusimama tena pale anapoangushwa na maumivu ya kimapenzi.
Zifuatazo ni mbinu ambazo zitakusaidia kuyabadilisha maumivu yako ya kimapenzi kuwa furaha.
JIFUNZE KUSAMEHE NA KUSAHAU
Hakuna
jambo ambalo hutuliza fikra na hisia za mapenzi kama kukubali kumsamehe
yule aliyekuudhi kabla hata hajakuomba msamaha na kuamua kusahau yote
yaliyotokea. Yawezekana wengi mtasema haiwezekani. Inawezekana na wote
waliojaribu mbinu hii walifanikiwa.
Marafiki,
lazima kila mmoja aelewe kwamba unapokasirika au kuumizwa, anayeteseka
siyo yule aliyekusababishia maumivu bali ni wewe mwenyewe. Hasira au
maumivu ya kimapenzi huwa kama moto mkali ambao huitafuna taratibu nafsi
ya mhusika.
Ukisamehe
maana yake unaupa moyo na akili yako nafasi ya kupata sehemu ya kutulia
na kuuzima moto ambao tayari ulishaanza kukolea ndani yako.
No comments:
Post a Comment