Saturday, 3 August 2013

Azam yaacha Mganda, Mkenya safari Sauzi


Azam Fc
Wachezaji wa kimataifa Humphrey Mieno kutoka Kenya na Mganda Brian Omony wameachwa kwenye msafara wa kikosi cha Azam unaotarajiwa kuondoka leo kwenda Afrika Kusini kwa ajili ya kambi ya mazoezi ya kujiandaa na msimu mpya wa ligi kuu ya Bara.
Meneja wa Azam Jemedari Said alisema Omony na Mieno wameachwa kwa sababu ni majeruhi hivyo ni wachezaji 22 tu ndiyo watakaokuwa katika msafara wa watu 33.
“Msafara wetu wa watu 33 utaondoka kesho (leo) saa 5:45 ukiwa na wachezaji 22 kati ya 24 waliosajiliwa msimu huu,” alisema Said.
“Mkenya Humphrey Mieno na Mganda Brian Omony tunawaacha kwa vile ni majeruhi na wanaendelea na matitabu yao.”
Said alisema wengine watakaokuwa katika msafara huo ni benchi la ufundi lenye watu nane na waandishi wa habari watatu na kwamba wakiwa huko watacheza jumla ya mechi nne na timu za ligi kuu ya Afrika Kusini kuanzia Jumatatu.
Ligi kuu ya Afrika Kusini ilianza jana kwa pambano kati ya Mpumalanga Black Aces na mabingwa watetezi Kaizer Chiefs.
Azam ambayo itaitumia michezo hiyo minne pia kujiandaa na pambano la Ngao ya Hisani dhidi ya Yanga la Agosti 17, itacheza na Chiefs keshokutwa, kwa mujibu wa Said.
Mechi ya pili ya Azam itakuwa Jumatano dhidi ya Mamelodi Sundowns, alisema Said kabla ya washiriki hao wa Kombe la Shirikisho la klabu za Afrika mwakani kuivaa Orlando Pirates Agosti 9.

Kambi ya mazoezi ya Azam Afrika Kusini itamalizika kwa pambano dhidi ya Moroka Swallows Agosti 12, alisema Said, mchezaji nyota wa zamani wa Majimaji, na kueleza zaidi kuwa:
Watakaporejea wataingia kambini kwa ajili ya pambano hilo la Ngao ya Hisani na mechi ya ufunguzi ya ligi kuu ya Bara dhidi ya Mtibwa Sugar ambayo itachezwa kwenye uwanja wa Manungu Complex.

No comments:

Post a Comment