Saturday, 3 August 2013

Yanga yaanza kulegeza msimamo


Karia
Mwenyekiti wa Kamati ya Ligi, Wallace Karia
 
Baada ya juzi Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kusema kuwa endapo Yanga itaendelea na msimamo wake wa kukataa udhamini wa kampuni ya Azam Media ambayo inatarajiwa kupewa haki ya kuonyesha mechi zote za Ligi Kuu ya Bara katika televisheni, klabu hiyo haitapewa mgawo wowote wa fedha, uongozi wa mabingwa hao wa Bara umetamka kwamba tatizo lao si fedha.
Akizungumza na gazeti hili jana mmoja wa viongozi wa juu wa Yanga (jina tunalihifadhi) alisema kuwa wao wanataka kuhakikishiwa kuwa klabu yao haitahujumiwa na wadhamini hao watarajiwa wa ligi ambao wanamiliki timu ya Azam ambayo pia inashiriki ligi ya Bara.
Kiongozi huyo alisema pia Yanga inataka ihakikishiwe na TFF pamoja na Kamati ya Ligi kwamba mdhamini wao kampuni ya bia Tanzania (TBL) itatendewa haki kama walivyokubaliana wakati mabingwa hao waliposaini mkataba.
“Tatizo letu si pesa, tunataka kuhakikishiwa kwamba hatutachakachuliwa na kumuweka TBL katika matangazo kabla na baada ya kumaliza mechi zetu,” alisema kiongozi huyo.
Aliongeza kwamba kamati ya utendaji ya Yanga imekuwa makini katika kutetea hoja yake kwa sababu inafahamu itakapomtendea haki TBL itapata mkataba mnono baada ya kumaliza mkataba uliopo sasa na hiyo imetokana na mabango ya wadhamini hao kuondolewa wanapokuwa kwenye mechi za ugenini.
Kiongozi huyo alieleza pia Yanga inataka ithaminiwe kutokana na hadhi yake na vile vile inasisitiza taratibu ni lazima zifuatwe katika kutangaza tenda kama ilivyofanyika miaka iliyopita.
Juzi mwenyekiti wa Kamati ya Ligi, Wallace Karia, aliiambia NIPASHE kuwa shirikisho halitarudi nyuma kuhusiana na mipango ya udhamini huo na wanashangazwa na kauli ya Yanga kuukataa wakati wajumbe wake walishiriki katika vikao vyote vilivyofanyika kabla ya kusaini maelewano ya mkataba na Azam Media.
Karia alisema kuwa pia kitendo cha Yanga kuukana udhamini huo wafahamu kwamba hali hiyo inachangia kukimbiza kampuni nyingine zilizokuwa na nia ya kudhamini soka nchini.
TFF inatarajiwa kusaini mkataba wa miaka mitatu na Azam Media wenye thamani ya Sh. bilioni 5.56 ambapo kila klabu itapata Sh. milioni 100 kwa msimu.
Mkataba huo utasainiwa baada ya siku 30 endapo haitatokea kampuni nyingine itakayotoa ofa ya juu ya hiyo iliyotolewa na Azam Media.

No comments:

Post a Comment