Saturday, 3 August 2013

Mpaka wa Namanga waongoza kusafirisha Tanzanite


Namanga 
 
Mpaka wa Namanga unaopakana na Tanzania na Kenya unaoongoza kwa upitishaji wa madini mengi ya Tanzanite, kwa kutumia njia za panya.
Kamishna wa madini Kanda ya Kaskazini, Benjamin Mchwampaka, aliyasema hayo jana, katika mada inayohusu taratibu za usafirishaji wa madini nchini, kwa maofisa wa idara mbalimbali mpaka wa Namanga.
Alisema kuwa madini hayo yanaingizwa nchini Kenya kama njia ya kuyavusha kupeleka nchi zingine, kutokana na nchi hiyo kutotoza kodi katika uingizaji wa madini hayo.
“Hawa wenzetu wa Kenya hawana tozo zozote katika madini, ili mradi ukifika tu, unapeleka sekta husika, kisha unayatoa nje ya nchi bila gharama zozote kulipa, hivyo hili ni tatizo, tukaamua tukae na sekta ya madini Kenya na wametuelewa na sasa hawatakubali kupokea tena madini yasiyo na nembo,” alisema.

Mchwampaka alisema makubaliano hayo yalikuja baada ya kufanya kikao cha pamoja na kukubaliana kila nchi kutokubali kupokea mzigo wa nchi nyingine bila nembo na vibali.
Alitoa mfano kuwa mwaka 2012 Tanzania ilisafirisha madini hayo tani 2.15 yenye thamani ya Sh milioni 72.70, kwenda nchi jirani ya Kenya, huku baadhi yao yakipelekwa kinyume cha taratibu.

No comments:

Post a Comment