Saturday, 10 August 2013

WAUMINI WA KIISLAMU WACHOMANA VISU JIJINI MBEYA ...SHEIKH AUMIZWA VIBAYA WAKATI WA IBADA YA IDD


WAUMINI wa dini ya Kiislamu waliokuwa katika ibada ya Swala ya Idd El Fitri katika msikiti mkuu wa Ijumaa uliopo Wilayani Kyela mkoani Mbeya wamekumbwa na taharuki baada ya Shekhe wao aliyekuwa akiongoza ibada kuvamiwa kibla wakati akiendesha ibada na kujeruhiwa.

Tukio hilo la aina yake limetokea majira ya asubuhi ambapo Shekhe huyo aliyetambuliwa kwa jina la Nuhu Mwafilango alishambuliwa akiwa katikati ya sijida baada ya mtu mmoja aliyedaiwa kuwa ni mwanafunzi wa shule ya sekondari ya kutwa ya Kyela, Ally Mwangosi kuchoma Shekhe huyo na kitu chenye ncha kali.

Taarifa kutoka msikitini hapo zinadai kuwa mara baada ya tukio hilo, Shekhe alipiga kelele wa kuomba msaada na ndipo waumini waliokuwa wakiswali msikitini hapo waliposhikwa na taharuki.

Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Waislamu Wilayani Kyela Bw. Daudi Mwenda alisema kuwa waumini walimuokoa na kumkimbiza katika Hospitali ya Wilaya kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

Bw. Mwenda alisema kuwa Shekhe huyo ameumizwa vibaya kichwani na kutokwa na damu nyingi. Waumini wawili waliojaribu kumuokoa Shekhe huyo nao walijeruhiwa kwa kuchomwa na kisu ikiwa ni pamoja na mweka hazina wa BAKWATA wilaya Ustadhi Khamis Hussein ambaye alijeruhiwa kichwani na sikioni.

Nao baadhi ya waumini waliokuwepo katika ibada hiyo walisema kuwa tukio hilo lilitokea wakati waumini wote wakiwa wamesujudu, ndipo waliposikia kelele na vurugu.

Mmoja wa waumini aliyejitambulisha kwa jina la Idd Hussein alisema kuwa liliibuka kundi la watu waliomsaidia kijana huyo, na kuibua vurugu kubwa iliyosababisha ibada ya swala ya Idd kuvunjika.

Akizungumzia tukio hilo Katibu wa BAKWATA mkoa wa Mbeya Shekhe Juma Killah alisema kuwa vurugu hizo zimetokea katika swala ya Idd na wahusika wa vurugu hizo ni  Waislamu ambao  wanaipinga BAKWATA.

 ‘’Hiki ni kikundi cha waislamu waliotoka Jijini Dar es salaam ambacho kimekuja huku na kimesambaa katika wilaya zote za mkoa wa Mbeya.Kikundi hiki  kinashawishi watu kuipinga BAKWATA na  kinafanya mambo ambayo BAKWATA hatukubaliani nayo,’’alisema Shekhe Killah.

Alisema kuwa kikundi hicho kilikuwa kikimtuhumu Shekhe wa Wilaya kuwa ni mshirikina na kwamba kutokana na hali hiyo hakupaswa kuongoza ibada msikitini na badala yake wao ndio waliopaswa kuongoza ibada msikitini hapo.

Kwa upande wake Shekhe wa BAKWATA mkoa wa Mbeya Mohamed Mwansasu alisema kuwa kitendo hicho kimeudhalilisha Uislamu na kwamba kilichofanywa na kundi hilo la watu si mafundisho ya dini ya Kiislamu.

Hata hivyo Shekhe Mwansasu alienda mbali zaidi na kusema kuwa katika kikundi hicho wapo  baadhi ya waumini wanaodaiwa kuwa ni askari polisi ambapo inadaiwa kuwa katika moja ya swala ya Ijumaa wiki iliyopita imamu aliyekuwa akiswalisha alivutwa kanzu yake na kutakiwa kutoka eneo la kuongozea ibada ili kuwapisha wao waendeshe ibada hiyo.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya Bw. Athumani Diwani amekiri kutokea kwa tukio hilo ambapo alisema kuwa watu sita wanashikiliwa na Polisi kufuatia vurugu hiyo iliyotokea majira ya saa 2:30 katika msikiti mkuu wa Ijumaa wakati wa swala ya Idd el Fitri.

Kamanda Diwani alisema kuwa kundi la waislamu wanaojiita kuwa ni wenye itikadi kali walivamia msikitini wakati waumini wengine wakiwa wameinama wakisujudu na kumvaa imamu kwa kumpiga kwa mateke na ngumi huku wakiwa na nondo, mikasi na visu.

Alisema waumini hao walikuwa na madai kuwa hawamtaki Shekhe huyo na kwamba uwezo wake ni mdogo katika dini.

Alisema kuwa Shekhe huyo aliokolewa na baadhi ya waislamu ambapo aliwataja walioshikiliwa na polisi kuwa ni pamoja na Mashaka Kassim(30)Issa Juma(37),Ahmed Kassim Magogo(35) Ibrahimu Shaaban(17) ambaye ni mwanafunzi wa shule ya sekondari ya kutwa ya Kyela anayesoma kidato cha Nne,Ambokile Mwangosi,(19)mwanafunzi wa kidato cha tatu shule ya sekondari Kyela, Sadick Abdul(28).

Kamanda Diwani alisema kuwa taratibu zinafanyika ili watuhumiwa wafikishwe mahakamani.

No comments:

Post a Comment