Pamoja na ukweli kuwa kulikuwa na ajenda kadhaa zilizokuwa zimepangwa kujadiliwa katika kikao hicho cha siku mbili kilichofanyika Dar es Salaam, suala la Zitto ndilo lililochukua muda mrefu zaidi kujadiliwa.
Habari za kuaminika kutoka ndani ya kikao hicho zilieleza kuwa wajumbe waligawanyika makundi mawili, baadhi wakipendekeza Zitto avuliwe nafasi yake ya Naibu Katibu Mkuu kwa maelezo kuwa anakwenda kinyume na taratibu za chama hicho na wengine wakipinga hatua hiyo kwa maelezo kuwa haina tija.
Tuhuma zilizokuwa zikimkabili Zitto Kabwe:
Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, mwanzoni mwa Novemba mwaka huu aliingia katika malumbano na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema kuhusiana na masuala ya posho, akituhumiwa na Lema kuwa anakataa posho za vikao bungeni, lakini anapokea posho kutoka mashirika mbalimbali nchini.
Pia, aliingia katika malumbano na chama chake baada ya kutumia kofia yake ya Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), kutuhumu vyama vya siasa kuwa hesabu zake hazikaguliwi na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Kauli ambayo jana Kigaila aliitolea ufafanuzi na kueleza kuwa Chadema kimekaguliwa na hesabu zake tayari zipo kwa Msajili wa Vyama vya Siasa.
Mvutano wa jana:
Mvutano wa jana ulianza baada ya Mbowe kufungua kikao hicho saa 4:00 asubuhi.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho zilieleza kuwa baadhi ya wajumbe, wakiwamo wabunge, walitaka Zitto avuliwe nafasi aliyonayo na kuwa mwanachama wa kawaida, huku wengine wakipinga hatua hiyo kwa maelezo kuwa Zitto hakuwepo katika kikao hicho na kwamba alipaswa kusikilizwa.
“Baada ya hali kuwa hivyo, Mbowe alipendekeza kuwa Zitto asijadiliwe kwa kuwa hakuwepo katika kikao hicho,” kilieleza chanzo cha habari hizo.
Zitto alikuwa katika safari ya kikazi huko Sudan Kusini akiwa amefuatana na wajumbe wa PAC.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa Zitto alitafutwa na alituma salamu kwa wajumbe wa kikao hicho akiwaeleza kuwa alikuwa njiani na kuahidi kuwa angehudhuria mara tu baada ya kuwasili.
“Zitto alituma ujumbe kuwa anakuja katika kikao, kilikuwa na ajenda nyingi lakini suala lake lilijadiliwa kwa kirefu sana,” kilieleza chanzo chetu. Licha ya ombi la Mbowe, bado wajumbe walishinikiza kuendelea kumjadili Zitto hivyo kusbabisha kuchelewa kujadiliwa kwa ajenda nyingine.
Tangu juzi, siku ya kwanza ya kikao hicho, ulinzi uliimarishwa nje ya Jengo la Ubungo Plaza na jana walinzi wa chama hicho, Red Brigade waliwatimua waandishi wa habari waliokaribia eneo hilo wakisema hayo ni maagizo kutoka kwa uongozi wa juu.
Yaliyojadiliwa ndani ya kikao:
Katika ufafanuzi wake kwa waandishi wa habari jana jioni, Kigaila alisema kikao hicho kilichoanza juzi, kimejadili mambo mbalimbali. Alisema juzi kikao hicho kilijadili muhtasari wa vikao viwili vya dharura vya Kamati Kuu vilivyofanyika hivi karibuni.
“Tumejadili taarifa ya uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kiembesamaki, Zanzibar unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni... tunathibitisha kuwa tutashiriki,” alisema.
“Kulikuwa na taarifa ya hesabu za chama zilizokaguliwa na kupelekwa kwa Msajili wa Vyama vya Siasa na taarifa za fedha za utendaji kuanzia Kamati Kuu iliyopita mpaka Kamati Kuu ya sasa,” alisema Kigaila.
Huku akionyesha kitabu cha ukaguzi wa fedha mwaka 2010/11 na 2011/12 alisema: “Kamati Kuu imeridhika kuwa chama kimekaguliwa na hatuna deni kwa msajili.
Ajenda za kuhitimisha kikao jana:
Alisema kikao cha jana kilijadili ajenda za uboreshaji wa jengo la makao mkuu pamoja na kupanga upya kurugenzi za chama hicho pamoja na nguvu kazi ya makao makuu ili kuweza kutekeleza vizuri majukumu yake.
“Ajenda inayoendelea hivi sasa ni ya uundaji wa programu ya `Chadema ni Msingi’, ambayo lengo lake ni kukijenga chama katika ngazi za chini kabisa. Huu ni mpango mkuu wa chama wa `Vuguvugu la Mabadiliko’ (M4C). Ajenda ya mwisho itakuwa ni kujadili hali ya kisiasa nchini.”
Zitto awasili ukumbini usiku na kuzua malumbano makali:
Zitto alifika katika kikao hicho jana saa 2.24 usiku akiwa na walinzi wanne na habari kutoka ndani zinasema kwamba mara baada ya kuingia, ajenda ya kumjadili ilirejea. Ilielezwa kwamba alipewa nafasi ya kujitetea baada ya kusomewa mashtaka yaliyokuwa yakimkabili.
Baada ya kurejeshwa kwa agenda hiyo malumbano makali yalizuka kwani wajumbe walikuwa wazungumza kwa sauti za juu na jazba kiasi cha kusikika nje.
Taarifa zaidi zinaarifu kuwa malumbano hayo yalifikia tamati kwa kumvua Zitto Kabwe nafasi zote za uongozi ndani ya CHADEMA ikiwemo ile ya Naibu Katibu Mkuu wa chama pamoja na nafasi ya Naibu wa Kambi Rasmi ya Upinzani.
No comments:
Post a Comment