Thursday, 30 January 2014

Godoro, miti ilivyowaokoa na kifo kwenye mafuriko



Baadhi ya watu wakibeba chakula cha misaada kutoka kwa wasamaria wema.

 Watu zaidi ya 25 walikwenda kwenye nyumba ya jirani iliyojengwa kwa matofali na kuezekwa bati ili kujiokoa, kwani nyumba zao ni za udongo ambazo baadhi yake zilikuwa zinabomoka. Hata hivyo walijikuta wakivamiwa pia na maji katika nyumba hiyo kiasi cha kulazimika  kuyachukua makochi, kuyapanga juu ya kochi jingine kisha kuweka godoro juu yake, wakasimama juu yake ili kujiokoa. Watoto wadogo walibebwa mabegani hadi walipokuja kuokolewa na wasamaria.


 Watoto wadogo walibebwa au kusimama kwenye mabega ya watu wazima, huku chumba kikiwa kimejaa maji. Hii ni hali ambayo ilitokea katika mafuriko ya hivi karibuni yaliyotokea Kilosa, mkoani Morogoro.

Hali ya mambo

Ilikuwa siku yenye mateso makubwa na uchungu wa kupotelewa na mali mbalimbali kwa wananchi wa Kijiji cha Magole, ambao walizingirwa na mafuriko.

Kila mtu alikuwa na aina yake ya kujiokoa; wapo niliowaona wakiwa juu ya miti  ilimradi tu ni namna gani ya kutafuta njia ya kujinusuru na kifo.

 Mwalimu wa Shule ya Msingi Magole Wilaya ya Kilosa Mkoa wa Morogoro, Marthin Kongera (42) anaeleza mkasa mzima uliyoikumba familia yake pamoja na yeye mwenyewe na majirani waliokimbilia katika nyumba yake iliyojengwa na matofali ya saruji yenye vyumba viwili na ukumbi mmoja ili kuweza kujihifadhi na mafuriko yaliyoikumba tarafa ya Magole Januari 22 mwaka huu saa 12 asubuhi.

Akizungumza na mwandishi wa makala haya katika nyumba za Shule ya Msingi Magole, Kongera anasema kuwa ilikuwa siku ya Jumanne, yeye na familia yake waliamka salama saa 12 asubuhi,  baada ya muda mfupi akijiandaa kwenda kazini (shule mita 40 tu kutoka nyumbani kwake). Alianza kuona maji yakitiririka huku yakiwa yamesomba uchafu na kadiri muda ulivyozidi kusogea mbele maji yaliendelea kufika eneo la shule na kuanza kusambaa sehemu kubwa.

Maji hayo yalielekea kwa kusambaa kwa kasi katika mitaa ya kijiji hicho.

“Ni miujiza ya Mwenyezi Mungu kwani kama hakupenda ufe huwezi kufa. Ndivyo ilivyotokea kwetu sisi, kama Mungu angependa tufe katika mafuriko haya basi katika nyumba yangu wangeopoa maiti 25 ya watu wazima na watoto,” anasema Kongera.

Baada ya familia ya mwalimu huyo kuzingirwa na maji hayo walishindwa kuyakimbia hasa baada ya maji mengine zaidi kuwavamia katika eneo hilo walilokuwepo.

Wakati akiangalia namna ya kujiokoa, kundi la majirani nalo liliingia kwenye nyumba yake kuomba msaada wakifikiri kwamba kwa vile nyumbani hiyo ni ya tofali maji yasingeweza kuathiri kama ilivyo kwao; kwani walitoka kwenye nyumba zilizojengwa kwa udongo na kuezekwa kwa nyasi, siyo tofali na bati kama ilivyo nyumba ya mwalimu.

Kongera anasema baada ya maji kuzidi na hakuna pa kukimbilia yeye pamoja na familia yake na wale majirani zake alichukua uamuzi wa kufunga milango na madirisha kisha kuwaamuru kinamama wasimame juu ya makochi na meza na watoto kusimama juu ya mabega ya mama zao huku wakiwa wameshikilia nondo za madirisha kwa muda wa zaidi ya saa nne.

“Kwa jumla kila aliyekuwa mle ndani alichoka sana, hebu mwandishi fikiria kusimama sehemu moja tena katika kochi na meza kwa zaidi ya saa nne huku wengine wakiwa na watoto wa miaka mitano hadi saba wamesimama juu ya mabega yao. Kama ingezidi saa moja au mbili, hali ingekuwa mbaya, kwani wengi walishaanza kuchoka,” anasema  mwalimu huyo.

No comments:

Post a Comment