Kijana mwenye umri wa miaka 23 amejikuta katika wakati mgumu, baada ya kuathiriwa na tabia ya kula mifuko na bidhaa za plastiki.
Kijana huyo, Robert kutoka huko Oakland, Tennessee
nchini Marekani alianza tabia hiyo kama mzaha akiwa na umri wa miaka
saba tu, ambapo alipendelea zaidi plastiki za rangi ya bluu ambazo kwa
mtazamo wake alikuwa akiona rangi hiyo ina utamu.
Kadiri miaka ilivyozidi kuongezeka, tabia hiyo
ilimwathiri na hata kujikuta akilazimika kutumia mbinu za ziada kuipata,
ikibidi kwa kuiba kwenye maduka makubwa au kwenye maduka ya mitaani.
Si hivyo tu, mara nyingine huchukua hatua ya kuiba
mifuko ambayo huhifadhiwa matunda kwa ajili ya maonyesho kwenye maduka
na kuyamwaga kisha kutokomea na mifuko hiyo.
Tangu alipoanza tabia hiyo, imeelezwa kwamba
tayari ameshatafuna zaidi ya mifuko 60,000 ya plastiki ambayo kwa wingi
wake inaweza kujaza uwanja wa kuchezea mpira wa miguu.
Kwa mujibu wa maelezo yake, huanza siku yake kwa
kula mfuko wa kwanza kama kifungua kinywa na hupendelea zaidi mifuko ya
rangi ya bluu ambayo hutumiwa kufunga magazeti.
Alieleza kwamba muda mwingine hulazimika kuanza
kurandaranda kwenye nyumba za jirani akitafuta mifuko hiyo ambayo wengi
wa majirani huitupa ovyo baada ya kufungua na kuchukua magazeti yao ili
kukidhi haja yake.
Robert anaamini kwamba mifuko yenye rangi nyingine
tofauti na rangi ya bluu pia ina ladha tofauti, hivyo wakati wa
majadiliano yake na kituo cha TLC katika kipindi chake cha Tabia Yangu
ya Ajabu alisema anaona bluu ni tamu zaidi.
Mara nyingine hulazimika kukaa hadi siku moja na
nusu bila kula chakula iwapo atapata dozi ya kutosha ya mifuko hiyo,
ambapo baada ya kujisaidia hali yake hurejea kama kawaida na kuendelea
na shughuli zake.
Kitendo hicho kimewashangaza wengi kwa kuwa hata
baadhi ya majirani hawakuwahi kujua kwamba kwa miaka yote alikuwepo
kijana ambaye alikuwa akiwasaidia kupunguza taka za mifuko ya plastiki
majumbani kwao.
Hata hivyo, mchumba wake, Ashley alisema amekuwa
akisumbuliwa sana na tabia hiyo ya Robert na amekuwa akijaribu kufanya
kila juhudi ili aachane nayo kabla ya ndoa yao inayotarajiwa kufungwa
miezi sita ijayo.
Jambo la kushangaza ni kwamba, japokuwa kitaalamu
ulaji wa plastiki kwa binadamu husababisha kuziba kwa utumbo na kuharibu
ini, vipimo alivyochukuliwa Robert vinaonyesha kwamba hana athari zozo katika maeneo hayo.
Katika mtiririko wa matukio yake, Ashley alisema aliudhika zaidi
siku walipokwenda kutafuta keki kwa ajili ya harusi yao, ambapo Robert
alipotakiwa kuonja alishindwa akisema kwamba ameshiba kupita kiasi
kutokana na plastiki alizokula.
Muda mfupi baadaye alilalamika kwamba ana maumivu
ya tumbo na baada ya kushauriwa kwa muda ndipo alipokubali kwenda
kumwona daktari kwa ajili ya vipimo.
Japokuwa Ashley amefahamu kuathirika huko kwa
mchumba wake tangu walopoanza uhusiano zaidi ya miaka miwili iliyopita,
anasema aliona ni jambo linalohitaji ukaribu na msaada zaidi ili
kumwepusha na tabia hiyo.
Kwa ajili ya upendo na mapenzi yake kwa Ashley,
Robert kwa sasa amemwahidi mchumba wake huyo kwamba atafanya kila
linalowezekana kuacha tabia hiyo ili kuwezesha ndoa yao iwe ya amani
mara wakati utakapofika.
No comments:
Post a Comment