Monday, 21 October 2013

Anakudanganya saaanaaaa!!! Mnase hivi!

J.J. Newberry mtaalamu wa masuala ya tabia aliwahi kusema kuwa ni kazi rahisi kumtambua mtu muongo endapo utajifunza mbinu za kumfahamu, lakini akaongeza kuwa ni vigumu sana kumnasa muongo kwa njia za kubahatisha. Huu ni ukweli kwamba, wengi huongopewa na wapenzi wao na kujikuta kwenye utata wa kuamini wanachoambiwa na wenza wao ni cha kweli au uongo.
 “Nimechelewa kwenye foleni, nilikwenda kumtazama  mama mgonjwa” Maelezo haya ukiyaangalia unaweza kuamini, lakini pengine unapolinganisha na muda aliofika mpenzi wako nyumbani unabaki kwenye utata, kama kweli alikwenda kumuona bibi yake au alikwenda kufanya usaliti? Kwa kutambua hilo, mada hii inakuja na njia 10 za kumtambua mtu anayeongopa.

 MNASE KUPITIA SHUKU
 Njia namba moja ya kumtambua mtu muongo ni shuku. Wataalamu wanasema kuwa kama mlio wa bunduki utatokea na mtu akakimbia bila hata kutazama ulikotoka ujue mtu huyo ana uongo ndani ya nafsi yake na kinachomkimbiza si mlio bali woga wake.
 Kwa maana hiyo kama ataingia mumeo au mkeo ndani na ghafla akaonesha kushtushwa na uwepo wako jua kuwa ana uongo moyoni au akiacha kufanya jambo fulani kwa kuingia kwako tambua kuwa kuna jambo la uongo ambalo linamuongoza. Muulize vizuri.
 MUULIZE  ASILOTARAJIA
 Swali la kushtukiza lisilotarajiwa linaweza kukusaidia kumtambua mtu muongo anasema Sir Walter Scott kutoka Uingereza ambaye ni mshauri wa masuala ya jamii. Anasema waongo wengi wanapodanganya huwa wametayarisha majibu yao, kupitia maswali wanayotarajia kuulizwa. Kwa mfano akisema, kulikuwa na foleni njiani anakuwa na maeneo ameyaweka tayari. “Yaani kutoka Kigogo pale njia panda magari yalikuwa hayatembei kabisa.”
 Sasa ili umnase muulize jambo ambalo haliko kwenye mpangilio wa uongo wake, kwa mfano hivi magari ya kutoka sehemu fulani yanayopitia hapo Kigogo siku hizi yanakatiza wapi kupisha foleni?” Utashangaa anaanza kutoa macho huku akitafuta jibu wakati inawezekana ulichomuuliza si cha kweli, lakini kwa sababu anadanganya atataka kukupa jibu, ujue huyo ni muongo.
 MBANE KUHUSU MAELEZO YAKE
 Waongo wengi huwa hawana kumbukumbu za zaida, wanapodanganya walikuwa wanakunywa baa fulani husahau kutunza kumbukumbu hizo na kujikuta baadaye wanataja kitu kingine au wakakana kutoa maelezo kama hayo. Hivyo unapokuwa na mtu muongo kariri maneno ya kwanza na kisha umuulize baadaye ukitaka ufafanuzi utashangaa yote yameshayeyuka kichwani kwa muongo na kubaki akikutazama asijue la kufanya.
 MTAZAME MUONEKANO WAKE
 O'Sullivan aliwahi kusema watu waongo huwa na sura tofauti wanaweza kucheka wakati nyuso zao zinalia. Au wakati mwingine kupenda sana kupata msaada wa nguvu za mwili kupitia kuchezea vidole au kushika shika majani.
 Kwa mfano unapokuwa unamtongoza mwanamke ukiona anaacha kukuangalia na kuanza kuchezea vidole au kijiti jua amekukubali hata kama kinywani ataendelea kukataa. Watu waongo nao huficha uongo wao kwa njia hizo. Hivyo unaweza kumtambua muongo kwa kutazama muonekano wake wakati akiongea na wewe.
 MTISHE KWA ADHABU
 Njia nyingine ya kumtambua mtu muongo, ni kumtisha kwa kuchukulia hatua za kustahili na kosa lake. Mapema tu katika mazungumzo yako unaweza kumwambia hivi: “Kwa kuwa umenichosha kwa tabia zako leo lazima niujue ukweli na nitahakikisha unachosema kina ukweli” Si unasema umechelewa kazini, mimi niko tayari kumpigia simu bosi wako kumuuliza” Baada ya kumpa maneno kama hayo ya vitisho anza kumuuliza, utaona anavyokuwa mpole maana anajua akikutajia alikwenda kwa rafiki zake utataka kwenda huko au kumpigia simu hivyo atalazimika kusema ukweli.
 TAMBUA KUPITIA ISHARA ZA MACHO

Paul Ekman mwanasaikolojia kutoka Chuo cha California Medical School cha San Francisco, anasema  mawazo yanayokuwemo ndani ya moyo wa mwanadamu hujulikana kupitia uso wake. Mwenye huzuni moyoni hutambulika usoni hata kama mhusika atakuwa akicheka kama nilivyosema na kadri ukweli wa jambo unavyozidisha msukumo moyoni uso nao hubadilika kulingana na ukweli huo, hata kama mtu atakuwa ameshikilia msimamo wake wa kukataa kukiri ukweli. Msome mtu kwa kumtazama usoni na usimpe nafasi ya kutazama pembeni.
 ANGALIA MKANGANYIKO
Njia nyingine ya kumtambua mtu muongo ni kumchunguza kuhusu mkanganyiko wa maelezo yake na ishara anazozitoa kupitia kichwa au mikono yake. Mtu muongo unaweza kumuuliza jambo kichwa kikakataa, maelezo yake yakakubali. Hivyo ni vema kufuatilia uhusiano wa maneno, ishara za mwili, sauti yake na vitendo vyake. Ukiona vinapishana tambua kuwa huyo ni muongo.
 KUHUSU HALI YAKE YA KAWAIDA
 Mtu muongo unaweza kumtambua kupitia kawaida yake, ikiwa mpenzi wako ni mtu wa furaha anapokutana nawe lakini ikatokea bila sababu yoyote anapoteza furaha na kutoona umuhimu wako tambua kuwa ana uongo moyoni mwake unamsumbua, ni vema ukamuuliza.
 MAELEZO MENGI
 Wapenzi wenye uongo huwa na maelezo mengi, utakuta kitu kidogo tu cha kujibu ndiyo au hapana yeye anatoa maelezo mengi yasiyokuwa na msingi. Ukiona hivyo tambua kuwa mpenzi wako ana tabia ya uongo na kwamba anarefusha maelezo ili kuujenga uongo wake uonekane ni kitu cha kweli.
 USIPUUZE UKWELI
 Pamoja na mambo yote tuliyojifunza kuhusu waongo, si vema kuyapuuza yote kwa sababu tu umebaini kuwa mtu fulani ni muongo, lazima ya ukweli yapewe nafasi yake. Kwa mfano muongo anapoeleza jambo la kweli muunge mkono, ili kumfanya mwenyewe atofautishe ukweli na uongo anaopika. Ukikataa yote atakuona wewe ndiyo muongo kwa vile utakuwa umekataa mambo ya ukweli aliyokuambia.

No comments:

Post a Comment