MASHABIKI wa Yanga jana Jumatano walijazana
kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es
Salaam kumpokea straika wao mpya, Emmanuel Okwi, lakini wakaishia
kumpokea beki wa Simba, Gilbert Kaze.
Ingawa uongozi ulionekana kushangaa uvumi
uliowajaza mashabiki wao uwanjani hapo wakiamini Okwi angetua kutoka
Uganda, mchezaji huyo hakuonekana na wakiwa wanazidi kusubiri
wakakumbana na Kaze majira ya saa 9 alasiri.
Kaze alikuwa akitokea Burundi alilokuwa tayari kuunganisha ndege kwenye Zanzibar kwenye kambi ya Simba.
Kaze alipotoka nje ya uwanja alikumbana na
mashabiki kibao na waandishi wa habari kiasi cha kumfanya ashituke,
lakini baadaye viongozi wa Simba waliofika kumlaki wakamwambia kwamba si
yeye anayesubiriwa na umati huo wa Yanga bali ni Okwi.
Lakini, mashabiki wa Yanga wakaanza kumzonga Kaze
mpaka kwenye gari wakimpa maneno ya kejeli na kumwambia: “Umepotea njia
wewe kwenda Simba...na Okwi anakuja.” Mchezaji huyo alicheka tu na wala
hakujibu chochote.
Kaze amechelewa kujiunga na wenzake ambao wako
chini ya kocha mpya, Zdravko Logarusic kisiwani Zanzibar kwa kile
kinachodaiwa, alikuwa anamuuguza mama yake mzazi.
Beki huyo wa kati, alitua na ndege ya Shirika la
Rwanda na kulakiwa na mmoja wa kiongozi, Medy Omary. Aliunganisha ndege
ya kwenda Zanzibar na leo Alhamisi ataanza mazoezi na wenzake chini ya
kocha mpya, Zdravko Logarusic. Hata hivyo, Kaze aliyekuwa kwenye haraka
kuunganisha ndege, alisema kwa kifupi: “Nashukuru nimerudi salama, kubwa
tutakutana uwanjani.” Ndiyo mchezaji pekee aliyekuwa hajajiunga na
timu, atakuwa na kazi moja ya kugombania namba na Mkenya Donald Musoti
aliyesajiliwa kutoka Gor Mahia na Joseph Owino raia wa Uganda.
Mbali ya kujaa uwanja wa ndege, makao makuu ya
Yanga, makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani, Kariakoo, kulikuwa na
utitiri wa mashabiki ambao walikuwa wanamsubiri Okwi.
No comments:
Post a Comment