NaibuWaziriwaHabari, Vijana, Utamaduni na Michezo Juma Nkamia akizungumza jana jijini Dar es Salaam wakati alipokuwa kiwaaga wajumbe wenzake wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa baada ya kuteuliwa katika wadhifa mpya. Kulia ni mwenyekiti wa kamati hiyo Edward Lowassa.
“Ni vizuri Waziri awaite wahariri azungumze nao, kwa sababu hukumu hiyo ya kutotoa ushirikiano kwa Waziri huyo haijulikani mwisho wake, ni vizuri kuzungumza na kumaliza tofauti zilizopo,” alisema Lowassa.
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa ameitaka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kuzungumza na wadau wake na kuchukua maoni yao ili muswada wa sheria mpya wa vyombo vya habari usaidie kutatua mgogoro baina yake na vyombo vya habari.
Lowassa, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya
Bunge ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, alitoa ushauri huo
jana katika hafla fupi ya kumuaga mjumbe wa kamati hiyo, Juma Nkamia,
ambaye ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na
Michezo.
“Muswada wa sheria mpya wa habari umekaa muda
mrefu bila ya kuwasilishwa bungeni, kwani kuna tatizo gani? Ni vizuri
mzingatie maoni ya wadau wengine wa masuala ya habari siyo kutaka
kuwapeleka jela tu waandishi,” alisema.
Hivi karibuni, Serikali iliwasilisha miswada ya
sheria mbalimbali ikiwamo Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 ikiwa na
vifungu mbalimbali vilivyotafsiriwa kuwa na mwelekeo wa kubana uhuru wa
vyombo vya habari.
Mathalan, ulipendekeza kuongeza adhabu ya faini
kwa makosa ya kuchapisha habari za uchochezi au zinayoweza kusababisha
uvunjifu wa amani. Ulipendekeza kuongezwa faini kutoka Sh150,000 hadi
kufikia Sh5 milioni kwa kosa hilo.
Mapendekezo hayo yalitolewa huku Serikali ikiwa imetoa adhabu za kuyafungia magazeti ya Mwananchi, Mtanzania na Mwanahalisi.
Kitendo cha kufungia magazeti hayo kiliwaudhi
wadau wa habari ambao waliazimia kutoripoti habari za Waziri wa Habari,
Vijana, Utamaduni na Michezo na Mkurugenzi wa Maelezo.
Lowassa alisema ni aibu na haileti picha nzuri katika jamii kuwapo kwa uhusiano mbaya kati ya pande hizo mbili.
“Ni vizuri Waziri awaite wahariri azungumze nao,
kwa sababu hukumu hiyo ya kutotoa ushirikiano kwa Waziri huyo
haijulikani mwisho wake, ni vizuri kuzungumza na kumaliza tofauti
zilizopo,” alisema Lowassa.
Mjumbe wa kamati hiyo, Suzan Lyimo alisema muswada
wa vyombo vya habari unatakiwa kuwasilishwa bungeni ili sheria
ipatikane mapema kabla ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika
baadaye mwaka huu na Uchaguzi Mkuu mwakani.
“Kwa kuwa wewe Nkamia ni mwanahabari, unaelewa
vizuri matatizo ya vyombo vya habari na waandishi wanavyofanya kazi
katika mazingira magumu.... muulete muswada bungeni ukiwa umekamilika
kila nyanja,” alisema.
Kwa upande wake, Nkamia aliahidi kufanyia kazi
ushauri huo wa kukutana na wahariri ili kumaliza tofauti baina yao na
viongozi wa wizara.
“Kwa kweli siyo vizuri, baba anaamka kisha hasalimiani na watoto
wake, waandishi tushirikiane, hakuna haja ya kugombana tunajenga taifa
moja,” alisema Nkamia.
Alisema anaamini sheria hiyo ikipitishwa itakuwa na mambo yatakayosaidia kuboresha tasnia ya habari.
Katibu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF),
Neville Meena alisema hatua ya kutotoa ushirikiano kwa Waziri wa Habari
hakutokani na chuki binafsi, bali ni kupinga ukandamizaji dhidi yao.
“Hatuwezi kukataa wito wa kukutanishwa na Waziri,
sisi hatujamchukia kama wengine wanavyofikiri, bali tunalenga
kuhakikisha sheria kandamizi zilizopitwa na wakati hazitumiki,” alisema
Meena.
Bunge liliagiza Serikali kupeleka muswada wa
Sheria ya Vyombo vya Habari ili ujadiliwe upya na Bunge hilo badala ya
kupeleka maombi ya marekebisho ya vifungu vya Sheria ya Magazeti ya
mwaka 1976 kama ilivyofanya Novemba, mwaka jana.
No comments:
Post a Comment