Wafuasi wa Chadema wanaomuunga mkono Zitto na wale wa uongozi wa juu, jana walipambana tena mahakamani kwa ngumi na mawe kisha kusababisha watu wawili kujeruhiwa.
Baada ya kurejea vifungu mbalimbali vya sheria, kanuni, amri na uamuzi wa kesi mbalimbali za Mahakama Kuu, Mahakama ya Rufani na za nje, Jaji Utamwa alisema anakubaliana mtoa maombi.
Dar es Salaam. Aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe ameshinda maombi yake dhidi ya chama hicho mahakamani.
Katika maombi hayo namba 1 ya mwaka 2014, Zitto
ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, aliiomba Mahakama Kuu, Kanda
ya Dar es Salaam kuizua Kamati Kuu (CC) ya Chadema kumjadili au kuchukua
uamuzi wowote kuhusu uanachama wake.
Zitto kupitia kwa Wakili Albert Msando alikuwa
akiiomba Mahakama itoe zuio hilo la muda hadi kesi yake ya msingi
itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.
Katika uamuzi wake jana, Mahakama Kuu ilikubaliana
na maombi na hoja za Zitto na kutoa zuio kwa Kamati Kuu ya Chadema na
au chombo chake chochote cha uamuzi kumjadili na kutoa uamuzi wowote
kuhusiana na uanachama wake, hadi kesi yake ya msingi itakaposikilizwa
na kuamuliwa.
Awali, Mawakili wa Chadema wakiongozwa na
Mwanasheria Mkuu, Tundu Lissu na Mkurugenzi wa Katiba, Sheria na Haki za
Binadamu, Peter Kibatala walipinga maombi hayo wakidai kuwa hayajakidhi
matakwa ya kupewa zuio la muda.
Katika uamuzi wake, Jaji John Utamwa alikubaliana
na hoja za Wakili Msando kuwa maombi hayo yametimiza matakwa yote ya
kupewa zuio hilo.
Matakwa hayo ni pamoja na kuwapo kwa mgogoro baina
ya pande mbili, hasara au madhara yasiyoweza kufidiwa na usawa katika
athari kwa pande zote.
Jaji Utamwa alikubaliana na hoja za Wakili Msando
kuwa iwapo Mahakama haitaingilia kati na kutoa zuio hilo, mtoa maombi
ataathirika zaidi kuliko wajibu maombi.
Akijibu hoja ya Wakili Lissu aliyepinga hoja ya
mtoa maombi kuathirika pamoja na wananchi wa jimbo lake kwa kukosa
uwakilishi bungeni, kuwa hata akipoteza ubunge kwa kuvuliwa uanachama
utaitishwa uchaguzi mdogo, Jaji Utamwa alisema uchaguzi mdogo huwa
unachukua mchakato mrefu.
Baada ya kurejea vifungu mbalimbali vya sheria,
kanuni, amri na uamuzi wa kesi mbalimbali za Mahakama Kuu, Mahakama ya
Rufani na za nje, Jaji Utamwa alisema anakubaliana mtoa maombi.
“Kwa hiyo ninatoa zuio la muda kwa Kamati Kuu ya
Chadema na au chombo chake chochote cha uamuzi kwamba kisimjadili na
kutoa uamuzi wowote dhidi ya mleta maombi kuhusiana na uanachama wake
kusubiri kusikilizwa na kuamuriwa kwa kesi yake ya msingi,” alisema Jaji
Utamwa.
Kabla ya kufikia uamuzi huo, Jaji Utamwa
alitupilia mbali hati ya kiapo kinzani ya Chadema iliyotolewa na Wakili
Kibatala baada ya kuwekewa pingamizi na Wakili Msando ambaye alidai kuwa
katika hati hiyo, kuna taarifa za kusikia ambazo hakueleza alipozitoa.
No comments:
Post a Comment