Wednesday, 5 February 2014

Lembeli aituhumu Serikali kubadilisha Hifadhi ya Arusha

Serikali inadaiwa kutoa maagizo kinyemela kurekebisha mipaka ya Hifadhi ya Taifa Arusha, bila kufuata utaratibu.


Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira imesema Serikali imekuwa ikitoa maagizo ya kubadilishwa kinyemela mipaka ya Hifadhi ya Taifa ya Arusha.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, James Lembeli alisema mwaka 2005 Serikali kupitia gazeti la Serikali namba 280, iliongeza mipaka ya hifadhi kwa kuingiza msitu wa asili na ule wa kupanda.
Lembeli alisema kwa mujibu wa taarifa walizonazo, Serikali ya awamu ya nne iliamua kubatilisha uamuzi wa Serikali kwa kuliagiza Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) kurekebisha mipaka yake.
Lembeli ambaye pia ni Mbunge wa Kahama, alikuwa akizungumza na waandishi wa habari juzi baada ya wajumbe wa kamati yake kutembelea hifadhi hiyo iliyopo nje kidogo ya mji wa Arusha.
Alisema kwa utaratibu iwapo Serikali ilikuwa inaona ilifanya makosa katika tangazo lake namba 280, mabadiliko hayo ya mipaka yalitakiwa yapelekwe bungeni kama azimio ili Bunge liamue.
Alisema kutokana na ubabaishaji huo, kuanzia wakati huo (mwaka 2005) mpaka sasa, yale maeneo ambayo Tanapa iliambiwa iyaache yanasimamiwa na chombo ambacho hakina mamlaka kisheria.
Kamati hiyo imeagiza Wizara ya Maliasili na Utalii kuwasilisha taarifa kwa kamati ili kuthibitisha suala hilo, ikiwezekana kuifahamisha aliyehusika kutoa maagizo hayo kwa Tanapa.
“Tungependa kufahamu aliyetoa maagizo hayo kwa Tanapa na kuwafanya washindwe kutekeleza sheria ile kupitia gazeti la Serikali, kuruhusu wananchi kufanya watakavyo ndani ya hifadhi,” alisema.
Wakati huohuo, kamati hiyo imesema anguko la shughuli za uhifadhi na utalii maeneo mbalimbali yaliyotengwa, zinatokana na tabia ya kuingiza siasa katika shughuli za hifadhi. Lembeli alisema kuna dalili za siasa kunyemelea uhifadhi na alitahadharisha kuwa,
 uhifadhi ni sayansi hivyo siasa haina nafasi badala yake utaalamu ushike hatamu.

No comments:

Post a Comment