Tuesday 29 October 2013

JE NGONO NI KIPIMO CHA MAPENZI YA DHATI...? TUSOME PAMOJA TUELEWE

              Wanaume wengi wanatumia kigezo hiki kama kuthibitisha au kudhihirisha mapenzi ya dhati. Utamsikia mwingine anasema: “Sasa kama hutaki kufanya mapenzi na mimi, utakuwa hunipendi.”
Kwa sababu wanawake nao wanaogopa kuachwa au wanatamani ndoa, kwa kuamini kwamba tendo hilo ni kila kitu wanajikuta wakikubali; sasa hapo inategemea, mwisho unaweza kuwa mzuri au mbaya!

MAPENZI NI NINI HASA?
Kila mmoja anaweza kuwa na maana yake, lakini kimsingi mapenzi hayana maana ya moja kwa moja! Kwa ujumla mapenzi ni hisia zenye msisimko wa pendo la dhati zinazotoka moyoni mwa mmoja kwenda kwa mwingine.

Pendo hukamilika ikiwa wawili hao kwa wakati mmoja watahisi hisia hizo, ingawa wakati mwingine mmoja ndiyo huwa wa kwanza kuanza kuhisi hisia hizo.

Tafsiri hii nimewahi kuitaja mara kadhaa katika makala zangu, kama wewe ni mdau wa kona hii utakuwa unakumbuka, kama ndiyo kwanza unasoma hapa, basi si vibaya maana utakuwa umeingiza kitu kichwani mwako.

Wakati mwingine inawezekana mkajikuta mmependana tangu siku ya kwanza tu mlipokutana, lakini wengine huchukua muda mrefu kidogo kabla hisia hizo hazijachukua nafasi sawasawa. Wapo wanaofikiria mapenzi ni ngono au ngono ni sehemu ya mapenzi. Hawa nitapingana napo kwa nguvu zangu zote.



HAKUNA ugonjwa mbaya kama utumwa wa fikra. Yaani uwezo wako wa kufikiria kuwa mikononi mwa mtu. Kwa maneno mengine naweza kusema kwamba, kukubaliana na jambo ambalo huna uhakika nalo, lakini kwa sababu wengi wanaamini na wewe unafuata mkumbo bila kuangalia athari zake.

Eti wakifanya mapenzi na wapenzi wao, ndiyo wataonesha kuwa wanawapenda! Ni sahihi kweli? Si sawa...

Msichana ambaye ameutunza usichana wake kwa miaka 22, auharibu kwa mtu mwenye tamaa zake halafu amuache? Nasema hapana...ni afadhali uendelee kuvumilia mpaka kwenye ndoa. Kwanza hakuna uvumilivu hapo; uvumilie nini wakati hujawahi kujaribu?

Heshima ya usichana wako ni zawadi nzuri sana kwa mwanaume ambaye ameitambua thamani yako na kuamua kufunga na wewe ndoa. Huyo ndiye anayestahili. Ikiwa utaamua kwa hiyari yako kutoa penzi, ni wewe tu, lakini isiwe kwa sababu ya kuonesha mapenzi.

LAZIMA NGONO?

Hakuna ulazima, wala faragha si kiashirio cha mapenzi ya dhati. Ngono ni kitu kingine na mapenzi ni kitu kingine. Hivi ni vitu viwili ambavyo havina uhusiano wowote. Asitokee mtu akakudanganya kwamba kwa kutoa penzi ndipo utaonesha unavyompenda. Si kweli. Kimsingi ngono huja baada ya tamaa kuingia kati ya wawili wanaopendana.

Hata hivyo, kuna uwezekano mkubwa, ukawa na tamaa ya kufanya ngono na mtu hata kama huna mapenzi katika moyo wako. Kimsingi suala la kufanya ngono siyo kithibitisho cha kuonesha mapenzi ya dhati.

Baadhi ya walio katika uhusiano, hudanyanywa na kipengele hiki. Utakuta msichana anaambiwa na ‘boyfriend’ wake kwamba ili aoneshe kuwa anampenda basi lazima akubali kufanya naye ngono.

Hata hivyo, baada ya kumaliza kufanya hivyo, kuna uwezekano mkubwa wa penzi hilo kuyeyuka! Ni kweli ni rahisi kuachwa kwenye mataa hasa kama mhusika alikuwa ameshikwa na tamaa badala ya mapenzi ya dhati.

No comments:

Post a Comment