MAPENZI!
Hivi umeshawahi kukaa chini na kujiuliza kwamba, kama yasingekuwepo
mapenzi ulimwenguni binadamu wangeishi vipi? Kimsingi ni swali gumu na
hakuna anayeweza kulitolea jibu la moja kwa moja. Ni sawa na wanaume
wanavyojiuliza kwamba wasingekuwepo wanawake wangeishi vipi.
Ninachotaka kukizungumzia leo ni kwamba, mapenzi yamekuwa yakiwasumbua walio wengi katika maisha yao hadi wengine kufikia hatua ya kujilaumu kwa nini wameingia katika ulingo huo.
Wapo ambao wamepoteza maisha kwa sababu ya mapenzi, wapo waliochanganyikiwa na wengine kuathirika tu kisaikolojia kwa sababu ya mapenzi. Pia wapo walioachishwa kazi kwa sababu ya mapenzi. Kimsingi mapenzi ni kitu hatari sana kama hakitawekewa umakini.
Lakini sasa licha ya mapenzi kuleta matatizo kwa binadamu, bado tunaambiwa kwamba, utakuwa peke yako kwa muda fulani wa maisha yako na mwishowe utatakiwa kutafuta mwenza ambaye utaishi naye kama mume na mke.
Swali la kujiuliza ni kwamba, je kama kila unapoingia katika mapenzi unaumizwa na mtu ambaye umempenda na ungetamani siku moja muoane, kuna ulazima wa kuendelea kung’ang’ania penzi lake? Na kama utaendelea kuling’ang’ania penzi la mtu ambaye anakuumiza kila wakati bila kujali, itakuwa inaleta maana?
Kimsingi katika maisha ya sasa hasa kwa wale ambao bado hawajaolewa au kuoa, wanatakiwa kuwa tayari kupenda na kupendwa lakini pia wanatakiwa kutopenda sana kwani madhara yake ni makubwa. Pia wawe tayari kuumizwa kwanza kabla ya kumpata yule mwenza mweye mapenzi ya dhati kwao.
Mapenzi ya sasa yamejaa usanii wa hali ya juu kiasi kwamba ukifanya uchunguzi utabaini wengi walio katika uhusiano wa kawaida yaani ‘boyfriend & girlfriend’ wanapitisha muda tu lakini uwezekano wa wao kuja kuwa kitu kimoja ni mdogo sana.
Unaweza kuwa katika uhusiano na mtu akawa anakuonesha mapenzi ya kweli mpaka mwenyewe ukajiona mwenye bahati lakini kumbe mwenzako anakufanyia usanii tu. Sasa utajuaje kwamba huyo uliyenaye hana mapenzi ya dhati kwako? Hapo ndipo penye shughuli pevu na ndiyo maana wakati mwingi tunajijengea imani tu. Tunaamini kwamba, kwa sababu ya mambo anayonifanyia mpenzi wangu, ni lazima atakuwa ameniweka moyoni mwake.
Tutambue tu kwamba mapenzi ya kujifanyisha hayawezi kuchukua muda. Utadanganya leo, utadanganya kesho lakini ipo siku mpenzi wako atabaini tu kwamba amedondoka katika penzi lisilo sahihi na hapo ndipo yaweza kuwa mwisho wa penzi hilo la bandia.
Ninachotaka kukushauri wewe msomaji wangu ni kwamba, unapotokea kuingia katika uhusiano wa kimapenzi na mtu kwa lengo la kutaka kuoana kisha yeye akaja kukuumiza kwa kukufanyia mambo mabaya, chukulia kwamba ni safari ya kuelekea kumpata mwingine mwenye mapenzi ya dhati kwako.
Najua utaumia sana lakini kutakuwa hakuna jinsi, kama yeye kaamua kukuacha huna nafasi ya kulirejesha penzi lake kwako kwa hiyo unatakiwa tu kukubaliana na hali halisi.
Ila sasa baada ya kuumizwa, hutakiwi kukurupuka kutafuta mtu mwingie wa kujaza nafasi hiyo. Hiyo ni mbaya sana kwani unaweza kujikuta unaingia tena katika penzi chungu kuliko hata lililopita. Kaa chini jiulize, mpaka kufikia mpenzi wako kukuacha ni wewe mwenye makosa au ni yeye?
Kama ni wewe lazima ujute kwanza na kuwa tayari kubadilika. Lakini kama utabaini kwamba hukuwa na kosa lolote bali uliyekuwa naye kaamua tu kukuumiza kwa sababu zake anazozijua, hilo muachie Mungu, yeye ndiye atakulipa wewe na aliyekutenda
No comments:
Post a Comment