Dar es Salaam. Moja kati ya sababu inayochangia wanafunzi wa
shule za msingi kumaliza shule bila kujua kusoma na kuandika inatokana
na kukosa mwongozo kuanzia ngazi ya familia kushindwa kuwanunulia vitabu
vya kujisomea.
Ni kwamba familia nyingi hazina utamaduni wa
kusoma vitabu, hali ambayo inasababisha pia kutowashawishi hata watoto
wao kusoma vitabu.
Idadi ya watu wasiojua kusoma na kuandika
Ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa
linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) inasema watu
wasiojua kusoma na kuandika Duniani wamefikia 774 milioni .
Ripoti hiyo inaeleza wazi kuwa idadi kubwa ya watu
hao wasiojua kusoma na kuandika wengi wao wanaishi katika bara ya
Afrika na Asia, na kwamba takwimu hizo zinaonyesha kiwango hicho
kimeongezeka wa asilimia nane kuanzia mwaka 1990.
Kwa upande wa Tanzania hadi kufikia mwaka 2002
idadi ya watu wasiojua kusoma na kuandika ilikuwa watu 6.2 milioni.
Idadi hiyo ni kwa watu wenye umri wa miaka 15 na kuendelea ambao ni sawa
na asilimia 31, lakini kwa sasa idadi hiyo imeongezeka na kufikia watu
zaidi ya milioni 14.
Mtaalamu wa Masuala ya Elimu kutoka Chuo Kikuu cha
Mtakatifu Augustine (SAUT) John Masanja, anasema zaidi ya watu
14milioni hawajua kusoma na kuandika hapa nchini na kwamba idadi hiyo
inasababisha washindwe kujitambua na kujishughulisha, hivyo kusababisha
umasikini .
Masanja anasema Serikali ina wajibu wa kuboresha
mifumo yake ya utoaji wa elimu, kwani bila kufanya hivyo kuna uwezekano
wa kurudi nyuma kimaendeleo na kiuchumi kutokana kuendelea kuwa na watu
wasiojua kusoma wala kuandika. Kutokana na tatizo hilo, Mradi wa Vitabu
vya Watoto nchini uitwao Children Books Project (CBP) umeanzisha progamu
ya usomaji wa vitabu katika shule za msingi 196 zilizopo katika wilaya
14.
Lengo la kuanzishwa kwa mradi huo ni kujenga
utamaduni wa kusoma kwa watoto wa shule za msingi kwa kuwapatia mafunzo
na vitabu bora vya kujisomea.
Mratibu wa Mafunzo na Ufuatiliaji kutoka CBP,
Marcus Mbigili anasema tathmini ya watoto wa shule za msingi inaonyesha
kuwa watoto wengi hawana uwezo wa kutosha wa kusoma.
Anasema Mradi wa Vitabu vya Watoto ulianzishwa
mwaka 1991 kutokana na hali mbaya iliyokuwepo ya ukosefu wa vitabu vya
kujisomea hasa vitabu vya watoto.
Mbigili anasema katika awamu ya kwanza ya mradi
huo, kazi kubwa ilikuwa kushirikiana na wachapishaji kuchapa vitabu vya
watoto huku awamu ya pili ilikuwa na malengo ya kushirikiana na
wachapishaji kuchapa vitabu, kushirikiana na walimu, kuboresha ujuzi wa
kusoma na kuimarisha wadau wa tasnia ya vitabu.
Mratibu huyo anafafanua kuwa katika awamu ya pili, pamoja na
kuwepo idadi kubwa ya vitabu vya watoto, bado kulikuwa na matatizo ya
kusoma miongoni mwa wanafunzi katika shule mbalimbali hapa nchini.
“Kutokana na matatizo haya, mradi wa CBP ulizindua
programu ya usomaji wa vitabu kwa baadhi ya shule za msingi kwa lengo
la kumfanya mtoto asome kwa maana ya kupata maarifa, ufahamu na
burudani”anasema Mbigili.
“Programu hii ilianza kwa majaribio katika shule
sita za Mkoa wa Dar es Salaam na sita kwa Mkoa wa Pwani na kazi kubwa
ilikuwa ni kutoa mafunzo kwa walimu wa shule hizo mbinu za kufundishia,
uanzishwaji wa maktaba, uandaaji wa vitabu na zana za
kufundishia,”anaongeza.
Shule zilizopo katika mradi huo wa CBP
Mpaka sasa jumla ya shule 196 kutoka wilaya 14 za
hapa nchini zimeunganishwa katika mradi wa huo na kwamba wilaya hizo ni
Kinondoni, Ilala, Temeke, Mkuranga, Bagamoyo, Halmashauri ya Wilaya ya
Kibaha, Halmashauri ya Mji wa Kibaha, Morogoro Mjini na Morogoro
Vijijini, Kilosa, Kisarawe, Rufiji, Mvomero na Kongwa mkoani Dodoma.
No comments:
Post a Comment