MAJONZI, huzuni na masikitiko
vimeikumba familia ya Lwena kufuatia mtoto wao mpendwa Dorryce Lwena
(27) kufariki dunia kwa kupigwa risasi mkono wa kushoto na ubavu wa
kushoto na watu wasiojulikana, Uwazi lilifuatilia.
Tukio hilo la kusikitisha lilitokea
mwanzoni mwa mwezi huu, saa tatu usiku, Uwanja wa Edosi, Kitunda, Ilala
hatua chache kutoka nyumbani kwa marehemu huyo.
Siku ya tukio, Dorryce ambaye ni
mwanafunzi wa Chuo cha Uhasibu Singida (DSA), alikuwa akitoka Kariakoo
kununua vifaa vya kwenda navyo chuo siku mbili mbele lakini kifo
kilimkuta akiwa anakaribia kufika nyumbani.
Kama ilivyo ada, baada ya kujulishwa
tukio hilo la kikatili, waandishi wa Uwazi walifika eneo la tukio na
kufanya mahojiano na baba wa kufikia wa marehemu ambaye alikuwa akiishi
naye baada ya baba mzazi kutengana na mama yake.
Baba huyo aliyejitambulisha kwa jina moja la Maganga alikuwa na haya ya kusema:
“Ilikuwa Jumamosi, Machi Mosi, mwaka
huu, saa tatu usiku nikiwa karibu na kwangu, mke wangu (mama wa
marehemu) alinipigia simu akaniambia kuna risasi zimepigwa karibu na
nyumba yetu, nikamwambia haraka sana wafunge milango na mtu asitoke nje
hadi itakapojulikana kuwa risasi hizo zilikuwa za nini.
“Muda mfupi baada ya kuongea na mke
wangu, dada wa Dorryce alinipigia simu akiniambia nirudi nyumbani
haraka kwani Dorryce amepigwa risasi na amefariki dunia.
“Nina gari, niliingia ndani yake haraka
tayari kwa safari ya kurejea nyumbani. Nikiwa nakaribia nyumbani
niliona kundi la watu, nilisogelea eneo hilo na kukuta mwili wa Dorryce
umelala katika dimbwi la damu.
“Nilikuta familia yangu, akiwemo mama
wa marehemu wakilia kwa uchungu. Iinibidi nikatoe taarifa Kituo Kidogo
cha Polisi Kitunda, nao walinishauri niende Kituo cha Polisi
Stakishari.
“Polisi walifika eneo la tukio na kufanya michoro kisha wakauchukua mwili hadi Hospitali ya Taifa Muhimbili.
“Mke wangu ana hali mbaya sana jamani.
Tangu tukio hilo amekuwa akizimia mara kwa mara, presha inapanda na
kushuka. Naombeni msimhoji,” alisema kwa masikitiko makubwa baba huyo.
Alisema mpaka siku hiyo familia ilikuwa haijui chanzo cha mauaji hayo.
Akasema: “Ninachokumbuka mimi siku hiyo
mke wangu alimkataza marehemu asiende Kariakoo lakini alikataa, akasema
kwa vile Jumapili atakwenda kanisani na Jumatatu ndiyo safari ya
kurudi chuo, afadhali aende siku hiyo.”
“Ila wakati marehemu yupo chuoni alizaa
na mwanaume mmoja ambaye tulimtaka amhudumie mtoto kwa vile mama yake
bado anasoma lakini alikataa, hivyo marehemu aliamua kumchukua mtoto na
kumpa. Hadi hapo tukawa hatuna uhusiano naye mzuri,” alisema mzee
huyo.
Waandishi wetu walifanya mahojiano na
majirani kutaka kusikia kama wanajua lolote juu ya tukio hilo ambapo
baadhi yao walisema mauaji hayo hayajawahi kutokea eneo hilo na kudai
kwamba marehemu ndiye anayejua sababu ya kupigwa risasi.
“Marehemu baada ya kupigwa risasi ya kwanza alilia kwa uchungu na kupiga kelele kuomba msaada. Hata hivyo, hakuna aliyejitokeza.
“Aliongezwa risasi ya pili sauti yake
haikutokea tena, wale watu walitimka na pikipiki ndipo wananchi
tukajitokeza, nahisi ni mapenzi,” alisema mwanamke mmoja anayefanya
biashara karibu na eneo la tukio.
Baba mzazi aliyejitambulisha kwa jina la Julius Jacob Lwena anayeishi Tabata Tenge, Dar yeye alikuwa na haya ya kusema:
“Kifo cha Dorryce kimeniuma sana, ila napenda kusema kwamba maisha yake kwa undani siyajui sana kwa sababu nilikuwa mbali naye.
“Mara ya kwanza marehemu alipomaliza elimu ya sekondari alijiunga na Chuo cha Polisi Moshi, alirudishwa kutokana na ujauzito.
“Baada ya kujifungua tulimpeleka Chuo
cha Utumishi Singida, bahati mbaya akapata mimba ya mwanaume mwingine,
ikabidi arudi nyumbani.
“Baada ya kujifungua tulimpeleka chuo cha uhasibu Singida na mauti yamempata alipokuja likizo,” alisema mzee huyo.
Marehemu alizikwa Machi 4, mwaka huu katika Makaburi ya Tabata Segerea jijini Dar. Mungu ailaze pema peponi roho yake. Amina
No comments:
Post a Comment