MKUU wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo ameliagiza Jeshi la Polisi mkoani humo, kumkamata Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema akihusishwa na uchochezi wa vurugu zilizotokea katika Chuo cha Uhasibu kilichopo Njiro jijini Arusha jana asubuhi.
Mulongo alithibitisha kukamatwa kwa mwanasheria wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Albert Msando ambaye anadaiwa kuwepo chuoni hapo na Lema pamoja na baadhi ya wanafunzi wanaodaiwa kuwa vinara wa vurugu hizo.
Vurugu hizo zilitokea jana saa nne asubuhi baada ya Mkuu wa Mkoa kufika chuoni hapo kwa ajili ya kuwasikiliza wanachuo ambao walitaka kuandamana kufuatia mwenzao Elly Kago (22) kuuawa na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia jana jirani na chuo.
Mulongo alifika chuoni hapo baada ya kupigiwa simu na Lema ambaye alifika mapema na kuzungumza na wanafunzi hao, huku akiwatuliza wasiandamane kufuatia kifo cha mwenzao.
Lema aliwaambia vijana hao kuwa mazingira ya nchi ya sasa ni magumu kufuatia wengi wao kukosa ajira na hivyo baadhi yao wasio wastahamilivu kujiingiza katika vitendo vya ujambazi na unyang'anyi.
Hivyo aliwataka wasiwe na jazba badala yake watafute ufumbuzi wa matukio hayo na kuangalia jinsi ya kumsitiri mwenzao.
Baada ya Mulongo kufika na kuwakuta wanafunzi wakizungumza na Lema, alipewa nafasi naye kuzungumza, lakini aliutaka uongozi wa chuo kuandaa vipaza sauti na mahala pazuri pa kuzungumzia.
Maelekezo hayo ya mkuu wa mkoa kutaka vipaza sauti yaliamsha maneno ya chini kwa chini na baada ya kuanza kuzungumza wanafunzi hao walianza kumzomea wakimlazimisha aache.
Alipokatisha hotuba yake, wanafunzi walianza kurusha mawe na hivyo kulazimika kuondolewa chuoni hapo pamoja na viongozi mbalimbali wa serikali chini ya ulinzi, huku mabomu yakirindima kuwatawanya wanafunzi hao.
Wanafunzi hao walisikika wakisema mkuu huyo ‘amewaboa’ kwa kuwa wao wana msiba yeye anaenda kudai vipaza sauti ili kusikiliza madai yao, huku akiwa amevaa suti, hatua iliyotafsiriwa kama kutojali msiba wao.
Alisema taarifa za awali za polisi zinasema kuwa vurugu na kifo cha mwanafunzi huyo vina mahusiano makubwa na masuala ya kisiasa kwa ajili ya watu kujijenga kisiasa na kwamba vyombo vya usalama vinaendelea na uchunguzi wa kina juu ya suala hilo.
Mkuu huyo wa mkoa hakutaja idadi ya wanafunzi waliokamatwa hadi jana bali alisema vinara wote wamekamatwa pamoja na Msando huku akisisitiza kuwa Lema ametoroka na anaendelea kusakwa.
“Jambo baya kwa leo ni siasa kuingia katika vurugu hizo, kwani Lema ndiye alihusika hata kuita viongozi wa serikali chuoni hapo ambapo aliingia hapo bila kufuata utaratibu na kuanza kuzungumza na wanafunzi,’’ alisema Mulongo.
Kaimu Mkuu wa Chuo, Dk. Faraji Kasida baada ya kupewa maagizo ya kukifunga chuo hicho ambacho kipo chini ya Wizara ya Fedha alitangaza kuwa kimefungwa kwa muda usiojulikana.
Vurugu hizi zimeibuka zikiwa zimebaki siku chache kabla ya kuanza kwa kampeni za uchaguzi mdogo wa madiwani katika kata nne za Jiji la Arusha.
No comments:
Post a Comment