Thursday, 11 July 2013

RAIS KIKWETE AWASHANGAA CHADEMA KUTAKA KAMBI YA KUJILINDA...DR. SLAA NAYE AWATAKA POLISI WAYAVUNJE MAKAMBI YA CCM


Rais wa Tanzania amewashangaa na kuwalaani CHADEMA kwa kutangaza kufundisha vijana namna ya kujilinda na kusema kuwa ni watu wa ajabu kama wamefikia huko.

Mh. Rais kayasema hayo katika kuhitimisha kongamano la amani  huku bwana Cheyo  nae akisema  kuwa  hata kama  ni kutaka kuwa rais wa nchi CHADEMA wamefika kubaya....


Wakati  mh. Rais  akiwashangaa CHADEMA,Katibu Mkuu wa chama  hiyo,  Dr Wilbroad Slaa amelitaka jeshi la polisi kuvunja mara moja makambi yote ya CCM nchini yanayotoa mafunzo kwa vijana wanaoitwa Green Guards.
 

Kauli  hiyo  ya Dr. Slaa  imekuja  baada  ya  polisi  kuwazuia  CHADEMA kuanzisha  kambi  yoyote  ya  kujihami  na  kwamba  hatua  kali  za kisheria  zitachukuliwa  dhidi  yao  endao  watakaidi  agizo  hilo

Dk. Slaa, amesema kauli ya Jeshi la Polisi inadhihirisha namna wahusika wasivyofahamu sheria kwa kile alichoeleza kuwa wao hawaundi majeshi bali vikundi vya ukakamavu.

Alisema ni heri msemaji wa jeshi hilo angekaa kimya kuliko kulifedhehesha Jeshi la Polisi kwa tamko lisilokuwa na ushawishi wa kisheria.


“Nawashauri hawa waanze na Tendwa…ila kwanini wameanza leo sisi tulishayalalamikia makundi ya CCM kwa barua na hata walipomaliza mafunzo yao kule Igunga tukapiga na picha wao hawakuinua mdomo kuliongelea,” alisema Dk. Slaa.

Alisema katika miaka minne iliyopita CHADEMA ilikuwa ikionyesha kwa ushahidi namna vijana wa CCM wanavyopewa mafunzo ya kijeshi, ikwamo silaha kutoka nje ya nchi huku wahusika wakiendelea kukaa kimya.

Aliongeza kuwa hali hiyo ya kuamka baada ya kauli ya CHADEMA inatia nguvu shaka yao, aliyodai kuwa makundi ya CCM yanafanya mafunzo kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi.

Dk. Slaa alitolea mfano kundi la vijana wa CCM walioweka kambi katika shule ya wazazi katika Kata ya Ivumwe, Mbeya mjini na kisha kuwateka katibu wa CHADEMA Mbeya mjini na baadhi ya wanachama wake.

Alisema katika tukio la Ivumwe wakati wa uchaguzi mdogo wa madiwani wa hivi karibuni, CHADEMA walitoa taarifa kwa Kamanda wa Polisi wa Mbeya ambaye aliwajibu kuwa wapeleke ushahidi kama vijana hao ni wahalifu.

Alibainisha kuwa CCM imekuwa na kawaida ya kukusanya vijana kutoka maeneo tofauti na kisha kuwapa mafunzo ya kijeshi na silaha kwa ajili ya kuwadhuru wapinzani na kutolea mfano Kambi ya Ulemo aliyosema ilikuwa na vijana waliopewa mafunzo ya kijeshi.

“Tunawasubiri tuone hatima yao ni nini, sisi tunajua Jeshi la Polisi limeshajitoa  kulinda viongozi wa CHADEMA sasa kwanini tusijilinde wenyewe,” alisema Dk. Slaa.

Source: BBC, Tanzania Daima,Jamii Forum

No comments:

Post a Comment