Monday, 21 October 2013

HASARA ZA MAPENZI YA KUCHUNGUZANA


Katika maisha mawazo ni kitu cha kawaida kwa mwanadamu, lakini hata hivyo matumizi ya akili lazima yawekewe mipaka na isiwe ni kitu cha kawaida ubongo kuruhusiwa kwenda mwendo mkali kulingana na uwezo wake.

Waundaji wa mashine, kwa mfano, wakati wanatengeneza injini waliweka mwendo kasi wa kiwango cha juu, hata hivyo huonya kuwa si kila wakati mwendesha chombo cha moto anaruhusiwa kutumia ‘spidi’ zote zilizomo ndani ya mashine yake.
 Hali hiyo ndiyo inayojitokeza katika uwezo wa ubongo katika kufikiri na kupata majibu ya kina ya nini kilichopo na kitakachotokea. Ni ukweli ulio wazi kwamba ubongo ni mashine kubwa yenye uwezo wa ajabu usioelezeka.

Watu wengi waliofanikiwa na wanaotaka kufanikiwa ni wale ambao wanajua namna ya kuutumia ubongo katika kupanga maisha yao. Kila unachokiona ni zao la ubongo kwani mawazo ndiyo mwanzo wa kila kitu kilichopo duniani. Binafsi naamini hata Mungu aliweza kabla ya kuumba ulimwengu.
 Lakini pamoja na umuhimu wa mwanadamu kutumia akili yake kupata majibu ya hisia, maono, mazingira na vitu anavyokutana navyo maishani, kuna wakati umuhimu huo hukosa maana na maonyo ya kuwa na udhibiti kasi ya fikra yanachukua nafasi.
  
Haijalishi mhusika ana uwezo wa kiasi gani ndani ya akili yake! Kumbuka pia onyo la dereva kutumia mwendo kasi kila anapowasha gari lake, halafu linganisha na akili yako au ya mwanadamu unayemtazama utagundua kuwa kithibiti mwendo kinahitajika hata katika mawazo.

Hebu chukua jukumu la kuutazama ulimwengu huu tulio nao na uangalie uozo wa wanadamu katika kujiheshimu, kisha ujiulize hivi kuna mwanaume au mwanamke ambaye anaishi bila kumsaliti mpenzi wake? Baada ya swali hilo wachukue rafiki zako unaokunywa nao pombe na kufanya kazi nao kazi uone kama hamjawahi kuoneshana nyumba ndogo, baadaye fumba macho uiulize akili yako kuna asiyesalitiwa?

Wakati unasubiri majibu endelea kuweka viashiria kichwani mwako kwa kumfikiria mkeo anayemhudumia bosi chai huko ofisini au Muuguzi anayefanya kazi chumba kimoja na Daktari usiku au askari polisi aliyeolewa anayekesha lindoni na bachela, kisha subiri majibu kutoka kwenye ubongo wako!

 Bila shaka kwa mchakato huo mfupi tu majibu ya haraka yatakayokuja ni hakuna asiyesalitiwa. Isipokuwa kuna kuuficha ukweli. Sasa kwa majibu hayo ya akili mkeo unampenda nini wakati unafahamu kuwa anatoa penzi kwa wanaume wengine kama wewe.

Thamani ya ndoa na umuhimu wako unatoka wapi, tuseme hupati uchungu pale unapohisi unaibiwa mumeo? Kama unapata inakuwaje pale akili inapokupa majibu kuwa mkeo si mwaminifu?
Hapa ndipo penye kiini cha somo letu kwamba, kuna wakati tunaruhusu mawazo yetu yakimbie mwendo kasi kwenye njia yenye mabonde na kona na wengi wetu tumeharibu ndoa zetu na wengine tumeachana na wapenzi wetu kwa ujinga wa kutokuzuia kasi ya akili zetu.

Inashangaza kusikia na kuona kuna baadhi ya wanandoa wanaishi kwa kupelelezana kila siku kama askari wakaguzi wa dawa za kulevya. Mke akichelewa kurudi lazima akaguliwe kwanza kama hakutoka kupasha mwili nje, kadhalika mwanaume  apimwe kwa kunuswa kama hakuchepukia nyumba ndogo.

Hivi tulishawahi kujiuliza kuwa tunautumia ubongo wetu vibaya kutafuta ufumbuzi wa mambo ya kipuuzi!? Tunawafuatilia wake zetu maofisini kwao ili iweje? Hatuaminiani kwa nini wakati tumeoana, je mapenzi yana faida gani ndani ya usaliti na kujua kuwa sio wewe peke yako unayefaidi tunda la mkeo au mumeo.

Wakati nikitafakari kuhusu mada hii kaka mmoja aliniambia kuwa amempata mchumba ambaye ni mzuri sana , anampenda na kumheshimu, lakini alitaka kujua atawezaje kumwamini kuwa hatamsaliti? Kabla sijamjibu akajaza hoja nyingine kwamba kuna watu kibao wanamsumbua mchumba wake kwa maana hiyo ana shaka kuna siku atalegeza msimamo na kumsaliti!

 Binafsi sikufikiria sana kumjibu swali lake, bali nilimwambia kuwa jibu la swali lako ni KUJIMILIKISHA UJINGA. Nikiwa na maana ile ile ya kudhibiti mwendo wa akili yake kwa kuacha kuwaza mambo ambayo yanaashiria kutumia mwendo kasi wa akili kwenye njia mbaya. Siku zote kushinda maisha kunahitaji uwezo wa mwanadamu wa kujua ni wapi awaze sana na kupata ufumbuzi na wapi awaze kidogo au asiwaze.

Maana haiwezi kuwa busara kwa mtu aliyemfuma mkewe na mwanaume mwingine atumie akili kujua  ilikuwaje mpaka kukawepo makubaliano au msukumo upi ulimvuta mkewe kuutoa utu wake kwa mwanaume mwingine?

 Inapofikia hatua hiyo umuhimu wa kulegeza mwendo wa akili kwa kusema sijui na sina haja ya kujua ilikuwaje, hata kama akili bado ina uwezo wa kujua mengine zaidi sema sitawaza juu ya jambo hili la kipuuzi! Ukifanya hivyo utakuwa sawa na dereva anayeendesha gari lenye injini yenye kasi kubwa lakini ameamua kwa makusudi tu kupunguza mwendo kwa usalama wa maisha yake.

 Hii ndiyo siri ya usalama wa ndoa na uhusiano wa mapenzi ndani ya hofu ya usaliti. Ukiona mawazo yanakuja kutaka kutoa jibu la kuchelewa kwa mumeo kurudi huku dondoo za kuwepo kwa msichana mwingine kazini kwake zikichipuka, yatupilie mbali mawazo hayo. NDOA MAANA YAKE NI KUAMINIANA. UKIONDOA UAMINIFU HAKUNA NDOA!

No comments:

Post a Comment