KILA ndoa ina matatizo, na yanaweza kufumuka wakati wowote. La muhimu ni
kwamba unapokuwa umeamua kujiingiza katika maisha ya ndoa unapaswa
kujifunza jinsi ya kukabiliana na matatizo hayo ili yaweze kuisha salama
na ndoa kuendelea kuwa salama.
Bila kujali umeenda umbali gani
katika barabara hii ya ndoa, zipo kanuni rahisi lakini za muhimu za
usalama katika barabara hii. Si rahisi sana kuzitekeleza kanuni hizi,
kwa wanandoa walio wengi, lakini ni lazima kuzitekeleza iwapo wahusika
wanapenda ndoa yao iwe salama.
Iwapo utazingatia kanuni hizi,
utaifanya ndoa yako kuwa imara zaidi. Katika usalama huu utapata pia
marupurupu – furaha, ngono, kuaminiana (kuaminiwa), mapenzi moto moto na
kadhalika. Hebu sasa na tuziangalie kanuni zenyewe: -
1. ONESHA MATENDO YA KIMAHABA
Usipojishughulisha
kwa lolote lile kwa ajili ya kumfurahisha mpenzi wako utasababisha
mwenzako achoke na hata kufikia mahala akakasirika. Ili kuepuka haya,
hakikisha kuwa unayapa kipaumbele mambo ambayo yanamfanya mpenzi wako
kujihisi maalumu kwako. Na njia rahisi zaidi ni kuwekeza katika matendo
madogo madogo ya kimahaba.
Kumbuka, kauli moja hasi au ya kuvunja
moyo inaweza kuhitaji kauli kama ishirini chanya ili iweze kufifia (si
kufutika) akilini mwa mpenzi wako. Hii ina maana kwamba, badala ya
kumlaumu mpenzi wako, wekeza zaidi katika kumsifia katika mambo yake, au
mambo anayoyafanya utakavyo.
Msifie mpenzi wako kwa nguo yake
mpya, msifie kwa kukujali, mpigie simu ofisini kwake na kumwambia kuwa
ulikuwa unamuwaza na kadhalika. Isipokuwa, hakikisha kuwa sifa hizi na
kauli hizi za mahaba zinadhihirika kutoka moyoni, zisije kuwa kama
mazoea tu.
Iwapo utafanya hivi, ni rahisi sana kumfurahisha
mpenzi au mwenzi mwenye nia njema na wewe. Kumbuka mambo yenu yalianza
hivi hivi, pale mlipokuwa bado mnafukuziana. Matendo madogo ya kimahaba
hayapaswi kuwa na mwisho, maana ndiyo hudumisha msisimko wa wenza.
2. TUMIA HISIA ZA MGUSO
Hisia
za mguso ni muhimu sana kwa wapenzi. Na njia mojawapo ya kumweka mpenzi
wako katika utayari wa kukupa kila kitu ni kumshika mkono unapotembea
naye kwenda dukani. Naam, Afrika hii unaweza kusemwa na hata kuchekwa,
lakini la muhimu kwako ni kwamba unamfanyia mwenzi wako wa maisha.
Unapomsalimia
mwenzi wako, gusa mashavu yake kwa ncha za vidole vyako. Jikumbushe
jinsi ulivyokuwa unamgusa katika siku za kwanza, kabla hujamzoea.
Ulikuwa ukimgusa kwa huba na tamaa kubwa. Mbusu kila panapoweza
kubusika, pitisha mkono wako kwenye nywele zake, na kadhalika. Kugusa ni
lugha muhimu ya mapenzi. Itaongeza msamiati wako wa mapenzi.
Sanjari
na kumgusa, onesha pia kuwa unamuunga mkono mwenzako. Unapotokea
ugomvi, wewe nenda upande wa mwenzi wako. Pia mtunzie siri zake maana
wewe ndiwe mwandani wake. Hata kama huko kazini au kokote watu
watazungumza siri za wenzi wao, wewe siri za mwenzako ziache kuwa baina
yake na wewe.
3. KUMBUKA HAKUNA MKAMILIFU
Unapokasirika,
au kukatishwa tamaa, au kuvunjwa moyo au kufadhaishwa, unaweza kushindwa
kujizuia kumlaumu aliyekusababishia hali hiyo, hata kama mtu mwenyewe
ni mwenzi wako wa maisha. Pia, ni kawaida kwa mtu kujaribu kumbadilisha
mpenzi wake anapodhani ana udhaifu fulani.
Hata hivyo,
unapojaribu kumkosoa na kumrekebisha mpenzi au mwenzi wako unamweka
katika hali ya kujitetea. Matokeo yake ni kwamba hatabadilika na pengine
ataacha kuwajibika. Matokeo mengine ni kwamba furaha yake itaondoka.
Kumbuka, unapomkosa mwenzako ni kama vile unapuuza asilimia 90 ya hulka
yake njema ambayo ilikufanya uvutiwe kuwa naye.
Kama kweli
unataka kumpa kipaumbele mwenzako na kisha kutarajia mazuri kutoka
kwake, basi badala ya kutaka kumbadilisha yeye, badilika wewe mwenyewe
kwa kuondoa mapungufu yako mwenyewe. Iwapo utajirekebisha, mpenzi wako
hatasubiri umlaumu au umgombeze, bali yeye pia atabadilika.
Katika
suala hili, ni vema kutambua kuwa hakuna mtu mkamilifu – si wewe, wala
yeye, wala mwingine. Mungu tu ndiye mkamilifu. Siku nyingine mpenzi wako
akifanya jambo ambalo unahisi linakukera, acha kuhemka. Badala yake,
jifariji kwamba alikuwa na lengo zuri japo matokeo hayakuwa mazuri. Na
kila siku, wiki au mwezi, chagua jambo moja ambalo unaliona kuwa zuri
kwake, kisha litaje. Linaweza kuwa ucheshi, utani na kadhalika.
Yaangalie hayo yaliyo chanya tu.
4. FAHAMU KUGOMBANA VIZURI
Migogoro
katika ndoa ni kitu cha kawaida. Naam, wengine husema ndoa isiyo na
migogoro ni sawa na kusema imekufa. La muhimu ni vile unavyokabiliana na
migogoro hiyo.
Kwa hakika, kushirikiana katika kutatua migogoro
ni vema zaidi kuliko kuhangaika mwenyewe. Naam, kama kila mmoja atakuwa
na nia njema, migogoro inaweza kuwa njia mojawapo ya kuzidi kushikamana
na mwenzako. Ni kwa kufahamu namna njema ya kukabiliana na migogoro
ndipo mtu huweza kumpenda mwenzake kama alivyo.
Kumlaumu mwenzako
ni kitu cha kuepuka kwa gharama yoyote. Pia, acha kukabiliana naye kwa
maneno, kwani utakuwa unawasha moto ambao haitakuwa rahisi sana kuuzima.
Wanandoa wenye furaha ni wale ambao huepuka sana kutumia vinywa vyao
dhidi ya wenzao. Hawa hufahamu jinsi ya kuzuia mazungumzo kulipuka na
kuwa ugomvi. Watu hawa hujitahidi kuepuka maneno ya kujiapiza kama
“kamwe” na kadhalika.
Iwapo ugomvi utatokea (naam, hakika
utatokea), jaribu kubadilisha mada, ingiza ucheshi, mwoneshe mwenzako
mapenzi ya ziada. Kama utabaini kuwa tayari umechelewa, tafuta suluhu
kwa kuondoka kwanza na kurudi baadaye kuendelea kuzungumza kila mmoja
anapokuwa katika nafasi nzuri ya kutumia vema akili yake.
5. ZUNGUMZA NAYE KWA MUDA MUAFAKA
Usianzishe
mazungumzo magumu au makali na mwenzi wako kama hauko mahala muafaka na
wakati pia si muafaka. Njaa na uchovu vinaweza kusababisha mtu kujibu
hovyo au kutojali. Pia si vema kumuuliza jambo mwenzako iwapo mmoja au
nyote mmepata kileo.
Vilevile, epuka kuzungumzia masuala magumu
ya kimahusiano iwapo jicho la pili litakuwa limeelekezwa kwenye kitu
kingine. Zima TV, pia zima simu na laptop. Kama ulikuwa unasoma gazeti,
lifunike ndipo uanze kuzungumza na mwenzako masuala nyeti ya kimaisha.
Kama ukiona mazingira hayaruhusu, chagua wakati mwingine.
Lakini
pia, kabla hujaanza mazungumzo na mwenzako, jiulize iwapo hutasababisha
rabsha. Jiulize, je, mazungumzo yetu yataisha kwa furaha? Kama utabaini
kuwa yanaweza yasiishe kwa furaha basi acha na kupanga siku nyingine.
6. TUMIA VEMA MASIKIO YAKO
Jambo
hili la mwisho ni muhimu sana katika kuimarisha uhusiano wa kindoa.
Ukitaka kupunguza migogoro baina yako na mwenzako, jifunze kuzungumza
kidogo na badala yake kuwa msikivu zaidi. Kauli za lawama, matusi,
kukosoa na nyingine za aina hiyo hubashiri mwisho wa uhusiano. Na hata
kama uhusiano hautaisha lakini ni rahisi ndoa kuwa ndoana.
Mazungumzo
yako na mwenzako yanapoanza kuchemka na kuonekana kama vile yanaelekea
kubaya, epuka kumkata kauli mwenzako – iwe ni kwa kutoa suluhisho au
kujitetea. Mwenzako anapokuwa na kitu kifuani, anataka kusikilizwa. Kwa
hiyo msikilize na uoneshe kuwa unamsikiliza kwa kutikisa kichwa
(juu-chini), au kumwitikia kwa mguno wa kumwonesha kuwa unamsikiliza na
kuheshimu maneno yake.
TIMIZA WAJIBU WAKO
Iwapo
utayazingatia mambo haya sita utakuwa umejenga msingi imara kwa mpenzi
wako kuwa wazi kwako na kukupa mapenzi yote. Namna hii, japo ndoa yenu
inaweza kupita kwenye misukosuko mara kwa mara, lakini itaibuka kidedea.
No comments:
Post a Comment