SURA ya mauzo katika sinema za Kibongo, Elizabeth Michael Kimemeta ‘Lulu’ ametoa ya moyoni kuwa kama siyo kuwekwa nyuma ya nondo za Mahabusu ya Segerea, Dar basi yangemkuta mazito.
Marehemu Steven Kanumba ‘The Great’.
Lulu alikaa Gereza la Segerea kwa takribani miezi kumi baada ya
kutokea kifo cha aliyekuwa mwandani wake, marehemu Steven Kanumba ‘The
Great’ aliyefariki dunia Aprili 7, 2012.Nyota huyo wa Filamu ya Foolish Age alifunguka mambo ya kushangaza hivi karibuni juu ya tukio hilo kupitia Kipindi cha Take-One, kinachorushwa na Clouds TV.
TATIZO FOOLISH AGE
Lulu alikuwa akizungumzia filamu yake hiyo ya Foolish Age ambapo alisema sinema hiyo inawasihi wasichana ambao wanapitia kipindi cha balehe ambacho ni hatari sana kwao.
“Kwa kweli kipindi cha foolish age ni cha hatari sana, nilicheza filamu hiyo ili kuwaasa wasichana wenzangu.
“Asikwambie mtu, mimi mwenyewe nilikokuwa nikielekea si kuzuri kabisa.
KAMA SIYO KANUMBA
“Ukweli ni kwamba kama siyo matatizo (kifo cha Kanumba) nikaenda mahabusu sijui ingekuwaje sasa hivi. Kukaa jela kulinisaidia kusitisha kasi ya tabia yangu, nikatoka nikiwa mpya.
“Yangenikuta mazito zaidi maana kipindi kile ilikuwa hatari tupu,” alisema Lulu ambaye ni mrembo wa haja.
Staa huyo aliongeza kuwa kipindi hicho kilikuwa cha hatari na hakitamani kijirudie hata kidogo katika maisha yake.
Alisema kwamba si ajabu inawezekana kipindi hicho ndicho kilisababisha matatizo yote yaliyomkuta. Alisema alikuwa akielekea kubaya.
HATAKI KIJIRUDIE
“Ni kipindi ambacho siwezi kukuhitaji tena katika maisha yangu si kizuri na kinatisha maana kuna wakati nilikuwa sisikii la mtu yeyote hata mama yangu mzazi,” alisema Lulu ambaye baada ya kutoka mahabusu haonekani akirandaranda mjini kama zamani.
Kabla ya utulivu huo alioupata nyuma ya nondo, Lulu alikuwa hakauki kwenye kumbi za usiku za starehe huku akilewa tilalila na kuyaweka maisha yake hatarini endapo angefanyiwa kitu mbaya.
Lulu alihusishwa na kifo cha Kanumba kwa kuwa siku ya tukio alidaiwa kuwa naye eneo la tukio ambapo alikamatwa na baadaye kuachiwa kwa dhamana akisubiri kesi ya kuua bila kukusudia.
SKENDO MPYA
Wakati hayo hayajapoa kumeibuka skendo mpya inayomgusa staa huyo mkubwa Bongo.
Madai mazito yameshushwa na wafuatiliaji wa mambo ya watu kuwa nyuma ya mwanadada huyo anayeng’ara kuna mbunge maarufu anayemiliki jimbo kwa kura za wananchi jijini Dar (tutamtaja baadaye).
ILIKUWA HIVI
Sosi: Hivi ninyi Global siku hizi hamuandiki skendo za mastaa?
Global: Tunaandika sana kwani vipi?
Sosi: Mna habari?
Global: Tunazo nyingi fuatilia magazeti yetu lakini ukitupatia ya kwako tutairusha hewani.
Sosi: Sasa mimi nina habari yangu.
Global: Inakuhusu wewe? Funguka.
Sosi: Hainihusu mimi. Ni ya ‘Kalulu Kadogo’.
Global: Siku hizi amekua, sema Lulu inatosha. Eeh... hiyo habari ikoje?
Sosi: Kwa taarifa yenu siku hizi anatoka na mbunge (anamtaja). Ndiye kamnunulia lile gari analokatiza nalo mjini na kampangishia bonge la mjengo kule Tegeta (Dar). Fuatilieni kwa watu wake wa karibu, naombeni msinitaje.
Global: Hatuwezi kukutaja ngoja tuzame mzigoni.
Gazeti hili lilifanya uchunguzi wake kwa watu wa karibu wa Lulu na kubaini kuwa ni kweli kwa sasa staa huyo amehama Tabata alikokuwa akiishi na mama yake, Lucresia Karugila na kuhamia kwenye bonge la mjengo Tegeta huku akisukuma gari kali (aina haikujulikana mara moja).
Madai mengine yalisema kwamba mke wa mbunge huyo alishamtafuta Lulu na kumuonya kuachana na mume wake.
LULU AFYATUKA
Baada ya kujiridhisha kuwepo madai hayo, juzi gazeti hili lilimtafuta Lulu na kumsomea mashitaka yake mwanzo hadi mwisho ambapo alifyatuka:
“Hivi ni nani anayeleta habari zangu Global? Analipwa na nani? Maana kila kukicha unasikia hili, halijapoa unasikia lingine.
“Si kweli kwamba natembea na huyo mbunge. Kwanza sina mazoea naye. Nakumbuka nilimuona mara moja tu sikumbuki ilikuwa kwenye shughuli gani.
“Huyo mkewe mimi simjui anafananaje. Nasema huko ni kuchafuana kusikokuwa na maana.”
VIPI KUHUSU KUPANGISHIWA NYUMBA?
“Ni kweli nimehamia Tegeta lakini sijapangishiwa, nimepanga mwenyewe. Hivi nikifanya jambo lazima iwe kuna mwanaume? Watu waache hizo. Wabadilike.”
VIPI KUHUSU GARI?
“Gari ninalo muda mrefu nimenunua kwa fedha yangu. Halina mkono wa mbunge, ni jasho langu.”
Kabla ya kuwekwa mahabusu, Lulu aliwahi kudaiwa kuhongwa nyumba na mbunge mwenye kitambi kikubwa, ishu hiyo aliikanusha kwa nguvu zote.
No comments:
Post a Comment