Katika maisha ya familia ndani ya jamii ni muhimu kwa mzazi kujenga utamaduni wa kumfunza watoto wako namna bora ya uvaaji.
Ikiwa mzazi utawajengea utamaduni wa mavazi watoto
wako na kumjengea utaratibu wa kumvalisha vazi fulani huku na wewe
ukiwa muumini wa vazi hilo, linaloakisi ustaarabu na utanashati ni wazi
kuwa mtoto wako atajengeka hivyo.
Kama wewe ni mvaaji wa nguo za heshima na
kumvalisha mavazi aina hiyo mtoto wako ni wazi utamjenga hivyo, lakini
pia ukimvisha kimini au kaptura ni wazi katika kuwa katika akili yako
kutakuwa na mavazi hayo tu pia atajengeka hivyo.
Kwa kuwa akili ya mtoto huamini zaidi kile
anachofanya mzazi wake awe baba au mama ni wazi kuwa itakuwa vigumu
kumbadilisha mtoto huyo. Kitakachofanyika itakuwa ni yeye kukua katika
msingi uliomwanzishia.
Hapa ndipo Waswahili walipokuja na usemi kuwa; “Mtoto umeleavyo ndivyo akuavyo.”
Wakati mwingine lawama tunazowapa vijana au watoto
tunaokutana nao barabarani wakiwa na mavazi ya ovyo huwa siyo zao bali
za wazazi wao, kwani kabla ya kuwalaumu tunatakiwa kuelewa kuwa kila
mtoto ana mzazi ama mlezi wake.
Kila mzazi au mlezi ana mwongozo wake katika
ufanyaji wa kila kitu ndani ya familia yake. Kuna mwongozo wa mavazi,
kuna mwongozi wa kula, kuzungumza, hata saa za kurudi nyumbani.
Inawezena huo ndiyo mwongozo waliopewa na vijana
tunaozungumzia hapo. Kumbuka kuwa mzazi ndiyo mtu wa kwanza kumwona
mtoto wake anapotoka nyumbani, hivyo kama hakumrekebisha akiwa nyumbani
ni wazi barabarani tutakaomwona tutabaki kuguna tu.
Mara nyingi mwongozo kwa mtoto hutumika kama
sheria zinazozilinda nyumba zetu. Ikiwa mwongozo wa nyumba fulani
unasema saa kumi na mbili jioni ni muda wa mwisho mtoto kuingia
nyumbani, basi muda huo watoto wote hutakiwa kuwa nyumbani kuendelea na
ratiba nyingine. Vinginevyo kinachofuata ni adhabu.
Hili husimamiwa hivyo hata katika suala la mavazi.
Ikiwa mzazi unataka kuweka mwongozo unaofaa kwa mavazi ya watoto wako.
Kumbuka kuwa kile unachomvalisha ndicho atakachokiamini hata atakapokuwa
nje ya nyumba yako.
Ni vizuri kuwajenga watoto wetu katika mavazi ya
stara. Haya yatachangia siyo tu kuwafanya waheshimike, bali pia
kuwafanya wawe na ujasiri na kuwaongezea uwezo wa kujiamini.
Mara nyingi mavazi ya nusu uchi, huchangia kwa
kiasi kikubwa kudharauliwa kwa watoto wetu, kwani watu wanaowatazama
huanza kuwapima kutokana na mavazi yao kwanza.
Wazungu husema; “Mavazi yako yanazungumza mengi kuliko maneno
yako.” Hivyo, kama wazazi tunapaswa kulijua hili. Tuwajengee watoto wetu
utamaduni wa kuvaa mavazi ya stara, kwani mavazi ndiyo msingi wa kila
kitu.
Tukumbuke kuwa watoto hujisikia huru kuvaa vazi walilolikopi kutoka kwa wazazi wao.
No comments:
Post a Comment