Sunday, 2 February 2014

Wasaliti na wakaidi CCM sasa basi, asema Kanali Kinana


Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana  

Tishio hilo lilitolewa jana na Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana alipokuwa akiwahutubia wananchi wa Kata ya Nsalaga jijini Mbeya.


Chama Cha Mapiduzi (CCM), kimetishia kuwatimua mara moja, wanachama wasaliti na wasiokubali kushindwa wakati wa kura za maoni za kuwania kuteuliwa ili kugombea urais, ubunge na udiwani.

Tishio hilo lilitolewa jana na Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana alipokuwa akiwahutubia wananchi wa Kata ya Nsalaga jijini Mbeya.
Kiongozi huyo mtendaji wa CCM alikwenda katika eneo hilo kukagua kazi za maendeleo ukiwemo ujenzi wa Ofisi ya CCM ya kata inayojengwa kwa nguvu za wanachama.
Kinana alisema Kata ya Nsalaga ina diwani wa upinzani na kwamba hiyo imetokana na CCM kukosea kuteua mgombea asiyetakiwa na wapigakura.
Alisema sababu nyingine ni usaliti unaotokana na walioshindwa katika kura za maoni ya kuwania kuteuliwa kuwa wagombea.
“Wasaliti walio CCM sasa basi, hawatavumiliwa na watakaogundulika tutawaonyesha njia ya kwenda wanakotaka,’’ alisema.
Kuhusu ujenzi wa Ofisi ya CCM, Kinana aliwapongeza wananchi wa kata hiyo kwa kujenga ofisi kubwa kwa njia ya kujitolea.
Alisema wakati umefika kwa Watanzania kufufua moyo wa kujitolea katika kujenga shule, zahanati na kutengeneza barabara za mitaani kama ilivyokuwa enzi za Mwalimu Hayati Mwalimu Julius Nyerere.
Mapema, Kinana alishiriki katika kazi ya kupalilia shamba la mjane Marge Kulimwa (76) kwa muda wa saa mbili.
Shamba hilo liko katika eneo la Mlima Nyoka, nje kidogo ya Jiji la Mbeya na katika mazungumza yake, aliwataka viongozi wa CCM katika ngazi zote kuwatembelea wakulima kwenye mashamba na kuonyesha mfano ili kuwatia moyo.
Kinana alisema tayari amewapa maagizo viongozi wa CCM kutembelea mashina yote nchini na kwamba sasa anawahimiza kuwatembelea pia wakulima kwenye mashamba yao na kushiriki kazi za kilimo kama njia ya kuwaenzi wakulima.
Katibu Mkuu na viongozi wakuu wengine akiwamo Makamu Mwenykiti wa CCM, (bara) Philip Mangula wapo jijini hapa kuhudhuria maadhimisho ya miaka 37 ya CCM .

No comments:

Post a Comment