Wednesday, 5 February 2014

Nani atazima moto wa Lowassa CCM


WanaCCM msiwe na shaka, tutavuka kwa nguvu zetu... wingi wenu  huu unanipa  faraja kuwa katika safari yetu na kwa kumte gemea Mungu tutashinda ...Tulifurahi pamoja, tulihuzunika pamoja na tutashinda pamoja.”
   

Tangu Lowassa atoe kauli kuhusu ‘safari yake ya matumaini’ zimetolewa kauli nyingi za ama kupingana naye au kumsapoti katika safari hiyo, hivyo kuhatarisha mshikamano wa CCM.

Nguvu ya makundi ya watu wanaotajwa kuwania urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) zinaendelea kukitikisa chama hicho huku makada wake wakitoa angalizo wakiutaka uongozi wa juu wa kuchukua hatua haraka  za kinidhamu kwa wahusika.
Wiki iliyopita wanachama wa chama hicho wanaodaiwa kutoka katika kambi tofauti zinazoisaka nafasi ya urais waliibuka na kutoa kauli zinazoonekana wazi kupigana vijembe, kila upande ukiuponda mwingine kuwa unavunja kanuni na katiba ya chama hicho.
Malumbano hayo ya makada wa CCM yanayoonekana dhahiri kuchagizwa na makundi pamoja na wafuasi wa vigogo wanaousaka urais kupitia chama hicho.
Ingawa makundi yanayosaka urais kupitia chama hicho ni mengi, ni kundi moja tu linalomuunga mkono aliyekuwa waziri mkuu, Edward Lowassa ndilo linaloonekana dhahiri kupigiwa kelele kwa kutajwa kwa majina bila kificho, hasa baada ya kauli yake kuwa ameanza safari, aliyoitoa mbele ya wageni wakati wa kuadhimisha mwaka mpya 2014.
Kutokana na kauli hiyo na mambo mengine, Katibu wa Uhamasishaji na Chipukizi wa UV-CCM, Paul Makonda aliibuka na kumshambulia Lowassa, suala ambalo limeyaibua makundi mengine, baadhi  yakiunga mkono kauli ya Makonda na mengine yakiibeza na kumshushia tuhuma za kuvunja kanuni za chama.
Mmoja kati ya waliojitokeza ni Makamu Mwenyekiti mstaafu wa CCM, John Malecela ambaye ameonyesha waziwazi kutofautiana na mipango na mikakati ya Lowassa.
Malecela anamuunga mkono Makonda, kwa kauli yake, ikiwamo kwamba Lowassa anafadhili mikakati ya kupingana na juhudi za sekretarieti ya CCM chini ya Katibu Mkuu, Abdulrahaman Kinana na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye.
Wakati Makonda na Mzee Malecela wakitoa tuhuma hizo, makundi mbalimbali ya Jumuiya ya Vijana UVCCM nao wameibuka na kumshutumu Makonda kuwa aliyoyasema ni maoni yake na siyo msimamo wa Jumuiya hiyo.
Kauli hiyo ya Makonda imeibua malumbano baina ya viongozi wa jumuiya hiyo, wengi wakimshutumu kwa “kutumiwa kumchafua Lowassa” na kwamba kauli aliyoitoa ni ya kwake na idara yake, wala isihusishwe na Umoja wa Vijana wa CCM.
Baadhi ya waliojibu ni pamoja na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) kupitia kundi la vijana, Jonas Nkya na Ramadhani Kimwaga,  pamoja na Mjumbe wa Baraza Kuu la jumuiya hiyo Mkoa wa Mbeya, Adam Mwakalinga.
Vijana hao kwa nyakati tofauti wanasema wamehuzunishwa na matamshi ya Makonda akimshutumu Lowassa na kutamka kuwa umoja huo hautaki kuingizwa katika masuala binafsi ambayo yanaweza kukigawa chama na jumuiya zake.
Mwakalinga anasema Makonda anapaswa kufanya kazi ya idara yake ya watoto badala ya kukurupuka na kutaka kuwaaminisha Watanzania kuwa Edward Lowassa si kiongozi mzuri huku akijua wananchi wenyewe na hata wapinzani wanaona uthubutu wake katika maendeleo hasa kwa vijana.

No comments:

Post a Comment