WAZIRI Mkuu mstaafu, Edward Lowassa amevitaka vyombo vya dola
na wafanyabiashara wakubwa nchini, kujenga mahusiano bora kati yao na
wafanyabiashara ndogo ndogo (Machinga) ili kuondoa tabaka la matajiri na
masikini linaloweza kuathiri uchumi wa taifa.
Lowassa
aliyasema hayo jana wakati akizungumza na machinga wa eneo la Makoroboi
jijini Mwanza, ambao pamoja na mambo mengine aliwachangia sh milioni 20
kwa ajili ya kutunisha mfuko wao.
Mwanasiasa
huyo ambaye pia ni mbunge wa Monduli, aliinyoshea kidole Serikali ya
chama chake cha Mapinduzi (CCM) na kuitaka ihakikishe inatekeleza kwa
vitendo ilani yake inayosisitiza wananchi kuwezeshwa kiuchumi ili
kuondoa matabaka.
Huku akishangiliwa na
wafanyabiashara hao, Lowassa ambaye aliongozana na baadhi ya makada wa
CCM kutoka ndani na nje ya Mwanza, alisema kila mwananchi wa Tanzania
lazima ale, ingawa kwa namna tofauti.
Alisema kuwa ili amani iwepo nchini, lazima Jeshi la Polisi na wafanyabiashara wakubwa wawathamini wafanyabiashara wadogo.
“Tunataka
tuwasaidie hawa vijana wetu, maana ni nguzo kubwa sana katika maendeleo
ya taifa. Ilani ya CCM inasema lazima watu wawezeshwe kiuchumi.
“Kwa
maana hiyo katika nchi yetu kila mtu lazima ale. Na kula kwenyewe
tunatofautiana, huyu anakula mkate na huyu anakula hiki. Na ili amani
iwepo lazima RPC au OCD na wafanyabiashara wawathamini machinga,”
alisema Lowassa.
Pia alitahadharisha kuwa endapo wafanyabiashara hao wadogo watadharauliwa katika nchi, lazima watakula sahani moja na matajiri.
Alitumia pia fursa hiyo kukanusha tuhuma dhidi yake kwamba amejilimbikizia mali.
“Wapo
baadhi ya watu wanasema hela ninazotoa hizi ni zangu. Mimi sina fedha,
ninazotoa ninapewa na marafiki zangu. Mimi si tajiri wa fedha, ila ni
tajiri wa marafiki na ushawishi ninao,” alitamba.
Katika
hatua nyingine, Lowassa alikataa kuulizwa maswali na wamachinga hao
akisema ameandaa kamati itakayoratibu harambee ya kuwachangia kwa lengo
la kupata sh bilioni moja.
“Kwa maandalizi ya
harambee nitakayorudi tena kuifanya, na ili mjue kwamba nipo makini
natoa hundi ya sh milioni 10 na milioni 10 nyingine nitaitoa leo hii,”
alisema Lowassa ambaye baadaye aliondoka kwa kutembea kwa miguu hadi
Mwanza Hotel.
Chanzo - Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment