Tuesday 28 January 2014

Hii ni hatari Hatufi ila cha moto tunakiona wananchi

Nilichokiona katika miji mbalimbali ya nchi hiyo, nilikinasibisha na ule msemo wa dhihaka wa baadhi ya vijana kuwa heri kuzaliwa mbwa Ulaya kuliko binadamu Afrika!


Kwa mara nyingine Watanzania wanaotumia umeme japo ni wachache lakini wameumizwa. Baadhi yao sasa wanafikiri warudie jadi yao ya kutumia kuni na vibatari.

Wakati hali ya maisha ikiwa ngumu, huku wengi tukiwa na vipato vya kuungaunga, Serikali imeridhia kupanda kwa bei ya umeme. Kila uchao maisha bora tuliyoahidiwa yanazidi kuwa kinyume chake, tena kwa kasi na ari zaidi.
Uzuri ni kuwa Watanzania wamelelewa na Serikali yao kuwa watu watulivu, wasiohoji na hata wapatwapo na majanga na shida , wataishia kuugulia tu ndani ya nyoyo zao.
Hii ndiyo ada ya Watanzania kwa miaka nenda rudi. Haishangazi kwa sababu hiyo tukawa Taifa la amani na utulivu siyo tu Afrika bali duniani kote. Kwingine kilichofanywa na Tanesco kingeshazua taharuki na majanga makubwa.
Inawezekana kwa hulka hii ya upole, utulivu, kutohoji mambo na kuvumilia shida, baadhi ya watu wanatumia mwanya huo kuwanyanyasa Watanzania.
Leo kwa mfano, siyo ajabu kuona maelfu ya wananchi wakifurushwa katika makazi yao ili kupisha mwekezaji mmoja wa kigeni. Wafanye nini wakati ardhi ni ya Serikali na ndiyo inayoamua wapi pafanywe nini?
Masaki, Oysterbay hawezi kupewa mwekezaji hata akitokea anayeweza kuyatamani, Lakini akitokea mwekezaji akaitaka Chanika yote au Kitunda yote, wahusika hawashindwi kuwaita wakazi wa maeneo hayo wavamizi. Watake wasitake wataondoshwa alimradi dhamira ya mwekezaji na wakubwa itimie.
Hii ndiyo Tanzania, nchi ya asali na maziwa lakini kwa walio wachache. Ni nchi iliyojaa taasisi nyingi zisizo na ubunifu wa kurahisisha maisha kwa wananchi kama lilivyo Shirika la Umeme (Tanesco).
Ubunifu pekee tena uliotukuka wa Tanesco ni kupandisha bei za umeme na kuwapigia magoti wadaiwa wake walipe madeni!
Julai mwaka jana nilikwenda Canada kwa ziara ya kikazi, nilibaini kwa macho yangu kwa nini Waafrika wengi wakiwamo Watanzania wanapenda kwenda kuishi ughaibuni.
Nilichokiona katika miji mbalimbali ya nchi hiyo, nilikinasibisha na ule msemo wa dhihaka wa baadhi ya vijana kuwa heri kuzaliwa mbwa Ulaya kuliko binadamu Afrika!
Canada haina tofauti na sisi kwa rasilimali, ni nchi kubwa iliyojaliwa aina nyingi za rasilimali kama ilivyo kwetu. Tofauti iliyopo ni kuwa wenzetu rasilimali hizo ni kwa ajili ya wote.


Licha ya wananchi wengi wa Canada kulia na kodi karibu katika kila bidhaa na huduma, mwishowe hucheka wanapoona kodi zao zikifanya kazi ya kuendeleza uchumi wa Taifa na ustawi wa wananchi wake.
Uwekezaji mzuri wa rasilimali zao unajidhihirisha katika maendeleo makubwa yaliyopo katika sekta zote ikiwamo elimu. Leo hii Canada ni moja ya nchi chache duniani zinazotumia sehemu kubwa ya pato la ndani katika kuendeleza sekta ya elimu.
Matokeo yake sekta ya elimu hasa ile ya juu, inawavutia maelfu ya wanafunzi kutoka nchi mbalimbali duniani. Hapa kwetu, licha ya ugumu wa maisha, viongozi wameshindwa kubuni njia za kupunguza makali ya maisha, kila siku sera na mipango ya maendeleo ni ile inayowaumiza wananchi badala ya kuwasaidia.
Ubunifu pekee ninaouona labda ni ule wa kujiongezea mishahara na posho, fedha zinazotokana na wananchi haohao wanaoteseka kimaisha.
Leo pamoja na Watanzania kuminywa kila kona, bado kodi zao zinashindwa kununua madawati shuleni au asprini hospitalini.
Hii ndiyo Tanzania na watu wake tusiokufa lakini cha moto tunakiona.

No comments:

Post a Comment