Wednesday, 21 August 2013

DIAMOND ATAJWA SAKATA LA UNGA AHUSISWHA NA MTANDAO WA MASOSANGE.

KWA mara ya kwanza tangu lilipoibuka sakata la watu maarufu kujihusisha ama na utumiaji au usafirishaji wa dawa za kulevya, jina la mwanamuziki anayeaminika kuwa na ukwasi mkubwa kwa sasa hapa nchini, Nasseeb Abdulmaliki, maarufu zaidi kwa jina la Diamond, limeanza kutajwa kuwa ni miongoni mwa vigogo wa ‘unga.’


Tayari mjadala mkubwa wa chini chini umeibuka kwa watu mbalimbali wakiwemo mashabiki wake, na taarifa ambazo zimelifikia MTANZANIA Jumatano kutoka vyanzo mbalimbali zimedai kuwa, mwenendo wa maisha ya Diamond sasa unachunguzwa na baadhi ya maofisa wa vyombo vya dola vya ulinzi na usalama.

Kutajwa kwa jina la Diamond katika sakata hili, kunatiwa nguvu zaidi na mwenendo binafsi wa maisha wa msanii huyo maarufu wa muziki wa kizazi kipya, unaokwenda sambamba na ukwasi mkubwa alioupata katika kipindi kifupi. 
Kama hiyo haitoshi, safari za nje ya nchi za mwanamuziki huyo unaohusisha ziara zake nchini Afrika Kusini na Uingereza, pia ni mambo ambayo yamechochea wingu la mashaka lililofikia hatua ya jina lake kuingizwa katika mtandao huo ambao katika siku za karibuni, umewagusa pia baadhi ya watu wenye majina makubwa katika jamii.

Kuhusu ziara hizo, kilicholeta mshtuko na dukuduku dhidi yake ni kuwapo kwa taarifa kwamba, katika moja ya ziara hizo za nje ya nchi, Diamond alifikia hatua ya kusafiri akitumia chumba kinachotumiwa na wageni mashuhuri (VIP), badala ya njia ya wasafiri wa kawaida.

Mbali na hilo, taarifa nyingine zinaeleza kwamba, mizigo ya msanii huyo ambaye mara kadhaa amekuwa akisafiri na kundi la wacheza shoo wake, imekuwa ikipita pasipo kupitishwa katika hatua za ukaguzi kwa namna ile ile ilivyokuwa kwa mabinti wawili wa Kitanzania walionaswa nchini Afrika Kusini baada ya kuruka mfumo wa ukaguzi wa JNIA.

Aidha, ukaribu wa kimahusiano kati ya Diamond na baadhi ya Watanzania wanaoishi nchini Afrika Kusini na ambao majina yao pia yameanza kuhusishwa na biashara hiyo ya mihadarati, ni jambo jingine ambalo limechochea harakati za kufuatiliwa kwa karibu kwa nyendo za Diamond.

Taarifa zaidi kutoka JNIA zinaeleza kwamba, miongoni mwa watu wanaoweza wakawa wamemponza Diamond ni wale ambao walionekana kuwa karibu na Agness Gerald ‘Masogange’ (25) na Melisa Edward (24), siku walipokuwa wakisafiri kwenda Afrika Kusini kabla hawajanaswa katika uwanja wa Ndege wa Oliver Thambo jijini Johannesburg nchini Afrika Kusini, wakiwa na shehena ya dawa za kulevya.

Mwenendo wa watu hao unatiliwa shaka kuwa huenda ni miongoni mwa wafanyabiashara wakubwa wa dawa za kulevya wenye maskani yao nchini Afrika Kusini, kwa sababu mbali na ukaribu na wasichana hao, pia walihusika kwa karibu kuusafirisha mwili wa mwanamuziki Albert Mangwair, aliyefia huko huko Afrika Kusini ambaye taarifa za kufa kwake ziligumbikwa na matumizi ya dawa za kulevya.

Alipoulizwa jana na MTANZANIA Jumatano kupitia simu yake ya kiganjani kuhusu taarifa hizo na iwapo amekwishahojiwa na vyombo vya dola baada ya jina lake kuanza kutajwa kuwa miongoni mwa orodha ya wasanii wa muziki wanaosafirisha dawa za kulevya, Diamond alikiri kuwa na pesa za kutosha kuishi maisha anayoyataka, lakini akakana kujihusisha na biashara hiyo.

Akifafanua tuhuma moja baada ya nyingine kwa mpangilio aliokuwa akiulizwa na gazeti hili, Diamond alisema katika maisha yake, hajawahi kujihusisha na utumiaji au usafirishaji dawa za kulevya, lakini madai hayo yamekuwa yakitolewa dhidi yake na watu ambao hawajui siri ya mafanikio yake.

“Kazi ngumu siku zote inalipa, sasa napata matunda ambayo yanatokana na kile nilichokifanya, iweje watu wanitilie mashaka, Watanzania ni mashahidi wangu wananiona navyochumia juani, nitaendelea kulia kivulini tu kwani nakula kwa jasho langu.

“Siyo kweli kwamba mizigo yangu haikukaguliwa na kama haikukaguliwa na ingekuwa na kasoro, basi Uingereza wangenitia hatiani, nilipita na nilikaguliwa.” Alisema Diamond.

Alipoulizwa kuhusu taarifa za kuwa mwanamtandao wa kundi la Masogange, pia alikanusha kwa kueleza kuwa hata siku aliyosafiri kwenda Afrika Kusini alikwenda peke yake uwanja wa ndege na kuongeza kuwa alikwenda huko kwa shughuli za kimuziki, ambapo safari nzima iligharimu zaidi ya Dola 30,000 za Kimarekani.

“Afrika Kusini nimekwenda kufanya kazi zangu na safari hiyo imenigharimu zaidi ya Dola 30,000, nilikwenda kurekodi nyimbo yangu mpya inayoitwa namba moja ambayo itaanza kusikika hivi karibuni.

“Unajua Watanzania sasa hivi wanajua mtu hawezi kufanikiwa au kupata maendeleo bila kuuza ‘unga’, hili si sawa juhudi za mtu ndizo zinamfikisha alipo, na mimi juhudi zangu ndio zinanifikisha hapa, watu waache kunijadili vibaya.” Alisema Diamond.

Kuibuka kwa taarifa hizi kumekuja ikiwa ni takribani miezi miwili sasa tangu Watanzania wawili, Agness Gerald ‘Masogange’ (25) na Melisa Edward (24), waliokuwa na uhusiano wa karibu na baadhi ya wanamuziki maarufu hapa nchini, kukamatwa nchini Afrika Kusini wakiwa na dawa za kulevya aina ya Crystal Methamphetamine zenye thamani ya Sh bilioni 6.8.

Mbali na kuwa na uhusiano wa karibu na wanamuziki, Edward anadaiwa kuwa alikuwa mfanyakazi katika mgahawa mmoja maarufu jijini Dar es Salaam, unaomilikiwa na mmoja wa vijana matajiri hapa nchini ambaye hata hivyo gazeti hili halijafanikiwa kumpata ili kufanya naye mahojiano.

Wakati huo huo, tayari hatua za kinidhamu zimekwishaanza kuchukuliwa dhidi ya wafanyakazi wa JNIA waliohusika kupitisha kilo 150 za dawa za kulevya, ambao Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, ametaja majina yao hivi karibuni na kuonyesha kwa waandishi wa habari ushahidi wa kuhusika kwao.

No comments:

Post a Comment