Thursday, 10 October 2013

MAANA HALISI YA MAPENZI INAPOTOSHWA

Kwa nguvu za Mungu wangu wa mbinguni mimi ni mzima wa afya njema na ninaendelea na majukumu yangu ya kila siku vyema. Kati ya majukumu yangu makubwa ambayo napaswa kuyatimiza kila siku ni pamoja na hili la kukumbushana juu ya kuwa bora katika uhusiano na wapenzi wetu.
Kwanza kabla sijaenda mbali sana katika mada hii ambayo naamini itawagusa wengi, ni vizuri kama tutajiuliza kwa pamoja maana ya mapenzi! Mapenzi humaanisha nini hasa? Mapenzi ni hisia ambazo zipo moyoni mwa mtu kwenda kwa mwingine, hisia hizi ili ziweze kuwa mapenzi ni lazima ziwe na ukweli na penzi la dhati huku moyo ukiwa na nafasi kubwa katika hilo. Hii ndiyo maana halisi ya mapenzi. Kwamba unapoingia katika uhusiano na mpenzio hupaswi kabisa kuwa na mtu mwingine kwakuwa utakuwa unaunyima haki moyo wako.
Pamoja na ukweli huo juu ya mapenzi lakini hivi sasa maana halisi ya mapenzi imepotoshwa, imebadilishwa na kuwa nyingine. Mapenzi ya siku hizi yamejaa ulaghai mtupu, hayana ukweli, kila siku ni maumivu juu ya maumivu. Kwanini watu wanaharibu maana halisi ya mapenzi?
Kuna matatizo mengi ambayo yanaweza kutokea ikiwa utakosa uaminifu kwa mpenzi wako, wakati mwingine matatizo hayo huweza kumlenga mwenzi wako moja kwa moja bila kukusumbua wewe lakini mwisho wa siku wewe utakuja kuwa na matatizo zaidi ya hayo unayoyafanya nyuma ya pazia hivi sasa.
Unaweza kujifanya mjanja sana kwa kuunganisha wapenzi zaidi ya kumi huko gizani ukiamini huonekani na hakuna matatizo yoyote ambayo unaweza kuyapata, kumbe unajidanganya maana kuna siku utakuja kuumbuka kwa kuonekana kwako huna uaminifu!
Hivi ni kwanini maana halisi ya mapenzi hivi sasa imepotoshwa? Ni nani muanzishi wa upotoshaji wa maana halisi ya mapenzi, utagunduaje kama mpenzi wako ni msaliti wa penzi lako. Haya na mengineyo utayapata katika mada hii, unachotakiwa kufanya ni kufuatana nami katika mfululizo wa makala haya utapata kitu kipya akilini mwako.
PENZI LA KITAPELI
Wengine huwa ni tabia yao ya asili, siyo mkweli kuanzia malezi ya wazazi wake hayasisitizi juu ya ukweli, ameshazoea kufanya mambo kiujanja ujanja! Kwa mpenzi wa aina hii ni vigumu sana kudumu naye. Ni mwepesi wa kutamka maneno ya mapenzi lakini ndani ya moyo wake kuna vitu viwili, kwanza anakutamani wewe na pesa zako na wakati huo huo anatamani kuwa na bwana mwingine kwa ajili ya kuongeza kitega uchumi, hili ni tatizo!
Mwanamke wa aina hii siyo ngumu kwake kukuita majina mazuri ya kimapenzi lakini akiwa hamaanishi kutoka moyoni mwake kwamba anakupenda. Hawa wapo wengi lakini ni vigumu sana kuwagundua mapema. Hawa huharibu kabisa maana halisi ya mapenzi.
Ngoja nikuulize wewe unayemsaliti mpenzi wako, unavyomfanyia mwenzako hivyo unadhani yeye hana moyo? Hivi hujui kuwa mwenzako anakupenda kwa mapenzi yake yote na amekuchagua wewe uwe mwandani wake? Siku akijiua kwa sababu yako utakuwa katika hali gani? Hebu acha utapeli wako wa mapenzi haraka sana!
Kuwa muwazi na kama unadhani haupo tayari kuwa na mpenzi basi mwache huru atafute mwingine mwenye msimamo uendelee na mambo yako na kama ni kujiuza ujiuze vizuri lakini ukijua kuwa siku moja utakuja kuingia mahali pabaya. Achana na tamaa za muda mfupi ambazo mwisho wake ni mbaya. Huyo mwanaume anayekudanganya leo, ujue kabisa kesho hayupo na wewe na atakuwa amekuachia virusi vyako vya kutosha! Kama umeamua kujitoa sadaka ni bora ukafa peke yako kuliko kumwangamiza na mwenzako ambaye hana hatia zaidi ya penzi lake la dhati kwako.
USHAWISHI...
Hili ni tatizo lingine linalochochea kuharibu maana ya mapenzi, ushawishi ni sumu nyingine katika hili. Hapa nitazungumizia pande mbili, ya kwanza ni ya mshawishi na mshawishiwa! Naweza kusema wote wana makosa maana anayeshawishi hutumia kila njia kumpata anayemhitaji lakini wakati huo huo anayeshawishiwa kukubali wakati akijua ana mpenzi ni kosa kubwa sana. Wanaume wengi watu wazima tena wenye familia zao hivi sasa ndiyo wanaoongoza kutafuta dogodogo wakidai kuwa damu zao zinachemka! Hutumia fedha, magari na kila aina ya vishawishi ili waweze kuwanasa wasichana hao wadogo wakitafuta penzi. Sijui kama wanaume wa aina hii wanatafuta nini kwa hao mabinti? Hivi kama ukigundua mkeo anakusaliti utajisikije?
Wewe unayewarubuni wasichana ambao wapo masomoni na kuwashawishi kwa fedha zako je, kama ni mwanao ndiyo angekuwa anafanyiwa hivyo ungejikiaje? Kwanini unakuwa na moyo wa chuma kiasi hicho? Ni ulimbukeni wa ajabu sana kumuacha mkeo nyumbani halafu uanze kuhangaika na vimada, wa kazi gani kwanza? Labda unatafuta penzi shatashata, sasa si bora umfundishe mkeo akufanyie hayo unayoyapenda? Kwani umemwambia unachotaka akashindwa kukupa?
Unapaswa kubadilika ndugu yangu maana dunia ya sasa siyo ya kuchezea! Kutoka nje ya ndoa siyo suluhisho, sana sana utakuwa unayafuata matatizo mwenyewe na mwisho wa siku utauchukua Ukimwi na kumpelekea mkeo ambaye ni mtulivu!
Upande wa pili ni wa wasichana ambao hushawishiwa na watu wazima, asilimia kubwa ya wasichana wa aina hii huwa na wapenzi wao, lakini kwa tamaa ya pesa hujikuta wakijitumbikiza katika uhusiano na wanaume hao. Kwanza hivi wewe binti hujipendi? Kwanini unaiacha akili yako bila kufanya kazi kiasi hicho? Hebu jiulize, mpaka amekufuata wewe ameshatembea na mabinti wangapi kama wewe? Kitu gani kilichomvutia kwako na wewe umevutiwa na nini wakati una mpenzi wako anayekupenda kwa dhati?
Hebu chekecha kichwa chako vizuri, mpenzi wako ameshakuvisha pete ya uchumba lakini unamsaliti ukijua wazi kuwa unafanya makosa kwanini unafanya hivyo? Tamaa ya fedha ndogo ndogo itakufikisha wapi kama siyo kaburini? Acha kuudhulumu moyo wa mpenzi wako, magonjwa siku hizi ni mengi, unatakiwa kutulia na kuachana na tabia zisizofaa ili mwisho wa siku uweze kuwa bora kwa mwandani wako.
Usanii umezidi katika mapenzi, hakuna ukweli tena kiasi watu wanaogopa kuingia katika uhusiano kutokana na woga wa kutapeliwa. Wengine huwa na msururu wa wapenzi wakiamini ni fasheni, nani kakudanganya ndugu yangu? Hakuna fasheni ya kuunganisha wapenzi ndugu zangu, sana sana utakuwa unatafuta matatizo na siku moja utakuwa unalia lakini wakati huo utakuwa umeshachelewa!
Uwongo wako siku moja utakuja kuwa na mwisho, hakuna mwongopaji aliyedumu bila kugundulika, hakuna msaliti aliyeendelea kufanya uchafu wake siku zote bila kugundulika na hata kama hutagundulika, ukimwi utakuja kukuumbua.
Hivi unafikiri dunia ni yako!? Achana na hiyo tabia yako mbaya mara moja. Najua kuna wengine watakuwa wanasema huyu Shaluwa vipi, mbona leo amekuwa mkali sana, inanibidi niwe mkali maana naona hali ilivyo mbaya.
Siwezi kuzungumzia juu ya kumfurahisha mpenzi wako kila siku umefika wakati sasa wa kuelezana ukweli! Nani asiyejua kuwa kuna ukimwi, hata wewe unayesoma unajua wazi kuwa kuna ukimwi lakini kwanini hutulii? Utakimbizana na wanawake mpaka lini? Unadhani utawamaliza? Tulia ndugu yangu, maisha ya leo siyo ya jana, kumbuka kuwa siku zinazidi kusonga mbele na haziwezi kurejea tena.
KATAA PENZI LA KILAGHAI...
Inawezekana upo katika uhusiano na tapeli wa mapenzi bila kujua, hiyo ni sumu na unachotakiwa kufanya sasa ni kuanza kumchunguza mpenzi wako mapema isije kuwa upo kwenye foleni! Hakuna kitu kibaya kama kuwa katika foleni ya wapenzi kwa mpenzi mmoja, tena mbaya zaidi awe ni yule ambaye moyo wako umempenda kwa dhati.
Kumbuka, kuwa katika uhusiano na mtu ambaye haeleweki ni sawa na kukaribisha matatizo katika maisha yako, huna sababu ya kuishi kwa wasiwasi ukiwa hujui mpenzi wako anakuchukulia vipi. Anza kumuwekea mitego mapema.
Lakini katika mitego yako achana na simu yake kabisa, huna sababu ya kuchunguza simu yake lakini kama ni msaliti utajua tu, unafikiri atajificha mpaka lini, atafanya mambo yake gizani mpaka lini? Kuna siku utagundua na kumuacha aendelee na umalaya wake kama ameona ndiyo maisha. Usikubali kabisa kuwa katika penzi la kitumwa, penzi la kisaliti, kuwa na mtu ambaye anakuchanganya wa kazi gani zaidi ya kukupotea muda na kukukaribishia machozi? Mchunguze sana na mwisho wa siku utakuja kugundua uongo wake ulipo. Usikubali kabisa kuwa na mpenzi mlaghai.
UTAMJUAJE MLAGHAI?
Hapa ndipo kwenye kazi, kwa bahati mbaya sana kama ikitokea ukampenda mtu sana hata kama akifanya mabaya kiasi gani unaweza usiyaone, kama wewe ni wa aina hii unapaswa kubadilika kifikra. Mwone wa kawaida, fanya uchunguzi wako polepole na kama ukiona moja kati ya mambo yafuatayo, ujue kuna kitu.
*Hataki kukutanisha na rafiki zake.....
Hii ni kati ya alama walizonazo tapeli wa mapenzi, ni mtu wa kufanya mambo kwa upekee sana. Kila dakika hakaukiwi na neno nakupenda sana, lakini moyoni mwake hakuna alama hata moja ya mapenzi kwako.
Ni vigumu kumtambua mtu wa aina hii lakini chunguza kuhusu hili, hapendi kabisa kukutanisha na rafiki zake na hata mkikutana nao kwa bahati mbaya basi hatakutambulisha na kama akikutambulisha hatakutambulisha kama mpenzi wake rasmi. Ataanza: “Ebwanae huyu ni rafiki yangu...tunaheshimiana sana...” ndivyo atakavyosema.
Tangu lini mpenzi akatambulishwa kama rafiki? Mtu anapomtambulisha mpenzi wake humtambulisha kwa kujisikia furaha moyoni kwamba anamtambulisha mpenzi wake lakini inakuwaje kwako akutambuilishe kama rafiki? Baadaye utakapomuuliza hawezi kuwa na jibu la maana, atabaki kukuambia hata kama akikutambulisha kama rafiki jamaa ataelewa kuwa ni mpenzi wake, hii inaingia akilini kweli?
Hakuna ukweli kama huo ndugu zangu! Huo ni ulaghai na anaogopa kukutambulisha kama mpenzi maana tayari ameshaonwa akiwa na wanawake wengine. Sasa kama ndivyo atatambulisha wangapi? Aseme wewe ni nani? Amka dada yangu!
*Hufanya mambo kwa kificho
Hii ni alama nyingine waliyonayo wanaume wa aina ninayoielezea katika mada hii. Siku zote mambo yake ni kwa siri kubwa, kama mna ahadi ya kukutana, hataki muongozane, atakuambia mkutane moja kwa moja sehemu husika. Hata muda wa kuondoka atafanya kila njia ili kila mmoja aondoke mwenyewe na kama mkiondoka pamoja basi ujue ni usiku na hakuna atakayewaona. Ikitokea akakubali kuongozana na wewe, hatapenda muongozane pamoja. Atalazimisha utangulie mbele yeye afuate nyuma, kwanini? Kwasababu anaogopa kujulikana kuwa yeye ni mpenzi wako na kama anaogopa anakupenda kweli? Mapenzi gani hayo yanafanywa kwa siri? Anakupotezea muda huyo.
*Hataki ndugu zenu wafahamiane
Mpenzi wa aina hii ni mjanja sana, kwanza kabisa atajifanya mtu mwenye ‘ubize’ sana, yote hii ni kukwepa kuwajua ndugu zako au wewe kuwajua ndugu zake! Wakati mwingine anakuwa hapendi ndugu zako na wake wakutane wakijua wazi kuwa nyie mna uhusiano, hili ni tatizo.
Hakuna uhusiano wenye heri na malengo ya kuishi pamoja siku zijazo ukawa wa kificho cha kiasi hicho. Kama ana nia na wewe basi atahakikisha anawafahamu baadhi ya ndugu zako na wewe unawafahamu baadhi ya ndugu zake, hayo ndiyo mapenzi ya kweli. Mapenzi hayaishii kwa nyie wawili pekee bali hata kwa ndugu zenu. Mnapojuana inakuwa rahisi kusaidiana hata katika mambo mengine ya kawaida.
Wewe mwanamke una thamani kubwa sana, usiidharau jinsia yako, usijishushe kiasi hicho, huyo anayekupotezea muda na kukuchezea sasa hivi hana thamani kama huyo aliyeandaliwa kwa ajili yako. Ngoja niwaambie kitu kimoja dada zangu, Mungu mwenyewe ndiye anayejua mwanaume wa kukuoa hivyo huna sababu ya kuendelea kuwa katika uhusiano wa manyanyaso na mateso kiasi hicho kwa sababu ya kubembelezea ndoa. Ndoa haibembelezewi, huletwa na Mungu mwenyewe!
Anakupiga chenga...
Hili ni tatizo lingine kwa mpenzi mtapeli, anakuwa mtu wa mambo mengi, kumpata kwake siyo rahisi. Anajifanya mtu wa kazi nyingi ambazo mwanzoni wakati mkikutana hakuwa nazo! Kipindi hiki anakuwa na visingizio vingi visivyokuwa na maana lakini lililokuwa akilini mwake ni kukwepa kuonana na wewe.
Tamaa ya mwili wake imeshaisha kwa maana hiyo haoni kama kuna umuhimu wa kukutana na wewe tena. Ukimwomba mkutane naye, hutoa sababu nyingi ili mshindwe kuonana.
Hata hivyo, ikiwa utakwenda kwake bila kumfaarifu kabla ‘surprise’ inawezekana ukamkuta yupo na mwanamke mwingine au akawa hana kazi kama alivyokudanganya awali. Mbaya zaidi ni kwamba huweza kukubadilikia na wakati mwingine kukupiga kwa kosa la kwenda kwake bila taarifa. Je, mpenzi wa aina hii anakupenda kweli? Jibu hapa ni hapana.
Anapunguza kasi ya mawasiliano...
Hii ni hatua nyingine ya mpenzi aliyekuchoka, haoni umuhimu wa kuwasiliana na wewe kama zamani na kama akifanya hivyo, ujue ana shida yake muhimu. Inawezekana alishakuzoesha kukupigia simu kila wakati au kukutumia sms za kukujulia hali, lakini kwa wakati huu hawezi kufanya hivyo tena.
Ukiona alama hii ujue mwisho wa penzi lenu unakaribia. Mwanaume wa aina hii anaweza kukupigia simu anapohitaji uende kwake kwa ajili ya kumfulia nguo zake, kumfanyia usafi nyumba/chumba chake, kumpikia na mambo mengine ambayo yatakuwa na manufaa kwake.
Haishangazi sana kuacha kukupigia simu kwa wiki nzima, lakini siku atakayokupigia ukakutana na maneno haya; “Nina hamu sana na wewe mpenzi wangu, njoo basi leo ulale nyumbani kwangu, naamini hutaniangusha!” Hapa anahitaji penzi lako ndiyo maana anakuambia kwa sauti laini kama hii. Dada yangu zinduka usingizini haraka, kwani wewe chombo cha starehe au kiwanda cha kuzalishia watoto?
Majibu yake huwa ya mkato...
Wakati huu huwa hapimi ajibu nini na lipi aache! Thamani yako kama mpenzi imeshaisha na sasa anakuona kama dada yake tu! Sana sana atakujibu vizuri pale anapokuhitaji (kingono) au anataka msaada kutoka kwako.
Wewe kama mpenzi wake una haki ya kumwuliza sababu za kuzima simu kwa saa tatu bila kukukutaarifu, na inawezekana huo ndio utaratibu wenu wa siku zote lakini kwa sasa unaweza ukakutana na jibu kama hili; “Lakini kwanini unanifuatilia sana maisha yangu wewe mwanamke? Naomba uniache, sipendi maswali ya jela!” Hivi kweli unaweza kumjibu mpenzi wako majibu ya hovyo kiasi hiki? Huyu ni tapeli anayekupotezea muda wako.
Hafurahii uwepo wako....
Hana furaha kabisa anapokutana na wewe, wakati mwingine anaweza kujisahau na kuonyesha wazi kuwa hafurahii kabisa uwepo wako nyumbani kwake. Anaweza kukuuliza muda utakaokaa ili ajue mapema. Wakati mwingine anaweza kuondoka au kukuambia ana mtoko muda mfupi baada ya wewe kufika kwake. Jiulize, anakwenda wapi penye umuhimu zaidi kuliko wewe? Jambo hili linahitaji akili ndogo sana kujua kwamba jamaa hana ‘time’ na wewe tena. Sasa unasubiri nini? Kuumizwa zaidi au kuteswa na mapenzi?
Siyo mtu wa kujali...
Hakusikilizi sana kama zamani, ni mtu wa kupuuza kila unachomwambia, lakini kama wewe ni mjanja sana wa mambo, anaweza kukusikiliza mara chache lakini kwa mambo yanayomhusu yeye. Kwa kifupi thamani na utu wako vinashuka na unakuwa mtu wa kawaida kwake kama walivyo rafiki zake wengine.
Ukiona alama hii, anza kuona taa nyekundu mbele yako, maana jamaa anakutafutia sababu ya kuachana na wewe. Usisubiri hiyo sababu, ondoka mapema na umuache na umapepe wake aone faida yake!
MAANA HALISI YA MAPENZI!
Ingiza hili ubongoni mwako; kila kitu kinafanyika kwa mipango! Hata Mungu mwenyewe wakati wa uumbaji alipanga kuumba kila unachokiona, yeye ndiye anayejua mwanzo na mwisho wa kila kitu. Kama ndivyo, una haja gani ya kuwa na wasiwasi?
Una sababu gani ya kuhisi lazima uolewe na huyo anayekutesa na kuunyong’onyesha moyo wako? Hakika huna haja ya kuumia kiasi hicho! Mungu amekuumba kwa makusudi, amekujalia ukakakua, ukasoma hadi ukafikia hapo ulipo hivi sasa. Hapana shaka kwamba anajua mume wako atakuwa nani, atakuja lini na mtaishi vipi? Anajua pia mwisho wa maisha yako utakuwa lini!
Kwa misingi hiyo, una sababu gani ya kuendelea kuutesa moyo wako wakati aliyekuumba yupo? Unafikiri haoni jinsi unavyoteseka, unavyolia na kuumia kwa sababu ya huyo anayekupotezea muda? Anajua...nenda kwake, msihi akuonyeshe aliyemwandaa kwa ajili yako na siku moja utaishi maisha ya furaha na amani. Nashukuru kwa kunisoma, Mungu akubariki sana

No comments:

Post a Comment