Saturday, 14 December 2013

MWALIMU AFA KIMIUJIZA JIJINI DAR

Mwalimu Gloria Tarimo ‘Ticha Gloria’ (29) aliyekuwa akifundisha katika Shule ya Mbezi High School ya jijini Dar, amefariki dunia katika mazingira ya kutatanisha huku baadhi ya ndugu, jamaa na marafiki wakidai kifo chake ni cha kimiujiza.
Ticha Gloria ambaye alikuwa akikaimu nafasi ya mwalimu mkuu wa shule hiyo, alifariki dunia Desemba 6, mwaka huu katika Hospitali ya Muhimbili jijini Dar huku wengi wakihisi kuna mkono wa mtu nyuma ya kifo hicho.
                                                      Marehemu Glory A Tarimo enzi za uhai wake. 
USHIRIKINA WAHUSISHWA
Akizungumza na gazeti hili, mmoja wa ndugu wa marehemu aliyeomba hifadhi ya jina lake kwa kuwa si msemaji wa familia alisema, kifo cha Ticha Gloria kinahusishwa na ushirikina kwa kuwa kabla ya mauti kumfika alikumbana na mambo mengi ya ajabu.
“Ni kifo cha ajabu kwa kweli na kimemshangaza kila mmoja wetu. Nakumbuka ilikuwa Juni, mwaka huu ambapo alienda kazini na alipofika kwenye mlango wa ofisi yake alikuta nazi imevunjwa.
“Licha ya kushangazwa na uwepo wa nazi hiyo, aliiruka kisha akaingia ofisini kwake. Kuanzia hapo alianza kuumwa mguu, kuna wakati akawa anahisi unawaka moto. Tulimpeleka Hospitali ya Muhimbili, akapatiwa matibabu na akapata nafuu,” alisema ndugu huyo. 
AKUTA NJIWA KWENYE KITI OFISINI
Ndugu huyo alizidi kueleza kwa masikitiko kuwa, baada ya tukio hilo la kukuta nazi imevunjwa kwenye mlango wa ofisi yake, mambo hayakuishia hapo kwani hivi karibuni alipoingia ofisini kwake alikuta Njiwa kwenye kiti chake.
“Alipiga kelele sana, walimu na wanafunzi wake wakaja  kushuhudia huku kila mmoja akishangaa na kuogopa kumtoa njiwa yule kwenye kiti.
“Mwalimu mmoja aliyefahamikwa kwa jina la Fadhili ndiye aliyemuondoa njiwa yule. Bila kujua kuwa roho yake inasakwa, Gloria akakaa kwenye kile kiti na kuendelea na shughuli zake,” alisema ndugu huyo na kuongeza:
“Haikuchukua muda mrefu akahisi kama anachomwa na kitu chenye ncha kali kwenye makalio yake huku kichwa kikimuuma sana. Walimu wenzake walimchukua na kumrudisha hospitalini.”
 
AANZA KUZIONA SIKU ZAKE MFULULIZO
 Ilielezwa kuwa, baada ya mwalimu Gloria kufikishwa hospitalini, hali ilizidi kuwa mbaya na akaanza kutokwa na damu ya hedhi mabongemabonge huku damu nyingine ikitokea puani.
 

Ndugu wa Marehemu.
“Hali ilikuwa hivyo, akawa anateseka sana huku wakati mwingine akilalamikia baadhi ya walimu wenzake kuwa ndiyo wanaotaka kumtoa roho.
“Kuna siku alimuita daktari aliyekuwa akimhudumia na kumwambia anamshukuru kwa kujitahidi kuokoa uhai wake lakini anaamini hatapona kwani anajua kuna walimu wamedhamiria kumuua ili wakalie kiti cha ualimu mkuu, baada ya hapo alikata roho,” alisema ndugu huyo ambaye ndiye aliyekuwa akiwasiliana na marehemu mara kwa mara.
 
WALIMU WANASEMAJE?
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti, baadhi ya walimu wa shule hiyo walisema wamesikitishwa sana na kifo cha Ticha Gloria, wakasema licha ya kwamba kila kifo kinapangwa na Mungu lakini hiki cha mwenzao kimeacha utata.
“Kwa kweli kifo cha Gloria kimenifanya niamini kuwa Mungu yupo lakini pia ushirikina upo. Amekufa kifo cha kimiujiza sana, mambo yaliyomtokea kabla ya kufariki dunia yanaashiria kabisa kuna mkono wa mtu,” alisema mwalimu mmoja wa kike aliyeomba hifadhi ya jina lake.
 MSIKIE MWENYE SHULE
Mkurugenzi wa shule hiyo aliyefahamika kwa jina la Said Mgude alielezea masikitiko yake juu ya kifo cha mwalimu Gloria kwa kuwa alikuwa mchapakazi sana ila akataka watu wasihusishe kifo hicho na mambo ya kishirikina.

“Kila mmoja lazima aumie kwa kifo cha Gloria, lakini nawasihi watu wamuamini Mungu na waachane na dhana za kishirikina. Shule yangu ni taasisi kubwa sana, minazi ipo mingi hivyo kama alikuta nazi imevujwa mlangoni inawezekana ilianguka tu na kupasuka.
“Kuhusu Njiwa hapa Dar es Salaam siyo jambo la ajabu kwa sababu wapo wengi sana, mimi siwezi kukubaliana na mambo hayo ya kishirikina na hakuna kitu kama hicho,” alisema.

Mwili  wa mwalimu Gloria uliagwa Desemba 10, mwaka huu katika Kanisa Katoliki Mbezi Mwisho jijini Dar na baadaye ulisafirishwa kwenda  Moshi Rombo mkoani Kilimanjaro na kuzikwa siku iliyofuata ya Desemba 11.
Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi-Amin

2 comments: