Sunday 26 January 2014

Amng’ata meno mtoto baada ya kumfanyia ukatili mkewe


Picha ikimwonyesha mtoto Zakaria (1) na jeraha lake lililotokana na kung’atwa na baba yake.  

Inawezekana hakuamini hivyo kwa kuwa mume wake Matata Makali (siyo jina halisi), ambaye alionekana mwenye upendo na kujali, pengine ni kwa sababu ya mapenzi mapya ya binti mdogo.


Wakati alipoolewa kuwa mke wa pili kwa mahari ya ng’ombe wanane, Katarina Mturi (22) alisindikizwa kwa ngoma na tamaduni za Kabila la Kikurya, wala hakuamini kama kuna siku ataichukia ndoa hiyo.

Inawezekana hakuamini hivyo kwa kuwa mume wake Matata Makali (siyo jina halisi), ambaye alionekana mwenye upendo na kujali, pengine ni kwa sababu ya mapenzi mapya ya binti mdogo.
Katarina alikuwa ameolewa mara ya pili akitoka kwa mume wake wa kwanza aliyedai hakuwa na hata chembe ya upendo ndipo kwa kushauriana, familia yake ilimrudishia mahari mwanaume huyo na ndoa kuvunjika.
Mwanamke huyo anasema kuwa alikaa nyumbani kwao kwa muda, ndipo akajitokeza Matata(45), akiamini kuwa sasa amepata mume mwema.
Hata hivyo, hali ilikuwa kinyume, kwani leo Katarina ambaye ni mkazi wa Kitongoji cha Chinato, kijijini Bisarara, Kata ya Sedeco katika Wilaya ya Serengeti iliyopo Mkoa wa Mara, amekuwa miongoni mwa wanawake wanaosimulia ukatili wa kijinsia katika ndoa. Kutokana na yaliyomkuta, anaona kuwa ndoa siyo tena hitaji lake muhimu maishani.
Kwa nini?
Pamoja na mateso, kipigo alichokuwa akipata, alijitahidi kuvumilia familia yake ikimtia moyo na kumweleza kuwa ndoa ndivyo zilivyo.
Lakini Katarina anasema hatosahau tukio la saa 2:30 usiku, Januari 8 mwaka huu, ambapo mumewe huyo mpya alimfanyia ukatili bila kuwa na chembe ya huruma.
Katarina anaeleza kwamba hofu yake sasa ni ukatili kumwachia ulemavu.
“Katika hali ambayo mpaka leo sijaielewa, nilikuwa ndani na wanangu wawili, mkubwa na huyu mdogo mume wangu aliingia ndani akaniamuru niswage ng’ombe usiku huo kwenda ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kwa malisho. Nilikakataa, kwa sababu ilikuwa ni usiku. Nilimweleza kuwa kisheria haikubaliki kuchungia mifugo ndani ya Hifadhi ya Taifa, tena  kuna wanyama wakali na mimi ni mwanamke nitafanyaje?,” anasimulia.
Katarina anaongeza akionyesha maeneo aliyoumizwa: “Maneno hayo yakamkasirisha na kilichotokea ndiyo kama unavyoona.”

Anasema kuwa mume wake alichukua fimbo na kuanza kumpiga mithili ya mbwa mwizi, bila kuchagua sehemu ya kupiga na kumuumiza maeneo mbalimbali ya mwili ikiwamo mguu, ambao sasa uko hatarini kuoza.
“Akanipiga mpaka mwenyewe akachoka; sikuwa na uwezo wa kukimbia kwani damu zilinitoka mno na mtoto alikuwa akilia baada ya kuona ninavyopigwa. Lakini mwanaume huyo hakuwa hata na chembe ya huruma. Nikitafakari  kosa langu sijui, nadhani alikuwa amepanga kwa muda mrefu kutekeleza lengo hilo,”anaeleza.
Baba amalizia hasira kwa mtoto
Katarina anasimulia kuwa baada ya kipigo hicho alichopata yeye, Matata alimrukia mtoto wake na kumng’ata meno mgongoni, akidai alimpandisha hasira baada ya kulia alipomwona mama yake (yeye Katarina) anapigwa.
“Bila chembe ya huruma aliamua kumrukia mtoto wa mwaka mmoja na kumng’ata mgongoni mpaka akamtoa nyama.  Licha ya mtoto kulia kutokana na maumivu makali aliyopata, Matata hakujali, hata mimi kudhani kuwa mwisho wetu na mwanangu ndiyo umefika,”anasimulia Katarina.
Agoma kuwapeleka hospitali
Licha ya majeraha waliyopata usiku huo wa Januari 8, siku iliyofuata ya Januari 9 Matata aliamka na kuendelea na shughuli zake, bila kujali, wala kuwa na dalili za kuwapeleka hospitali mkewe na mwanawe ingawa aliona kuwa mkewe hakuweza kutembea kutokana na jeraha na maumivu aliyokuwa nayo.
Mama abeba jukumu
Meremo Mturi (43), mama mzazi wa Katarina anasema kuwa akiwa nyumbani kwake katika shughuli zake za kawaida, ghafla alimwona binti yake (Katarina) na mjukuu wake wakisindikwa hadi nyumbani kwake hapo.
“Nilipowaona nilistuka nikajua kuna jambo lisilo la kawaida wametendewa, ndipo Katarina akanisimulia nami nikashuhudia hali halisi, niliogopa sana,”anasema.

No comments:

Post a Comment