Wednesday 5 February 2014

Polisi yamsaka Lema kwa vurugu


“Nimepiga marufuku maandamano kwa vyama vyote, tunataka mji wa  Arusha uwe na utulivu,”

Jeshi la Polisi mkoani Arusha linamtafuta  Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema na watu wengine watatu ili kuhojiwa kuhusu malalamiko ya vurugu zilizotokea kwenye mikutano ya kampeni za uchaguzi wa kiti cha udiwani Kata ya Sombetini wiki iliyopita ambapo watu kadhaa walijeruhiwa.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alisema jana ofisini kwake kuwa maandamano yaliyopangwa kufanywa na Chadema leo yamepigwa marufuku kwa maelezo kuwa madai yao bado yanashughulikiwa.
Kamanda Sabas aliwataja baadhi ya wanachama kuwa wanatafutwa kwa ajili ya mahojiano kuwa ni Anold Kamde na wengine akiwataja kwa jina moja moja ambao ni Frank na Daudi.
“Nimepiga marufuku maandamano kwa vyama vyote, tunataka mji wa  Arusha uwe na utulivu ili wanaofanya kampeni waendelee na wanaofanya kazi wasibughudhiwe. Ninamtaka Lema afike kwa Kamanda wa Upelelezi wilaya ahojiwe,” alisema Sabas
Kwa upande wake, Godbless Lema alisema  kuwa hana taarifa ya kutafutwa polisi kwa ajili ya mahojiano na kama anahitajika basi utaratibu ufatwe wa ili aweze kuhojiwa.
“Ninachofahamu ni wanachama wetu watatu ambao Ofisi ya Kamanda wa Upelelezi wa Wilaya ya Arusha ilinitaka niwape taarifa zao kuwa walikuwa wanahitajika kwa mahojiano,” alisema Lema
Chadema wilaya  ya  Arusha ilipanga kufanya maandamano wakitaka polisi iwakamate watu wanaodaiwa kuwa wafuasi wa CCM wanaofanyia vurugu na kuwaumiza wanachama wao kwenye mikutano yao ya kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani Kata ya Sombetini.
Hata hivyo, Lema alisema baada ya mashauriano na Polisi, wamesogeza mbele hadi kesho Alhamisi kwa kuwa baada ya kuwasilisha barua yao ilibainika kuwa CCM nao waliomba kufanya maandano yao leo Jumatano. Kamanda Sabas  alisema wanachama kadhaa wa CCM wanaolalamikiwa na Chadema kuhusu vurugu hizo wameshahojiwa  na wanahitaji kuwahoji wanachama watatu wa Chadema pamoja na Lema kutokana na malalamiko ya wafuasi wa CCM ambao  wanadai kufanyiwa fujo na wafuasi wa Chadema.

No comments:

Post a Comment