Saturday, 10 May 2014

MTOTO MCHANGA ANAHITAJI USAFI WA HALI YA JUU..............

ken4
Mtoto mchanga anahitaji usafi wa hali ya juu, kuanzia mwili wake, nguo, mazingira anayokaa hadi yule anaye mhudumia. Sababu ya uchanga wake ni rahisi sana kupata magonjwa mbalimbali kama atakuwa kwenye mazingira yasiyo na usafi wa kutosha.


 Hakikisha mwili wake ni msafi kwa kumuogesha angalau mara mbili kwa siku hasa katika sehemu zenye joto, na nguo zake  zifuliwe kila siku kwa maji safi na sabuni. Unapofua nguo za mtoto  hakikisha hazichanganywi na nguo za watu wazima na ni vyema nepi zikawa zinafuliwa muda mfupi baada ya kuchafuka. Haipendezi kuweka nepi chafu kwenye ndoo kwa masaa mengi, kwanza zitaleta harufu mbaya, zitakuwa ngumu kutakata na zitaharibika mapema.

Unapomuogesha mtoto ni vyema ukitumia maji ya uvuguvugu na kamwe usimuache mtoto kwenye beseni la maji bila kumshikilia. Kuna watoto wengine huwa hawapendi maji na wanalia sana muda wa kuoga, unaweza kuwa unamuimbia na kumchekea wakati unamuogesha ili aweze kuwa mtulivu na kuona kuwa kuoga ni jambo la kufurahisha. Kumbuka kumbadilisha mtoto nepi mara tu anapojisaidia ili kumuweka katika hali nzuri na kumuepisha na michupuko. Kama unaumia nepi za kutupa (disposable diapers) hakikisha mtoto hakai nayo muda mrefu sana inaweza mletea madhara.

Kitanda cha mtoto kinatakiwa kiwe safi wakati wote na pia chumba anacholala kisiwe na hewa nzito wala vumbi. Watu wote wanaomhudumia mtoto lazima wawe katika hali ya usafi na pia ni vyema kama kucha zikiwa fupi hii itasaidia mikono kuwa safi zaidi.  Kama unaweza ni vizuri pia nguo za mtoto zikawa zinanyooshwa baada ya kufuliwa na kukauka ili kuua vijidudu na inashauriwa kuepuka kuanika chini nguo za mtoto maana majani mengine yanaweza mdhuru mtoto au wadudu wakatembelea juu ya nguo na baadaye mtoto akadhurika. Usafi utapunguza magonjwa mengi kwa mtoto wako na kumfanya awe na afya na furaha.
Mungu akubariki sana.

No comments:

Post a Comment