Sunday, 26 January 2014

Chadema wapokewa kwa mbwembwe za kipekee Mbeya


Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk Wilbroad Slaa.

Chopa yazunguka anga la mji huo kabla ya kutua, vituko ,shangwe vyatawala.


Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk Wilbroad Slaa na Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (Sugu) jana walipokewa kwa mbwembwe na umati wa wafuasi wa chama hicho waliovalia sare za chama hicho huku wakiwa na mabango.

Viongozi hao wakiwa katika chopa walitua katika uwanja wa mikutano wa Ruanda Nzovwe saa 10.30 jioni wakitokea Sumbawanga na Chunya ikiwa ni ziara ya mikoa ya Nyanda za Juu Kusini katika Operesheni (M4C) Pamoja Daima.
Umati wa wafuasi wa chama hicho ulipagawa baada ya kutua kwa Chopa hiyo ambapo baada ya Dk Slaa na Sugu kuteremka, waliwazonga huku kila mmoja akitaka kuwa karibu na viongozi hao.
Kabla Chopa hiyo haijatua ikitokea Chunya, rubani aliizungusha katika sehemu kubwa ya jiji la Mbeya na wananchi wengi walionekana wakishangilia huku wakipeperusha bendera za chama hicho na kukimbilia katika viwanja hivyo.
Dk Slaa
Akizungumza na wafuasi wa chama hicho, Dk Slaa alisema Chadema siyo chama cha watu wa mjini pekee yake bali hadi vijijini na kwamba ndiyo maana viongozi wamekuwa wakiwatembelea huko.
“Operesheni hii ni ya chopa zinazotembea nchi nzima hadi vijijini lakini CCM wakiona hivyo wanaona wivu na kuzusha propaganda kwamba tumepata fedha kutoka nje, huo ni woga wao tu,” alisema Dk Slaa.
Alipowauliza wafuasi hao kama wana vitambulisho vya kupigia kura, zaidi ya nusu ya watu waliohudhuria mkutano huo walinyoosha mikono kuonyesha kwamba hawana vitambulisho.
Kufuatia majibu hayo,Dk Slaa akasambaza fomu maalumu za kujaza watu wote wasio na vitambulisho vya kupiga kura.
“Wasio na vitambulisho wajaze fomu hizi ili Chadema iweze kuibana Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) irekebishe daftari la wapiga kura,” alisema Dk Slaa huku akishangiliwa na wafuasi waliokuwa wakimwita rais, rais rais,
Dk Slaa alisema Chadema imejiandaa vya kutosha kuingia Ikulu na kwamba Rais Jakaya Kikwete ajiandae kuliacha jengo hilo waingie kutatua kero za wananchi.
Kwa upande wa Mbunge wa Mbeya Mjini, Mbilinyi alisema Serikali ya CCM itaanguka tu mwaka 2015 kwa sababu imekuwa ikiwasababisha kero nyingi kwa wananchi.


Alisema Serikali imekuwa ikisema inatoa elimu bure wakati mwaka huu ili kumwandikisha mwanafunzi wa darasa la kwanza mzazi anatakiwa kulipia Sh60,000.
“Huu ni uongo wa viongozi wa Serikali wanasema wanatoa elimu bure wakati kuna wazazi wameshindwa kuandikisha watoto wao kwa kukosa kiasi hicho cha fedha,”alisema Mbunge huyo.
Mbilinyi alisema hivi karibuni Serikali imepandisha bei ya umeme na kuendelea kuwasababishia wananchi kero za gharama kubwa ya maisha.
“Kwa mtindo huo Serikali ya CCM inaendelea kujitafutia maadui ambao ni wananchi wanaochoshwa na kero,”alisema Mbilinyi.
Naye Mbunge wa Mbozi Magharibi, David Silinde alisema kitendo cha Serikali kushusha viwango vya ufaulu kwa wanafunzi wa shule za sekondari ni hatari kwa elimu ya Tanzania.
“Kwa kushusha viwango vya ufaulu, wanafunzi wataendelea kuwa wajinga huku rekodi zikionyesha wamefaulu mitihani,”alisema.

No comments:

Post a Comment