Tuesday, 28 January 2014

SAMAHANI KWA PICHA HII...LAZIMA CHOZI LIKUDONDOKE...MTOTO HUYU NASUMBULIWA NA MARADHI YA AJABU TANGU KUZALIWA KWAKE...!

LAZIMA utokwe machozi! Grace John mkazi wa  Mzumbe, Mvomero mkoani Morogoro yupo kwenye wakati mgumu kutokana na maradhi ya ajabu yanayomsumbua mwanaye Honolina Christian Mkude (11).


Honolina anasumbuliwa na ugonjwa wa kuota nyama sehemu za mwili wake zinazofanana na pembe za mnyama, ugonjwa ambao unamtesa tangu kuzaliwa kwake. 

ILIKUWAJE?
Akisimulia kisa kizima, mama mzazi wa Honolina, Bi. Grace, anasema tangu amemzaa mwanaye huyo ni mitihani baada ya mitihani.
 

Mazungumzo hayo yalifanyika hivi karibuni katika kituo cha mabasi ya mikoani, Msamvu, mjini hapa wakati mama huyo na mwanaye wakihangaikia kuchangisha fedha za usafiri wa kwenda Moshi kutafuta tiba zaidi katika Hospitali ya Kilimanjaro Christian Medical Centre (KCMC). 

“Ndugu mwandishi, kwa kweli sijui hatima ya mwanangu. Nilimzaa akiwa ameota nywele sehemu zote za mwili wake, hadi usoni. Mimi na mume wangu tulishangaa, lakini tuliendelea na matibabu katika hospitali mbalimbali maana baadaye alianza kupatwa na uvimbe. 

MTIHANI MWINGINE
“Jamani ndugu yangu... Mungu ana mitihani yake. Mume wangu (Christian Mkude) ambaye ndiye alikuwa tegemeo pekee kwetu, alifariki mwaka 2007 kwa ajali ya gari, wakati akisaka fedha za  matibabu ya mwanetu.
 

“Kifo chake, kwangu kimekuwa pigo mujalabu. Sina pa kukimbilia na hivi juzi tu tulikuwa tumelazwa Hospitali ya Mkoa (Morogoro) na hapo tumepewa barua ya kwenda KCMC kwa matibabu zaidi.

“Hivi unavyoniona nachangisha fedha ili nipate angalau nauli za kutufikisha kwanza hospitalini.  Nimechanganyikiwa kabisa,” alisema Bi. Grace kwa majonzi na kuongeza: 

“Wakati tatizo la mwanangu linaanza sikutegemea kama siku moja angekuja kuwa hivi. Zilianza kuota nywele mwili mzima, baadaye vidonda vikaanza kumtoka na sasa hali imebadilika na kuota nyama hizi kubwa kama mapembe kama unavyoona.” 

SAUTI YA BI. GRACE KUTOKA MOSHI
Misaada ya fedha kidogo alizopata kwa wasamaria wema waliomuona Msamvu, ulimsaidia mama huyo kusafiri hadi Moshi na kufika katika Hospitali ya KCMC.


Akizungumza kwa njia ya simu kutoka Moshi, Bi. Grace alisema: “Nawashukuru waliniosaidia, tumefika salama na mwanangu hapa KCMC, ndiyo tumeanza taratibu za matibabu.” 

BADO ANAHITAJI MSAADA
“Madaktari wametupa moyo, wamesema watajaribu kumsaidia mwanangu. Watamtoa hizo nyama ila kwa sababu kutabaki na mashimo lazima wapandikize nyama nyingine. 


“Tumeshakubaliana kuwa mimi ndiye nitakayekatwa sehemu ya nyama kutoka kwenye makalio yangu kwa ajili ya kumsaidia mwanangu,” alisema Bi. Grace, kilio kikisikika kwenye simu. 

Akaongeza: “Wameshachukua nyama za mwanangu na kwenda kupima na baadaye watachukua zangu ili kuona kama zinaendana, upasuaji ufanyike. Gharama kwa ajili ya matibabu hayo wamesema ni shilingi 400,000 na mimi sina uwezo.

“Watanzania wenzangu, naombeni mnisaidie ili niweze kuondokana na hili tatizo. Mimi ni mjane na sina kazi ya kueleweka, napigania uhai wa mwanangu. Naombeni msaada wenu,” alisema. 


 SHIRIKI BARAKA
Kumsaidia mhitaji wa kweli huongeza baraka katika kipato, vitabu vitakatifu vinaeleza wazi. Ndugu wasomaji wetu wapenzi, kwa yeyote atakayeguswa na mateso ya familia hii, anaweza kumsaidia chochote mama huyo kupitia simu zake namba 0719 749542 (Tigopesa) na 0762 425973 (M - pesa).


No comments:

Post a Comment