Sunday, 21 April 2013

HISTORIA YA WACHAGA

Wachagga ni kabila la watu wenye asili ya Kibantu wanaoishi kaskazini mwa Tanzania chini ya mlima Kilimanjaro, mkoani Kilimanjaro. Shughuli kubwa ya Wachagga ni biashara na kilimo.
Wachagga ni kabila la tatu kwa ukubwa nchini Tanzania. Takwimu za mwaka 2003 zinaonyesha kuwa idadi ya Wachagga mkoani Kilimanjaro ni 200,000.

Vikundi vya Wachagga

Wachagga wana historia ndefu ya asili yao na maingiliano yao na makabila mengine. Kabila la kichagga ni mkusanyiko wa makabila madogo madogo (ya Kichagga) yaliyosambaa kijiografia kuzunguka mlima Kilimanjaro kuanzia Mashariki Tarakea, Rombo hadi magharibi ya Kilimanjaro Siha, Machame. Makabila ya Kichagga ni Wa-Rombo, Wa-Marangu,Wa-Kilema, Wa-Old Moshi, Wa-Kibosho, na Wa-Machame. Makundi mengine madogo ya wachagga ni Wakirua-Vunjo, Wa-Uru, na Wa-Siha.

 

Lugha ya Kichagga

Lugha ya Kichagga, inabadilika kuanzia unapotoka Tarakea mpaka unapofika Siha magharibi mwa Kilimanjaro. Kutokana na tofauti hizo Kichagga kimegawanyika katika Kirombo, Kimarangu, Ki-Old Moshi,Kikibosho, Kimachame, Kikirua na Kisiha. Lugha hizi zinakaribia kufanana kulingana na jinsi makabila hayo yalivyopakana. Kwa mfano, Ki-Old Moshi kinafanana na Kikirua, ambacho nacho kinafanana kidogo na Kimarangu. Vile vile Kisiha kinafanana sana na Kimachame ambacho pia kinafanana kidogo na Kikibosho. Baadhi ya Wamachame walihamia sehemu za Meru Arusha na kuchanganyikana na Waarusha, lugha yao ikabadilika kidogo na kuwa Ki-meru. Kwa sababu hii Wameru wanasikilizana sana na Wamachame ingawa lafudhi zao zinatofautiana kidogo.

Historia ya elimu kati ya Wachagga

Wachagga wanajulikana kwa uwezo wao mkubwa wa kufanya biashara na pia kilimo. Moshi ni maeneo ya mwanzo ambayo Wamisionari wa Kikristo walijenga makanisa na shule. Sababu hii imefanya Wachagga kuwa kabila lenye watu wengi zaidi walio na elimu ya kisasa na mkoa wa Kilimanjaro unaongoza kwa idadi ya shule za sekondari nchini Tanzania. Kulingana na takwimu za elimu mkoa wa Kilimanjaro una shule za sekondari zaidi ya 320. Pia mkoa una shule za msingi zipatazo 950. Idadi hii ya shule ni kubwa zaidi ya idadi ya shule katika mikoa mingine Tanzania.
Shule nyingi za sekondari ziko katika mkoa huu kwa sababu zifuatazo: 1) Hali ya hewa na vivutio vya kitalii katika mkoa huu viliwavutia zaidi walowezi na wakoloni na kuweka makazi yao hapo. Hivyo wamishinari walijenga shule za kwanza wakifuatiliwa na serikali za wakoloni 2) Serikali ya Tanzania ilirithi shule zilizojengwa na wakoloni 3) Wachagga waliobahatika kupata fedha binafsi baadaye waliwekeza kwenye ujenzi wa shule binafsi kama kitega-uchumi. Wakati wakazi wa mikoa mingine walisubiri serikali iwajengee shule. 4) Ukichanganya sababu 1,2 & 3 utagundua shule katika mkoa Kilimanjaro vimezidi sana idadi ya shule katika miko mingine yote.
Ni vema pia kusema kwamba shule hizi kuvutia wanafunzi kutoka Tanzania nzima, haziwasomeshi wachagga tu.

Kilimo na chakula

Wachagga hulima mazao ya chakula kama vile mahindi, maharagwe,viazi, ndizi, ulezi na mboga mbalimbali. Mazao ya biashara kama vile kahawa, nyanya na vitunguu.


Ndizi za Wachagga

Ingawa wachaga wa leo wanakula vyakula mbali mbali kama vile ugali, wali na viazi, chakula kikuu cha Wachagga ni ndizi. Kuna ndizi za aina mbalimbali na hutumika kwa matumiza tofauti. Mfano ndizi kisukari ni fupi na huachwa hadi ziive na huliwa mbivu kama tunda. Ndizi mshare kukatwa zikiwa mbichi na kupikwa chakula mbalimbali pamoja na nyama ya ngombe, kondoo au mbuzi. Mara nyingine hupikwa na maharage, choroko,kunde au hata maziwa ya mtindi. Vyakula vya ndizi huja kwa ladha tofauti kama vile ndizi nyama, mtori, machalari, kiburu na kadhalika.
Aina nyingine ni ndizi-ngombe ambazo huachwa ziive halafu humenywa na kutumiwa kutengenezea pombe maarufu iitwayo mbege. Mbege hutengenezwa kwa kutumia ndizi mbivu, maji, na ulezi.
Aina nyingine ni ndizi-mzuzu. Hizi zikikomaa huachwa zianze kuiva kidogo halafu huchomwa na kuliwa kama kitafunwa pamoja na chai au pombe. Ukipita mitaa ya Darisalamu utaona ndizi- mzuzu zikichomwa sambamba na muhogo au kuku-vumbi au kiti-moto.

Wachagga na muhogo

Inasemekana kuwa "mchagga halisi, hali muhogo - akila muhogo atakufa". Usemi huu umetokana na historia ya mababu kuwa wachagga waliopanda mihogo Kilimanjaro enzi za kale walikufa baada ya kuila. Historia hiyo yaweza kuwa ya ukweli kwa sababu aina nyingi za mihogo zinajenga sumu ya sianidi ndani yao; watu waliozoea kutumia mihogo huwa na njia za kuondoa sumu kwa kwa kuiloweka mihogo katika maji kwa muda. Lakini kama Wachagga wale wa zamani hasa wa Machame walifanya jaribio bila kujua mbinu ya kuondoa sumu ajali iliweza kutokea. Cha kushangaza ni kwamba huko huko Kilimanjaro, majirani na watani wa wachagga yaani Wapare walikuwa wameshazoea mihogo na ilikuja kuwa moja ya chakula chao kikuu.

Ulaji kiti-moto

Pamoja na kilimo cha mazao, wachagga hupendelea sana kufuga nguruwe. Tabia ya kula nyama ya nguruwe ijulikanayo leo kwa jina la "kiti moto" ni moja ya mambo yaliyoenezwa na wachagga. Ulaji wa "kiti moto" haukupendeza baadhi ya wenyeji wa Pwani kama Dar es Salaam ambapo wachagga walihamia, kwani wakaaji wengi wa Pwani ni Waislamu kwa hiyo nguruwe kwao ni haramu. Wakazi wa Dar es Salaam watokao makabila mengine na wasiyo waisalmu kwao kula nguruwe ilikuwa "ruksa".

Majina ya Kichagga

Majina ya kiukoo ya Kichagga pia huashiria wanatoka sehemu gani ya Uchaga, japo si lazima kuwa hivyo: mfano familia maarufu za Kichagga nchini Tanzania ni kama Kimaro, Swai, Massawe, Mushi, Lema, Urassa, Nkya, Ndosi, Meena hutoka Machame. Akina Temu, Mlaki, Mlay, Lyimo, Moshiro, Mselle, Kileo, Kimambo, Tesha wanatoka Old Moshi na Vunjo. Kavishe,Mariki, Tarimo, Laswai, Mallya, Mrema, Mkenda, Massawe, Lyaruu, Makyao, Mowo, Lamtey, Tairo, Mramba, Kauki wanatoka Rombo. Sawe, Usiri, Shayo, Kiwelu, Makundi, Urasa, Mtui, Moshi, Meela, Minja, Njau wanatoka Marangu na Kilema. Rite, Makule, Minja, Mashayo, Chao, Shao, Makawia, Ndesano, Kimario, Tilla, Mariale, Tarimo, Mafole, Kituo, Mrosso, Lyakundia, Kessy, Mmbando, Matemba, Ndenshau, Morio, Akaro, Matowo, Towo, Mkony, Temba na kadhalika hutoka Kibosho.
Wachagga wengi hupenda kurudi nyumbani kipindi cha Krismasi, ikiwa ni kuwatembelea wazazi wao, rafiki, au ndugu. Ingawa wengi hudhani kwamba Wachagga wameathiriwa sana na dini ya Ukristo kwa kuwa wengi wao ni Wakristo na hiki huwa ni kipindi cha likizo kwao, inaaminika pia kuwa kurudi kwao Uchagani wakati wa Krismasi ni pamoja na kutembelea ndugu zao na kujumuika pamoja katika kuumaliza mwaka baada ya kazi nyingi za kutafuta pesa kwa mwaka mzima.


Utawala wa jadi ya Wachagga

Watawala wa kichagga waliitwa "Mangi". Hawa walihodhi mashamba, ngombe na waliheshimiwa kama viongozi wa kikabila. Walikuwa na nguvu za kisiasa na utajiri. Baadhi ya ma-mangi mashuhuri katika historia ni kama Mangi Rindi aliyeingia mikataba na wakoloni (wajerumani), Mangi Sina wa kibosho - anajulikana kwa uhodari wake wa vita katika kupigana na wamachame na kupora ngombe na mazao yao na Mangi Marealle wa Marangu na Vunjo. Wakoloni walipokuja Kilimanjaro waliingia mikataba na viongozi hawa wa kikabila ili kuweza kuweka misingi yao ya kikoloni. Pia ndugu na watoto wa ma-Mangi walikuwa wa kwanza kupata elimu ya kikoloni, kwa hiyo waliweza kushirikishwa katika serikali za kwanza. Hawa pia wanaaminika walikuwa ni kama mabepari wa kwanza wa ki-jadi, maana walifanyiwa kazi na watu wengine wakati wao ma-mangi wamekaa kuhesabu mali zao. Usemi maarufu wa "u-Mangi-meza" inawezekana kuwa umetokana na watawala hawa wa kichagga.

Ardhi

Ingawa ardhi ni msingi wa maendeleo kwa watu wote, kwa wachagga, ardhi ni mali sana kwa sababu kilimo chao ni cha mazao ya kudumu kama kahawa na ndizi hukaa shambani kwa muda wa miaka mingi. Mojawapo ya urithi wapewayo watoto ni "kihamba". Hii ni sehemu ya ardhi ambayo mtoto anategemewa atajenga na kuanzisha familia yake. Bahati mbaya watoto wa kike walikuwa hawapewi kipaumbele katika ugawanaji wa vihamba. Uhaba wa ardhi uchagani ulipelekea wachagga wengi kuhamia mikoa mingine. Hivi leo utakuta wachagga wakiishi Dodoma, Morogoro, Iringa, Mbeya nk wakiwa wamepanda migomba yao na kuendesha biashara za maduka ya vyakula. Ukienda kwenye mikoa hii utakuta wamejenga jamii zao na vyama vyao vya kusaidiana wakati wa sherehe au matatizo. Aidha hata pombe ya mbege utaweza kuikuta katika makusanyio ya wachaga mikoani mbali mbali.

Maoni juu ya Wachagga

Ingawa wanaume wa kichagga hupendelea kufanya kazi mbali na kwao, wake zao hukaa nyumbani (Moshi) na hufuga ngombe na kazi za shambani. ila kwa sasa kutokana na ugonjwa wa ukimwi tabia hii imepungua miongon mwao. Wanawake wa kichagga (hasa kutoka Rombo) hujulikana kama wafanyakazi hodari. Huchangia sana katika mapato ya nyumbani na chakula. Ingawa kipato cha wachaga ni kikubwa kulinganisha na cha makabila mengine, takwimu zinaonyesha watoto wa mkoa wa Kilimanjaro kuwa kuongoza kwa utapiamlo. Sababu kubwa ya watoto kuwa na utapiamlo kunatokana na wazazi kujali zaidi kazi kuliko muda wa kuwahudumia watoto. Wengi wa wototo ni wale ambao wazazi wao ni watu wapombe na kipato chao kinaishia kilabuni. Utaona kwamba uchagani kuna vilabu vingi vya pombe na vinaongezeka kwa sababu imekuwa nibiashara kubwa. Karibu kila kaya kumi natano kuna kila cha pombe na kiwango cha chini kabisa cha pombe inayouzwa kwa siku katika vilabu hivyo si chini ya dede sita au lita mia moja. Pombe ni sababu moja ya watoto kuwa na utapiamlo Hii inawezekana kuwa matunda ya wazazi kutowalisha watoto wao chakula cha kutosha au chakula bora. Kuna sehemu nyingine za Uchaggani kama Old Moshi na Kibosho ambapo watoto wadogo hupewa pombe ya mbege asubuhi mchana na jioni. Sababu nyingi ni kazi; mama wa kichagga anaweza kushinda shambani kutwa na hawana desturi ya kubeba watoto mgongoni kwenda nao shambani hivyo wanakuwa nyumbani ama wenyewe au na mayaya. Mfano ulio dhahiri ni nyakati za asubuhi na mapema kwenye vyombo vya usafiri karibu robo tatu ya abiria ni wanawake wakienda katika shuguli za kibiashara na kilimo na vivyo hivyo nyakati za jioni wakirudi majumbani. Hao ni nje ya wale wanaotumia usafiri wa miguu ambao ni wengi zaidi. Pia baadhi ya wamama wa kichaga wanawajali waume zao zaidi kwani nyama nzuri ni ya baba. Kuepuka gharama baba ataandaliwa chakula kizuri tofauti na chakulawalichoandaliwa watoto japo ni chakula kilekile.

No comments:

Post a Comment