Mazingira ni jambo lingine linaloathiri
afya. Iwapo maji tunayokunjwa na kutumia ni safi na salama, iwapo hewa
tunayovuta si chafu, maeneo tunayofanyia kazi ni salama na pia nyumba
tunazoishi, basi afya zetu huwa salama zaidi ikilinganishwa na watu
wanaoishi kwenye maeneo yasiyo na maji safi na salama au kuvuta hewa
chafu na kufanya kazi kwenye mazingira ya hatari. Uchunguzi uliofanywa
na chuo kikuu cha Zuyd nchini Uholanzi umeonesha kwamba, kuvuta hewa
iliyochafuliwa kwa gesi za magari kwa lisaa limoja kunatosha kumpatia
mtu mfadhaiko wa kifikra au stress katika ubongo wake. Utafiti mwingine
uliofanywa na chuo kikuu cha India cha Purdue umebainisha kuwa, sumu
kali inayotokana na sumu ya risasi, inayoweza kuiingia mwilini mwa
binadamu kutokana na kula vitu vilivyoingiwa na sumu hiyo, nchini
Marekani huathiri maelfu ya watoto kuliko kiwango dhaifu cha sumu hiyo
kinachoweza kuwepo katika vifaa vya kuchezea na mapambo
yanavyosafirishwa.
Afya ya binadamu pia huweza kuathiriwa
na watu wanaomzunguka. Iwapo una familia unayoiangalia au marafiki
katika jamii yako, basi una nafasi kubwa ya kuimarisha afya yako kuliko
mtu ambaye anaishi pekee au hana familia na marafiki. Uchunguzi
uliofanywa na chuo kikuu cha Washington nchini Marekani umegundua kuwa,
ushirikiano wa kifamilia ni jambo zuri kwa mtu na hupunguza kesi za atu
kujiua, hasa wale wanaopatwa na matatizo ya mfadhaiko wa kifikra au
wanapokuwa na fikra ya kutaka kujiua. Vilevile tamaduni, mila na
desturi za jamii na jinsi watu wanavyozithamini itikadi hizo, zina
mafasi kubwa katika afya zao ingawa matokeo yake huweza kuwa mazuri au
mabaya. Kwa mfano mazoea na mila ya kuwakeketa au kuwatahiri watoto wa
kike na wanawake ina madhara makubwa kama vile kuongeza kiwango cha
maambukizo ya magonjwa na hata matatizo ya kiakili miongoni mwa
wasichama na wanawake wanaofanyiwa jambo hilo. Utafiti uliochapishwa
katika Jarida la Afya ya Jamii na Elimu ya Magonjwa ya Mlipuko
umebainisha kuwa, wakati vijana wanapovaa mavazi kwa mujibu wa mila na
tamaduni za makundi au makabila yao, suala hilo huweza kuwapunguzia
uwezekano wa kupatwa na matatizo ya kiakili baadaye maishani.
Urithi wa jenetiki ni suala jingine linaloathiri afya za watu. Kuishi
muda mrefu, siha ya mwili kwa ujumla na kupatwa na baadhi ya magonjwa na
hata kuzaliwa nayo, ni masuala yanayoainishwa na jinsi jeni zetu
zilivyo mwilini tangu wakati tunapozaliwa. Mambo mengine ni pamoja na
vyakula tunavyokula, harakati zetu kifizikia, tabia na mazoea tofauti
kama kuvuta sigara au kunywa pombe na kutumia madawa ya kulevya. Pia
jinsi tunavyoweza kuvumilia mfadhaiko wa kifikra au stress yote hayo
yana nafasi muhimu katika uzima wetu kimwili na kiakili. Suala jingine
tunaloweza kulitaja hapa ni matumizi ya vituo vya afya na hospitali.
Jamii ambayo ina vituo vya afya vya kutosha, vilivyo vizuri na vyenye
kukidhi mahitaji ya watu wa jamii hiyo, watu wake wana nafasi zaidi ya
kuwa na siha nzuri kuliko jamii au watu wanaoishi maeneo ambayo hayana
vituo vya afya au hospitali. Kwa mfano nchi zilizoendelea zenye vituo
vya afya na hospitali za kutosha na nzuri, watu wa nchi hizo huishi
maisha marefu zaidi ikilinganishwa na nchi masikini zenye upungufu
katika sekta hiyo. Jinsia ya mtu pia huathiri afya yake. Kuna magonjwa
yanayowapata wanawake zaidi na kuna magonjwa yanayowapata wanaume zaidi.
Hali ya miili ya wanawake hutofautiana na wanaume na hata kazi na
shughuli wanazozifanya pia huweza kuathiri afya zao kwa ujumla. Kwa
mfano, kubeba mimba na kujifungua, kansa ya ovari na kizazi huathiri
afya ya wanawake katika hali ambayo wanaume hupatwa na kansa ya tezi
kibofu na ya korodani. Wakati wa vita wanaume hushiriki kwa wingi kuliko
wanawake na matokeo yake ni kuuawa au kujeruhiwa. Wanawake na wasichana
huenda wakawa wahanga wa vitendo vya utumiaji mabavu dhidi yao na
ukatili kuliko watoto wa kiume na wanaume. Katika baadhi ya jamii watoto
wa kike na wanawake huwa hawapewi fursa ya kupata elimu na kujiendeleza
kama wanaume, suala ambalo huathiri afya zao pia. Tafiti nyingi
zimeonyesha ubaguzi wa kijinsia katika utoaji huduma za afya hata katika
nchi zilizoendelea.
Miongoni mwa mambo muhimu yanayoijenga
afya ya mwanadamu ni kula lishe salama na mlo uliokamilika. Tunaposema
lishe salama na mlo uliokamilika au healthy balanced diet kwa kimombo,
tunamaanisha masuala muhimu mawili. Moja ni kula kiwango kinachotakiwa
cha chakula kwa mujibu wa harakati na hitajio la mwili wako, na pili ni
kula aina tofauti za vyakula vinavyotakiwa ili kuijenga siha ya mwili.
Tunapaswa kufahamu kwamba, kula lishe bora ni suala muhimu linalochangia
kuimarisha afya ya mwili. Lishe salama na iliyokami inamaanisha kula
vyakula tofauti kutoka katika mafungu manne makuu ya vyakula na
kupunguza baadhi ya vyakula katika milo tunayokula kila siku.
Aina ya vyakula vinavyopaswa kuwepo
kwenye milo yetu ni pamoja na matunda na mboga kwa wingi. Kiwango cha
kutosha cha wanga kama vile mkate, wali, viazi, pasta na vinginevyo na
ni bora viwe vinatokana na aina mbalimbali za nafaka kamili
zisiokobolewa. Maziwa na vyakula vinavyotokana na maziwa kama mtindi na
jibini. Vyakula vyenye protini kama vyama, samaki, mayai, maharagwe na
vinginevyo na vilevile kiasi kidogo cha sukari , mafuta na chumvi.
Ufuatao ni ushauri au vidokezo muhimu
(tips) kuhusiana na namna ya kula vyema ili kuzilinda na kuziimarisha
afya zetu. Tunashauriwa mlo tunaokula uwe na kiasi cha kutosha cha
wanga, kwani aina hiyo ya chakula huipa miili yetu nguvu. Tunashauriwa
kula matunda na mboga kwa wingi kila siku. Baadhi wanasema, ni bora kula
aina 5 za matunda tofauti na mboga kwa siku. Pia tunashauriwa kula
samaki kwa wingi kwa uchache mara mbili kila wiki na kama hatutoweza
kufanya hivyo au kwa wale ambao samaki wanawadhuru na wale wasiokula
nyama, wanapaswa kula virutubishi muhimu vinavyotupatia mada
zinazopatikana kwenye samaki kwa ajili ya afya ya miili yetu.
Tunashauriwa kupunguza kwa kiasi kikubwa sukari na mafuta katika milo
yetu. Vilevile tunashauriwa kula chumvi kwa kiwango kidogo, isizidi
gramu 6 kwa siku kwa watu wazima. Tunapaswa kufahamu kuwa, baadhi ya
vyakula tayari vina kiwango cha chumvi ndani yake kwani karibu theluthi
moja ya chumvi katika milo yetu hutoka katika vyakula ambavyo tayari
vimeshatengeneza kama supu iliyo tayari, sosi, mikate, asusa (snacks),
pai, pizza vyakula vinavyosindikwa na kuhifadhiwa. Hivyo kuna umuhimu wa
kula vyakula hivyo kwa kiasi kidogo. Hii ni kwa sababu ongezeko la
chumvi mwilini huweza kumfanya mtu apatwe na shinikizo la damu, hali
ambayo huweza kusababisha ugonjwa wa moyo na kiharusi. Suala jingine
tunalopaswa kuzingatia ni kunywa maji ya kutosha, tunashauriwa kila siku
kunywa kiasi cha gilasi 6 hadi 8 za maji au vyakula vingine vya
majimaji kama juisi na kadhalika, ili kuzuia upungufu wa maji mwilini.
Maji yana faida nyingi na baadhi yake ni kuusaidia mwili kuondoa kwa
urahisi sumu na mabaki yasiyotakiwa mwilini. Kusaidia kulainisha macho
na maungio ya mwili na pia hutusaidia wakati wa kumeza.
Jambo jingine tunaloshauriwa ni kuupa
mwili harakati, mazoezi ya mara kwa mara na kuwa na uzito unaotakiwa
kiafya. Jengine ni kutoacha kula kifuangua kinywa. Tunatakiwa kustaftahi
kila siku kwa sababu chakula hicho cha asubuhi huupa mwili nguvu ya
kuanzia siku na huamsha utendaji kazi wa mwili kwa ajili ya siku nzima.
No comments:
Post a Comment