Thursday, 16 May 2013

Mawaziri wa JK wakingiana vifua Bungeni

 
Rais wa Serikali ya awamu ya nne Tanzania Jakaya Kikwete akitafakari jambo.

WAKATI  Kauli ya Serikali iliyotolewa bungeni juu ya kufutwa kwa matokeo ya mtihani wa kidato cha nne na sababu za kufeli kwa wanafunzi wengi, ikiendelea kuzua hoja mbalimbali ndani ya Bunge na Nje ya Bunge la Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Waziri Mkuu Mizengo Pinda leo ameendelea kumkingia kifua Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Dk Shukuru Kawambwa.
Akijibu maswali mbalibali katika kipindi cha maswali na majibu Bungeni leo, Waziri Mkuu Pinda alisema kwamba ni mapema sana kuchukua hatua ya kumwajibisha waziri husika kwa sababu Tume aliyounda kuchunguza chanzo cha kufeli kwa wanafunzi bado wanaendelea na kazi yao.
"Jamani inabidi kwanza tusubiri tume iliyoundwa ituletee majibu sahihi na mapendekezo ya jinsi ya kutatua tatizo hili, pili sidhani kwamba kuwajibisha watendaji katika suala hili ni jambo la busara kwa sababu tatizo hili ni kubwa sana na linaguza nchi nzima"alisema Waziri Mkuu katika moja ya majibu yake Bugeni.
Hata hivyo wakati mjadala huo ukizidi kuvuta hisia za watanzania mbalimbali ndani na nje ya nchi, imebainika kwamba Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ilibariki mabadiliko ya mfumo mpya wa kupanga madaraja.
Taarifa ya Serikali iliyosomwa bungeni Mei 3, mwaka huu na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi ilisema Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), lilifanya mabadiliko ya mfumo bila kushirikisha wadau.
“Baraza la Taifa la Mitihani lilikuwa linachakata alama za mwisho kwa kutumia mfumo ambao ulikuwa unabadilika kwa kutegemeana na hali ya ufaulu wa mwanafunzi... lakini mwaka 2012 lilitumia mfumo mpya wa kuwa na viwango maalumu vya kutunuku (fixed grade ranges).”
“Tume imebaini kwamba, pamoja na mfumo huo kuandaliwa kwa nia nzuri, utaratibu huo mpya haukufanyiwa utafiti na maandalizi ya kutosha kabla ya kutumika. “Baraza la Taifa la Mitihani limeelekezwa kuzingatia kuwa pamoja na kwamba sheria ya kuanzishwa kwake inawaruhusu kufanya marekebisho ya mchakato wa mtihani, lakini marekebisho yoyote ya kubadilisha utaratibu wa kupanga viwango vya ufaulu na madaraja ya matokeo ya mtihani lazima yahusishe wadau wote wanaohusika na mitalaa, ufundishaji na mitihani.”

No comments:

Post a Comment