WAPENZI
wanagombana, ndoa zinavunjika na familia nyingi zipo kwenye msoto kwa
sababu ya ubinafsi. Tunazungumza mengi lakini ukweli ni kwamba endapo
kila mmoja atafanikiwa kuushinda ubinafasi, upendo utashamiri kila kona.
Ubinafsi
una matawi mengi. Mtu anaposaliti, maana yake ametekwa na tamaa
binafsi. Anashindwa kutambua kwamba yeye ni mpenzi wa mtu, kwa hiyo
anatakiwa kulinda penzi la mwenzake. Hajui kama anachokifanya ni dhuluma
ya hali ya juu.
Ukweli
ni kwamba unapoanzisha uhusiano na mtu, maana yake umeamua kumchagua
yeye ndiye amiliki penzi lako. Kwa hiyo ukienda kulitoa kwa mwingine,
huo ni ubinafsi. Umeingiwa na umimi kwa kuona kwamba unatoa rasilimali
za ndani ya mwili wako mwenyewe.
Kwa
nini ukimfumania mwenzi wako panachimbika? Ni kwa sababu alichokitoa
kwa mtu mwingine ni chako, kwa maana hiyo amekutendea dhuluma. Ndiyo
maana ukawa na jeuri ya kupigana kwa sababu haki yako imetumika ndivyo
sivyo.
Hivyo
basi, usaliti ni ubinafsi. Umeingiwa na jeuri kwamba unacho ndani ya
mwili wako, kwa hiyo unaweza kukitumia bila kumshirikisha mwenzi wako.
Hiyo ni tabia mbaya mno. Kabla ya kusaliti, fikiria
utakavyoumia pindi utakaposalitiwa.
Kama
inauma, ni kwa nini umtende mwenzako? Je, umemuona yeye hana moyo? Anza
leo kukemea ubinafsi. Popote pale utakapoona unachukua nafasi, upinge
kwa sababu ni adui mkubwa mno kwenye mapenzi. Siku zote usiseme “nipo”,
sema “tupo”.
Unapozunguka,
usiwaze “upo”, unatakiwa kuwaza “mpo”. Hii itakusaidia kulinda siti ya
mwenzako kila utakapokwenda. Hakikisha nafasi ya mwenzi wako
haichafuliwi au kutolewa mkopo. Kama ilivyo kwenye soka, wachezaji
huchezea timu nyingine kwa mkopo ndivyo na mapenzi ya sasa yalivyo.
Ni
kweli mtu ana mpenzi wake lakini anavyojieleza anatoa picha kwa
muulizaji kuona kwamba aliyepo si muhimu sana. Hii husababisha muulizaji
aombe kukaa na baadaye hukaribishwa. Wengi walikaribishwa kwa mkopo,
mwisho wakawa wamiliki wa jumla.
Kwa
nini umwambie huyo mtu kwamba anaweza kukaa, wakati unajua siti ina
mmiliki wake halali? Kwa porojo za kitoto, eti mnaambiana mfanye siri.
Kinachosikitisha ni kwamba ukisikia na mwenzako naye kagawa siti yako
kwa mwingine, macho yatakutoka kwa hasira.
Si
wakati wa kuchukia unapotendwa, bali unatakiwa uache ubinafsi. Haliitwi
penzi bila kuwepo watu wawili. Lazima uhakikishe unalinda la mwenzako
ili na lako lilindwe. Somo la mkuki kwa nguruwe kwa binadamu mchungu,
linafundisha kuacha ubinafsi. Mfikirie mwingine.
Kama
ambavyo ubinafsi unavyowatesa wananchi pale kiongozi mwenye dhamana
kiserikali anaposhindwa kutimiza majukumu yake na kuamua kushughulikia
shida zake binafsi, huku akitumia rasilimali za umma, ni kirusi hatari
kila upande.
Baba
anapoamua kufuja fedha wakati anajifahamu anayo familia inayomtegemea,
huo ni ubinafsi. Anafikiria kutumbua yeye binafsi, wakati anatakiwa
kujenga msingi wa familia. Anashindwa kujua kwamba fedha anazotafuta si
zake peke yake.
Kama
anaona anatakiwa kutumia fedha zake peke yake, basi hapaswi kujipa
mzigo wa kumiliki familia. Mtu anapokuwa baba au mama, uamuzi wake
unatakiwa uwe kwa ajili ya wengi. Kumaliza mshahara kwenye kumbi za
starehe ni ukatili kwa familia hususan mtoto ambaye hakukuomba umlete
duniani.
Usijidanganye
kwamba unajimiliki mwenyewe. Wewe unamilikiwa na familia yako, kwa hiyo
una deni na wajibu mkubwa kwa wale wanaohusika. Kabla ya kwenda nyumba
ya kulala wageni na huyo unayemtamani, fikiria kwamba unamilikiwa.
Baba
au mama, anapokwenda hoteli na mpenzi wa nje. Akakubali kuvua nguo na
kufanya mapenzi. Ajitambue kuwa anachezea maisha ya watu wengine. Kuna
maradhi, kwa hiyo unatakiwa uwe na afya njema ili wanaokumiliki
waendelee kupata huduma yako.
Unafahamu
kwamba mapenzi yanaua. Unaelewa kuwa unaposhindwa kuwa mtulivu
nyumbani, unaiba muda wa familia yako. Kumbe sasa, fedha siyo zako ila
ni za familia. Unaweza kupata picha kwamba viungo ni vyako lakini penzi
si lako. Ukilitoa ni wizi, ni dhuluma iliyopitiliza.
No comments:
Post a Comment