Saturday, 11 May 2013

Watoto waangalia filamu za ngono mitaani...

Uchunguzi uliofanywa na Waandishi wa habari katika mitaa mbalimbali jijini Dar es Salaam, umebaini kuwepo kwa idadi kubwa ya mabanda ya kuonyesha filamu katika makazi ya watu, hivyo kuwapa watoto nafasi ya kutazama picha zisizofaa kimaadili.

Dar es Salaam. Kuwepo kwa mabanda mengi ya kuonyesha filamu yasiyo na usimamizi nchini, kumewapa watoto wadogo nafasi ya kuangalia picha za ngono, huku Serikali ikishindwa kuchukua hatua stahiki ikiwamo kuyafunga mabanda hayo.
Uchunguzi uliofanywa na Waandishi wa habari katika mitaa mbalimbali jijini Dar es Salaam, umebaini kuwepo kwa idadi kubwa ya mabanda ya kuonyesha filamu katika makazi ya watu, hivyo kuwapa watoto nafasi ya kutazama picha zisizofaa kimaadili.
Uchunguzi huo uliofanyika mchana na usiku, umebaini kuwa baadhi ya wazazi huwapa watoto wao fedha kwenda katika mabanda hayo bila kujua aina ya filamu wanazokwenda kuangalia, huku wazazi wengine wakiwa hawana taarifa kuwa watoto wao huingia katika mabanda hayo.
Katika mitaa ya Kigogo na Mburahati, baadhi ya wanawake walikutwa saa tatu usiku wakiangalia filamu kutoka barani Asia huku wakiwa wamebeba watoto wadogo. Sehemu kubwa ya filamu hiyo ilikuwa ikionyesha watu wakishiriki tendo la ndoa.
Msimamizi wa banda hilo (jina tunalo) alipoulizwa alisema: “Hilo ni picha la Amitabh Bachchan.”
Hata hivyo, baada ya kuiangalia video hiyo kwa muda wa zaidi ya dakika 20, ilibainika kuwa filamu hiyo ilikuwa imechanganywa na filamu nyingine tofauti na ile iliyotajwa.
Katika banda moja lililojengwa kwa mifuko ya plastiki katika Mtaa wa Kabojonga, Mtoni Kijichi walionekana wanawake wanne wakiwa wamekaa sakafuni saa tatu usiku, huku wamewapakata watoto wadogo waliokuwa wamelala.
Chumba hicho kilikuwa kimejaa watoto wanaokadiriwa kuwa na umri kati ya miaka mitano hadi 17. Walikuwa wamekaa kimya, wakifuatilia filamu iliyotafsiriwa kwa Kiswahili
Kama ilivyokuwa katika mabanda mengine, watoto hao walikuwa wakiangalia filamu kutoka barani Asia iliyofahamika kwa jina la Train.
Msimamizi wa banda hilo, muda wote alionekana kushika ‘remote control’ kwa ajili ya kusogeza mbele baadhi ya sehemu katika filamu hiyo, ambazo zinaonyesha utupu kitendo kilichowafanya watazamaji kulalamika.
“Ina scratches nyinyi, hamuoni?” alijibu msimamizi wa banda hilo, lakini ukweli ni kwamba alikuwa akitaka kusogeza mbele sehemu inaonyesha watu wakifanya ngono.
Saa nne usiku, katika banda jingine eneo la Mbagala Charambe, watoto wawili walikutwa wakiangalia filamu kupitia tundu lililopo kwenye moja ya kona ya banda hilo lililojengwa kwa turubai kuukuu. Ndani ya banda watu walikuwa wakiangali filamu ya ngono.

No comments:

Post a Comment