Saturday, 11 May 2013

Wanasayansi wagundua njia ya kuangamiza malaria duniani...



Moja ya tahadhari ambayo wanasayansi hao wanaichukua, taarifa hiyo inasema ni kuzuia kimelea wa malaria kujijengea usugu dhidi ya bakteria, Wolbachia..

Dar es Salaam. Wanasayansi nchini Marekani wamegundua aina ya bakteria ambao wana uwezo wa kumfanya mbu awe na kinga dhidi ya vimelea vya malaria.
Kwa kawaida mfumo wa maisha wa vimelea wa malaria hukamilika kwa kuishi kwa mbu na binadamu.
Ugunduzi huo wa wanasayansi utakatisha maisha ya vimelea hao wa malaria wanaofahamika kama Plasmodium na kuweza kuufanya ugonjwa huo unaoongoza kwa kuua watu wengi duniani uwe ni historia.
Wanasayansi hao kupitia taarifa kwa vyombo vya habari iliyosambazwa kupitia mtandao na Taasisi ya Kukabiliana na Magonjwa ya Mzio na Kuambukiza (NIAID),wameeleza kuwa ugunduzi huo unaweza kuzima kabisa tabia ya mbu ya kumwambukiza binadamu ugonjwa wa malaria.
Katika ugunduzi huo ulioongozwa na Dk Zhiyong Xi wa Chuo Kikuu cha Michigan walifanikiwa kubaini dawa itakayotumika kama chanjo kwa mbu anayeeneza malaria ili imfanye atengeneze kinga ya kutokuruhusu vimelea vya malaria kuishi kwenye mwili wake.
Wakijua fika kwamba kimelea wa malaria huanza kuishi kwa mbu aina ya Anopheles kabla ya kuambukizwa kwa binadamu anapomuuma, waliona hiyo ni njia pekee ya kuumaliza ugonjwa huo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, walimtaja bakteria anayefahamika kama Wolbachia kuwa ana uwezo wa kuzuia maendeleo ya Plasmodium kwenye mwili wa mbu.
Kulingana na ugunduzi huo wana uwezo wa kutumia utaalamu wao katika kumfanya bakteria Wolbachia aishi kwa mbu anopheles.  Mbu anayeishi na bakteria huyo wa Wolbachia ataweza kukifanya kizazi chake chote kiishi na bakteria huyo.
Ugonjwa wa malaria unaongoza kwa kuua idadi kubwa ya wat duniani.
 

No comments:

Post a Comment